Tanzania yatoa kauli utafiti ukibaini dawa za saratani bandia, duni Afrika

Dar es Salaam. Kufuatia utafiti mpya ulichapishwa na Jarida la Afya ‘The Lancert Global Health’ umebainika uwepo wa dawa duni na bandia za saratani Afrika, huku Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) ikieleza hatua zinazochukuliwa kufuatia utafiti huo.

Utafiti huo uliochapishwa hivi karibuni kupitia jarida hilo, umeeleza dawa zilizochunguzwa kwa nchi ya Ethiopia, Kenya, Malawi na Cameroon zilikuwa duni au bandia.

Matokeo ya utafiti huo yanamaanisha kuwa, watu wanapewa dawa ambazo huenda zisifanye kazi ipasavyo kutokana na kukosa viambata muhimu vinavyohitajika kudhibiti au kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 3, 2025 namna Serikali ilivyojipanga kuhakikisha usalama wa dawa za saratani kwa wananchi, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Dk Adam Fimbo amesema kupitia kanzidata yao wanaanza kuangalia dawa zilizohusika kwenye utafiti kama zipo soko la Tanzania wazifanyie uchunguzi.

“Tutaangalia kwenye kanzidata zetu kama dawa hizi tumezisajili, kama zipo nasi tupime kama zinakidhi au hazikidhi na zikikidhi zitabaki sokoni na kama hazikidhi zitaondolewa,” amesema.

Fimbo amesema TMDA ina mifumo inayofanya kazi na inatambulika na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutokana na ubora wake.

Amesema TMDA ni taasisi ya kwanza Afrika kuonekana kuwa na mifumo yenye ufanisi mkubwa, akisisitiza pamoja na ubora huo haina maana sokoni hakuwezi kukutwa dawa ambazo hazina ubora.

Mkurugenzi huyo amesema kazi kubwa ya mamlaka hiyo ikishasajili bidhaa inakwenda sokoni na kuchukua sampuli na kuzipima na inapokutana na sampuli mbovu huondolewa sokoni na kama ina ubora huendelea kubaki sokoni.

Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema matokeo ya utafiti huo unategemea na umahiri wa mamlaka za udhibiti wa dawa.

Msasi amesema nchi ambazo utafiti umefanyika hakuna mamlaka ambayo umahiri wake unaweza kuifikia TMDA ndio maana udhibiti unakuwa changamoto.

“Kwetu tunajitahidi kudhibiti, dawa nyingi za saratani wateja huwa wanapenda ya peke yao tunaagiza nje inaletwa sasa hizi ndio zinaleta shida, kwasababu hakuna aliewahi kwenda kukiulizia hicho kiwanda kama kipo kinazalisha,” amesema.

Kundi la watafiti kutoka Marekani na barani Afrika walikusanya taarifa za dozi za dawa, wakati mwingine kwa siri, kutoka hospitali takribani 12 na maduka ya dawa 25 katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kupitia utafiti huo uliochapishwa hivi karibuni kupitia tovuti ya jarida hilo, watafiti walipima takribani aina 250 za sampuli kutoka chapa mbalimbali, takribani asilimia 17 (moja kati ya sita) zilionekana kuwa na viwango visivyofaa zikiwemo bidhaa zinazotumika katika hospitali kubwa.

Kwa mujibu wa wataalamu kwenye utafiti huo, wagonjwa wanaotumia dawa zenye viambata pungufu huona uvimbe wao ukiendelea kukua na kuenea zaidi mwilini.

Ripoti za awali zimewahi kubaini viwango vya juu vya dawa duni za viua vijasumu, dawa za malaria na kifua kikuu, lakini huu ndio utafiti wa kwanza kubaini kiwango kikubwa cha dawa za saratani bandia au zenye dosari zikisambaa katika mfumo wa huduma za afya.

“Sikushangazwa na matokeo haya,” amesema Lutz Heide, Mfamasia kutoka Chuo Kikuu cha Tübingen nchini Ujerumani, ambaye hapo awali amefanya kazi Wizara ya Afya ya Somalia na ametumia zaidi ya muongo mmoja akifanya utafiti kuhusu dawa duni na bandia.

Heide hakuhusika moja kwa moja katika kundi la watafiti waliotekeleza uchunguzi huo, lakini amesema ripoti hiyo imeangazia tatizo ambalo halijawahi kupimwa kwa kina hapo awali.

“Nimefurahishwa kwamba, hatimaye, kuna mtu amechapisha ripoti ya namna hii kwa utaratibu mzuri, hii ni mara ya kwanza kufanyika utafiti wa kina na wa kimfumo kuhusu eneo hili,” amesema.

Mtafiti mwandamizi katika uchunguzi huo Lieberman kutoka Chuo Kikuu cha Notre Dame nchini Marekani, ameiambia Shirika la Habari la Ujerumani DW, zipo sababu  nyingi zinazosababisha uwepo wa  bidhaa zenye ubora duni.

Sababu hizo hujumuisha hitilafu katika mchakato wa uzalishaji au kuharibika kwa bidhaa kutokana na mazingira duni ya kuhifadhi.

Marya amesema baadhi ya dawa kwenye utafiti huo ni bandia kabisa, jambo linaloongeza hatari ya kutokuwepo kwa ulinganifu kati ya kile kilichoandikwa kwenye nembo ya bidhaa na dawa halisi iliyo ndani.

Janga la dawa bandia Afrika

Pia, amesema kutambua bidhaa duni au bandia si jambo rahisi, kwa kawaida, mtaalamu wa afya au mgonjwa anaweza kufanya ukaguzi wa macho tu kwa mfano, kuchunguza lebo ya dawa kuona kama kuna utofauti au kuangalia rangi ya vidonge na sindano kubaini kama bidhaa ni bandia.

Hata hivyo, njia hizo si za kuaminika katika utafiti huo, ni takribani robo tu ya dawa duni zilizobainika kwa njia ya uchunguzi wa macho na zilizobaki ziligunduliwa kupitia uchunguzi wa maabara.

Kwa mujibu wa DW, Marya Lieberman amesema kutatua tatizo hilo kutahitaji kuboresha mifumo ya udhibiti, pamoja na kutoa teknolojia za uchunguzi na mafunzo katika maeneo yanayohitaji huduma hizo.

“Ukishindwa kupima dawa, huwezi kuisimamia kisheria,” amesema.

Ameongeza kuwa dawa za saratani ni ngumu kuzishughulikia na kuzichambua kwa sababu ni sumu kali, na maabara nyingi hazitaki kufanya kazi hiyo.

Hilo ndilo analosema ni tatizo kuu katika nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako waliendesha utafiti.

Ingawa baadhi ya nchi hizo zina maabara nzuri, bado hazina miundombinu ya usalama inayohitajika kwa ajili ya kushughulikia dawa za chemotherapia (matibabu yanayotumia dawa kali kuua seli za saratani).

Daktari wa Magonjwa ya Binadamu Hospitali ya Rufani Kanda ya Mbeya, Ernest Winchislaus amesema uwepo wa dawa duni za kutibu saratani ni tishio kubwa kwa juhudi za kukabiliana na saratani.

Amesema hali hiyo hupunguza ufanisi wa matibabu, huathiri matokeo ya wagonjwa, na pia hupunguza imani ya wananchi kwa mifumo ya afya.

“Ni muhimu kuimarisha uwezo wa taasisi za udhibiti wa dawa, kuweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa usalama wa dawa (pharmacovigilance),

Kushirikiana na taasisi za kimataifa kama WHO na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa kitaifa wa uchunguzi wa ubora wa dawa, hasa kupitia maabara na mifumo ya kitaalamu,” amesema.

Dk Winchislaus amesema ushirikiano huu unaweza pia kusaidia katika kujenga uwezo wa wataalamu wa afya kupitia mafunzo ya mara kwa mara na kubadilishana ujuzi.

Sambamba na hilo, amesema ni muhimu kuielimisha jamii na watoa huduma za afya kuhusu hatari za dawa duni.

Amesema kupitia kampeni za uhamasishaji wa hudumu za afya, wananchi wanapaswa kupewa taarifa sahihi zitakazowawezesha kutambua dalili za dawa zisizo na ubora unaotakiwa,

Mtazamo huo wa kitaalamu hautofautiani na ule unaotolewa na daktari wa binadamu, Anwar Mohamed aliyesema mgonjwa anapaswa kutumia dawa kwa ushauri wa wataalamu wa afya.

“Daktari ndio akuandikie dawa na ndio ahakikishe unatumia ipasavyo ukienda kununua dawa ambayo uliwahi kutumia ni changamoto kwa afya yako, kwani unaweza kupewa isiyo sahihi kwako,” amesema Dk Mohamed.

Related Posts