RC RUKWA AIPONGEZA TRA KWA KUWA KARIBU NA WALIPAKODI

:::::::

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhe. Makongoro Nyerere ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwa karibu na Walipakodi na kutatua changamoto zao kwa wakati hali ambayo imeleta utulivu katika ukusanyaji wa Kodi nchini.

Akizungumza mkoani Rukwa baada ya kutembelewa ofisini kwake na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda na Uongozi wa TRA leo tarehe 03.07.2025 Mhe.Makongoro amesema amekuwa akifanya kazi kwa karibu na Uongozi wa TRA mkoa wa Rukwa na kushiriki kuwasikiliza Walipakodi na kutatua changamoto zao.

Mhe. Makongoro amesema katika kuongeza wigo wa Kodi amekuwa akifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kurahisisha biashara baina ya Tanzania na nchi jirani kwa kuzingatia kuwa mkoa anaouongoza upo mpakani pia kutafuta namna nzuri ya kusafirisha mizigo kwa njia ya Boti ili kupunguza msongamano wa maroli mpka wa Tunduma huku akikaribisha Wawekezaji katika mkoa huo.

Amesema wananchi wanapoona maendeleo yamefanyika kwenye maeneo yao ikiwemo kujenga shule, zahanati na vituo vya afya pamoja na miundombinu mbalimbali wanaongeza kasi ya ulipaji Kodi ili kuhakikisha serikali inawaletea maendeleo kwa kodi zao.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda amemshukuru Mhe. Makongoro kwa kuisaidia TRA Rukwa na kueleza kuwa kazi ya ukusanyaji wa Kodi inayofanywa na TRA ni kwaajili ya wananchi maana fedha yote wanayokusanya inaingia kwenye mfuko Mkuu wa Serikali ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Bw. Mwenda amesema katika utekelezaji wa majukumu ya TRA ya kila siku wamekuwa wakizingatia maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutaka wakusanye Kodi bila kutumia mabavu na kuleta utulivu wa walipakodi nchini.

Aidha Bw. Mwenda amewapongeza Watumishi wa TRA mkoa wa Rukwa kwa kufanikiwa kuvuka malengo ya makusanyo kwa mwaka mzima kwa asilimia 130 maana walitakiwa kukusanya Shilingi Bilioni 44 lakini wamekusanya Shililingi Bilioni 57 na lengo jipya ni kukusanya Shilingi Bilioni 61.7.

Vile vile ameongeza kuwa kazi ya TRA ni kutoa huduma ndiyo maana wamekuwa wakisogeza huduma za Kodi karibu na Wananchi kwa kuweka vituo mpaka kwenye maeneo ambayo hayana makusanyo makubwa ili kuwezesha wananchi kupata Huduma kwa karibu.

 

Related Posts