Uislamu unahimiza kusaidiana na kushirikiana ili kujenga jamii yenye huruma, haki na mshikamano wa kweli.
Hakika, haifichiki kwa mwenye akili timamu kwamba jamii inayojengwa juu ya ushirikiano na mshikamano, yenye mapenzi ya kipaumbele na undugu miongoni mwa watu wake, huwa ni jamii imara, iliyostawi na iliyojengeka.
Jamii ya aina hii haiwezi kubomolewa na yeyote, wala haitetereki kwa sababu ya misukosuko ya wakati. Kama Allah alivyosema: “Na saidianeni katika wema na uchamungu, wala msisaidiane katika dhambi na uadui…..”(5: 2).
Katika Uislamu, mshikamano wa kijamii unamaanisha kuwa mtu mwenye uwezo anatakiwa awajibike kwa wale wasiokuwa na uwezo katika jamii.
Bila shaka, kuna hali nyingi katika jamii zinazohitaji msaada wa dharura. Huyu ana njaa na anahitaji chakula, yule ni mgonjwa na anahitaji matibabu, mwingine hana makazi au mavazi au blanketi, au anahitaji elimu.
Mtume wa Allah (Rehema na amani ziwe juu yake) amesema: “Muislamu ni ndugu ya Muislamu mwingine, hamdhulumu wala hamtelekezi. Na atakayesaidia haja ya ndugu yake, Allah naye atatimiza haja yake. Na atakayemuepusha Muislamu na dhiki, Allah atamuepusha na dhiki miongoni mwa dhiki za Siku ya Kiama….”
Mtume pia alithibitisha kwa maneno makali na ya wazi kuwa jamii nzima ina wajibu wa kumsaidia kila mtu mwenye uhitaji. Akasema:“Si muumini anayeshiba huku jirani yake ana njaa pembeni yake.”
(Bukhar)
Maswahaba wa Mtume walikuwa wakisaidiana kwa dhati walipokumbwa na dhiki. Mfano katika mwaka wa njaa kali (Ar-Ramadah), mwishoni mwa mwaka 17 na mwanzoni mwa 18 Hijria, wakati wa ukhalifa wa Umar bin Khaṭṭāb, ardhi ilikauka kwa sababu ya ukosefu wa mvua hadi ikawa kama rangi ya majivu.
‘Umar Khaṭṭab aliapa kutokula mafuta wala nyama hadi mtihani huo utakapokwisha. Al-Ḥafidh Ibn Kathir anasema:
“‘Umar aliizunguka Madina usiku mmoja katika mwaka wa njaa, hakukuta mtu yeyote anayecheka, wala watu wakizungumza katika nyumba zao kama kawaida. Hakukuwa hata na ombaomba. Alipouliza sababu hiyo, akaambiwa: ‘Ewe Amir wa Waumini, waombaji waliomba lakini hawakupewa, wakakata tamaa ya kuomba…’”
Hali hii ilikuwa ni dhiki ambayo mtu mmoja hangeweza kuikabili peke yake. Ilikuwa ni lazima kwa jamii nzima kushirikiana ili kukabiliana nayo.
Kwa hiyo, Khalifa Umar aliomba msaada kwa Amr bin al-Aṣ gavana wa Misri: Naye akatuma misafara ya chakula. Magavana wengi wa miji ya Kiislamu pia walifanya jambo hilo. Hivi ndivyo Muislamu anavyopaswa kuwa wakati wa dhiki na majanga kuwasaidia wenzake.
Mtume wa Allah alitoa mifano bora kabisa ya kupenda kheri kwa watu na kuwasaidia wahitaji. Mfano hai ni kisa chake na Jabir bin Abdillāh, mmoja wa Maswahaba wakubwa, ambaye baba yake aliuawa katika Vita vya Uhud.
Baba yake alimwachia Jabir dada zake saba, ambao hawakuwa na mlezi isipokuwa yeye peke yake, pamoja na deni kubwa lililokuwa mzigo kwa kijana huyu aliyekuwa bado mdogo kiumri. Jabir alikuwa na mawazo mengi kuhusu madeni yake na kulea dada zake.
Madeni yalikuwa yakimwandama asubuhi na jioni. Alishiriki pamoja na Mtume katika vita ya Dhat ar-Riqa, akiwa juu ya ngamia dhaifu na mlegevu aliyekuwa akichelewa sana kujiunga na kundi. Kwa sababu hiyo, Jabir alibaki nyuma kabisa ya msafara. Mtume ambaye alikuwa akitembea mwisho wa jeshi, alimkuta Jabir na kumwambia: “Una nini, ewe Jabir?” Akajibu: “Ewe Mtume wa Allah, ngamia wangu amenichelewesha.” Mtume akasema: “Mwinue,” na alipoinamisha ngamia wake, Mtume akachukua fimbo mkononi mwa Jabir na kumpiga ngamia kidogo tu. Ghafla ngamia akasimama kwa nguvu na kuanza kukimbia kwa ari na nguvu kubwa.
Mtume alimgeukia Jabir kwa upole, akijua kuwa ni kijana aliyejitolea kwa ajili ya dada zake hadi akaamua kuoa mwanamke mkubwa wa umri kwa lengo la kuwalea vizuri dada zake. Mtume akamwambia kwa tabasamu: “Huenda tukifika Madina, mkeo akifurahi kwa kurejea kwako, akakuandalia mikeka laini na kukutandikia mazulia.” Lakini Jabir akakumbuka hali yao ya umasikini na kusema: “Mikeka! Wallahi, ewe Mtume wa Allah, hatuna hata mikeka.” Mtume akamfariji akisema:
“Hakika mtakuwa na mikeka, In shaa Allah.”
Kisha wakaendelea kutembea, na Mtume akampa Jabir dirham arobaini kama msaada wa kuanzia maisha yake.
(Imam Aḥmad 3/372).
Mwandishi anapatikana kwa simu 0712 690811