::::::::::::
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,
Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameipongeza Ofisi
ya Msajili wa Hazina kwa mageuzi makubwa iliyofanya katika mashirika ya umma.
Mhe. Kikwete alitoa pongezi hizo Ijumaa, Julai 4, 2025, alipotembelea banda
namba 39 (Ukumbi wa Kilimanjaro) katika maonesho ya 49 ya biashara maarufu kama
Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
“Tunaishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya uongozi imara wa Msajili wa
Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, kwa kuwezesha taasisi za umma kuongeza ufanisi
wao,” alisema Mhe. Kikwete.
Aliongeza: “Wote ni mashahidi, katika uongozi wa awamu ya sita chini ya Mhe.
Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya kiutendaji
katika taasisi za umma.”
Ofisi ya Msajili wa Hazina imewezesha kuimarika kifedha kwa mashirika ya umma
yaliyokuwa na mitaji hasi na yaliyokuwa yanapata hasara mfululizo, ambapo sasa
yameweza kuondokana na utegemezi wa ruzuku ya Serikali na kufanikiwa kutoa
gawio.
Baadhi ya mashirika hayo ni pamoja na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi
(OSHA), ambapo mchango wake katika Mfuko Mkuu wa Serikali ulikuwa Sh10.5
bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25.
Pia, katika orodha ya mashirika ambayo kwa sasa yanajiendesha kwa ufanisi ni
Shirika la Taifa la Madini (STAMICO), Shirika la Umeme (TANESCO), na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
Mhe. Kikwete alisema serikali itaendelea kuiunga mkono ofisi ya Msajili wa
Hazina katika kuhakikisha safari ya mageuzi inafanikiwa.
“Endeleeni kufanya kazi kwa bidii na pale ambapo kuna mambo mnataka yabadilike
katika taasisi ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hesabuni mmepata
ushirikiano kutoka kwetu,” alisema Mhe. Kikwete.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Ofisi ya
Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri, alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la
ufanisi kwenye baadhi ya Mashirika kutokana na mageuzi yaliyofanyika na
yanayoendelea kufanyika katika Mashirika ya umma.