​​​​​​​Mbunge Kasalali Mageni abwaga manyanga Jimbo la Sumve

Dodoma. Wakati dirisha la wagombea  kuchukua fomu za ubunge na udiwani likihitimishwa jana, Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni ametajwa kuwa miongoni mwa walionyanyua mikono na kusema inatosha.

Mageni ambaye ameongoza jimbo hilo kwa muhula mmoja akipokea kijiti baada ya kifo cha Richard Ndasa, anaweka rekodi ya mbunge aliyeongoza muhula mmoja lakini anaamua kuachia kwa hiyari yake.

Hata hivyo, Bunge litamkumbuka Mageni kama mmoja wa watu machachari ambaye alitishia kuisimamisha bajeti ya Serikali kwa sababu ya ujenzi wa kituo cha mazoezi ambacho kilipaswa kujengwa kwenye jimbo lake lakini ikataka kuhamishiwa Ilemela.

Hoja nne zinabaki kumbukumbu ya michango yake ndani ya Bunge ambazo alitikisa kwa kiasi kikubwa na kuwaweka mawaziri matumbo moto.

Miongoni wa hoja kubwa ni ilikuwa ni suala la ajira ambalo alilizungumza kwa mawanda mapana kiasi cha kuwavuta na wabunge wengine hasa alipohoji juu ya mfumo aliouita mbovu katika kuwapata watumishi.

“Tunalo tatizo kubwa sasa hivi kwenye nchi yetu la wananchi kupoteza imani na mfumo wa ajira serikalini, wabunge wote wamesema humu, tena tunazo meseji mpaka zimejaa kwenye simu, za watu kuomba tuwasaidie kupata kazi Serikalini,” alisema Mageni.

Mbunge huyo alisema watu wamehamisha imani kwa Wabunge, wameondoa kwenye mfumo ajira kutokana na usiri mkubwa akitolea mfano watu wanaomba tume ya ajira ambako kuna kanzidata na huambiwa aliyekosa amewekwa humo lakini ajira ile ile ikitoka hawatumii kanzidata bali wanatangaza upya.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamefika wakati wamegundua kwamba mfumo wa ajira ni wa dili,yaani wananchi wanatupa ujumbe kwamba huko tuna askari wa dili, sasa kama tunataka hivi ni lazima tujifikirie, yaani kuna kitu kwenye mfumo wa ajira wananchi wameshaondoa imani,” alisema.

Kwenye hoja ya kikokotoo, aliitaka Serikali iwape watu fedha zao akisema haiwezekani mtu aliyefanya kazi kwa muda mrefu, amepokea mshahara wake na Serikali haikuhusika na chochote kwenye mshahara wake, leo anastaafu zinakuja habari kwamba hawezi kutunza hela yake.

Hoja hiyo ilivuta hisia za wabunge wengi ambao walisimama na kuiunga mkono wakibainisha kuwa wanapata kelele nyingi wawapo majimboni.

Mageni anaondoka akiacha rekodi ya mapambano baina yake na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Dk Damas Ndumbaro (Waziri wa Katiba) kuhusu mradi wa ujenzi unaojulikana kama Construction of Sports Center of Excellence katika Mji wa Malya uliopo Jimbo la Sumve.

Mradi huo wenye thamani ya Sh13 bilioni, ulisainiwa Julai 6, 2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye alitiliana saini mkataba huo na Kampuni ya CRJE East Africa kwa ajili ya ujenzi wake katika viwanja namba 30, 31 na 32 eneo la Malya, wilayani Kwimba.

Hata hivyo, alisema siku 21 baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela iliandika barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikijibu barua yake ya Juni 2, 2023 ya kuomba eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha michezo, jambo alilolitafsiri kama njama za kukiondoa kituo hicho.

Hoja nyingine itakayomweka kwenye kumbukumbu za kibunge ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.

“Katika nchi hii kuna maeneo ambayo yanabandua lami yanaweka mpya na kuna maeneo ambayo hayana hata milimita moja ya lami kama ilivyo kwa jimbo la Sumve,” alisema

Kwa mujibu wa Mageni, jimbo la Sumve lililoko wilayani Kwimba, halina kabisa lami. Alisema wilaya hiyo ni miongoni mwa zilizoanzishwa kabla hata ya uhuru.

Alitaka ujenzi wa lami kilimoita 71 uguse maeneo ya Magu – Bukwimba – Ngudu mpaka Nhungumalwa kwa kiwango cha lami na kwamba, anashangazwa kuona ahadi hiyo ikiota mbawa tena.

Related Posts