Arusha. Serikali inatarajia kuanzisha biashara ya kuuza wanyama hai kwa mataifa mbalimbali duniani, ikiwa ni juhudi za kuboresha uchumi wa wafugaji pamoja na kukuza pato la taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa jana, Julai 2, 2025, wilayani Longido, mkoani Arusha, na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo katika ngazi ya mkoa.
Amesema kuwa, mbali na faida inayopatikana kupitia uuzaji wa bidhaa za mifugo, hususan nyama, Serikali imeanza majadiliano na nchi za Falme za Kiarabu na Misri kwa ajili ya kuanzisha biashara ya uuzaji wa wanyama hai.
Dk Kijaji ameeleza kuwa biashara hiyo inatarajiwa kuanza mara tu baada ya serikali kupata cheti cha ithibati kutoka Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), ambacho kitakuwa kama kibali rasmi cha kuruhusu shughuli hiyo kufanyika kimataifa.
“Tuko hatua za mwisho kupata cheti hicho, na uzuri tumeshaanza mazungumzo na nchi za Falme za Kiarabu na Misri ambao wameonyesha nia ya kufanya biashara hiyo ya mifugo hai,” amesema.
Amesema kuwa lengo kubwa ni kufungua zaidi masoko ya mifugo kimataifa kwa ajili ya kukuza kipato cha wafugaji na taifa kwa ujumla.
Hadi kufikia Aprili 2025, Tanzania ilikuwa imesafirisha jumla ya tani 9,863.41 za nyama, zenye thamani ya dola za Marekani milioni 44.07.
“Kiasi cha mauzo yetu nje ya nchi kinaweza kuongezeka mara dufu tukipata cheti hicho ambacho kitaiwezesha Tanzania kuingia hadi masoko ya Ulaya.
“Changamoto ilikuwa ni cheti, lakini pia kutokuwa na kampeni za kitaifa za kuchanjwa mifugo yetu badala yake wafugaji walijitegemea kuchanja wenyewe, Pia kutambua taarifa za mifugo yetu ilipo na hali zao hasa kwa usalama wa walaji, ndio maana Rais (Samia Suluhu Hassan) amezindua kampeni hiyo inayokwenda nchi nzima,” amesema.
Mbali na hilo amesema Serikali imeanza kupima na kuyafanyia urasimishaji maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya nyanda za malisho na kuyapatia hati ili kuyalinda dhidi ya matumizi mengine.
Akizungumzia chanjo hiyo amesema Serikali imewekeza zaidi ya Sh216 bilioni kutekeleza kampeni hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.
Mbunge wa Jimbo la Longido, Steven Kiruswa amesema kuwa kampeni hiyo itaisaidia kuongeza thamani ya mifugo yao lakini pia kukuza uchumi wa wananchi wake ambao zaidi ya asilimia 95 wanategemea ufugaji.
“Serikali imefanya mengi kwetu wana Longido, tunachoomba kwa sasa itukumbuke kwenye mabwawa yetu ambayo yamejaa udongo na kutishia kukauka, wakati ndio tegemezi letu kubwa kama vyanzo vya maji kwa matumizi ya nyumbani na mifugo yetu,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi amesema kuwa atahakikisha chanjo hiyo inakwenda kutekeleza katika wilaya zote za Arusha ili kuipa thamani mifugo ya Mkoa huu.
“Tunatambua thamani ya mradi huu na umuhimu wake katika kuhakikisha wafugaji wananufaika nayo hivyo tutakwenda kusimamia vema ulete matunda yaliyotarajiwa”
Mbali na hilo amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kuhamia ufugaji wa kisasa kibiashara kwa kunenepesha mifugo yao michache na kuuza kuliko kufuga wengi wasio na thamani.
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kali amesema kuwa chanjo hiyo iliyoanza leo, imeambatana na vifaa vya kazi ikiwemo pikipiki 12 na vishkwambi.