Mzee Samatta umeenda, hadithi zako tutazisimulia

ALIYEKUWA Rais wa Awamu ya Pili Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliwahi kusema maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa duniani, kwa sasa msemo huo unatumika kumsimulia maisha ya staa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Ally Pazi Samatta.

Mzee Samatta alikutwa na umauti leo Jumapili asubuhi na nilipokea ujumbe mfupi katika simu yangu uliyoandikwa; ‘Mzee wako Samatta hatunaye tena duniani’. Ilinichukua dakika kama tatu kuujibu kisha kuchukua hatua ya kupiga simu nikidhani nimesoma vibaya.

Nilimpigia simu kiungo wa zamani wa KMC, Prisons, Mbeya City, JKT Mgambo, African Lyon, Mohamed Samatta mmoja wa watoto wa Mzee Samatta, aliyekiri ni kweli mzee hatunaye tena.

Imeniwia vigumu kusimulia angalau kwa uchache namna nilivyomfahamu Mzee Samatta aliyenichukulia kama bintie na si mwandishi wa michezo, alikuwa mtu mwenye busara, hekima, upendo na hofu ya Mungu aliamini utu kuliko vitu alivyokuwa anasisitiza vinapita.

MZ 01


Siku tatu kabla ya kifo, nilipokea simu kutoka kwake, akiniambia ‘binti yangu naumwa utakapopata muda uje kuniona’, ingawa sauti yake haikuonyesha kama mtu aliyezidiwa, nikamjibu ‘Pole baba ‘Mzee Pele’, nitajitahidi kuja kukujulia hali’, kisha akampatia simu mkewe niliyempa pole ya kuuguza naye akasisitiza; ‘Uje umuone mzee wako’.

Kati ya vitu muhimu alivyoniambia siku hiyo vitakavyosalia kumbukumbu katika maisha yangu alisema: “unapopata changamoto katika maisha yako silaha ya kwanza iwe ukimya, bidii, kumtegemea Mungu na vitendo vyako viwe na nguvu kuliko maneno na kifo pekee ndicho kije kikatize ndoto zako.”

Ni kitu alichokisisitiza sana bila kujua siku za usoni nitapokea msiba wake.

Kisha akanigusia kuhusiana na binti yake anayeitwa Sophia aliyekuwa anatamani kusomea taaluma ya habari na sasa amechukua masomo ya utalii, akanisisitiza ikitokeaa akaja akasomea mambo ya habari uje kuwa msaada wa kumuelekeza maadili na kujituma.

MZ 02


Ni miaka mingi iliyopita kwa mara ya kwanza nilifunga safari ya kwenda kuhojiana na Mzee Samatta nyumbani kwake, Mbagala Rangi Tatu, nilimkuta akiwa na watoto wake, Said mchezaji wa zamani wa Polisi Tanzania, Mohamed na wajukuu zake.

Baada ya kujitambulisha akamwambia Said akanichukulie soda, nilipogundua ni mzee mcheshi baada ya Said kuleta soda zilikuwa katika mfuko kama nne hivi, akaniuliza unakunywa soda gani, nikajibu pepsi kwa bahati mbaya haikuwepo, akamwambia kijana wake ‘haya rudi tena dukani ukachukue’, nikajikuta naingiwa na hofu kuona nasumbua watu.

Baada ya Said kurejea na pepsi akamwambia baba yake ‘nimerudi afande’, kisha wakaanza kucheka, baadaye katika stori za hapa na pale nikagundua ni mzee msomi aliyekuwa kamanda wa polisi na mchezaji mahiri enzi zake.

MZ 03


Tangu siku hiyo alinieleza alipenda nidhamu yangu akawa na ushirikiano mkubwa na magazeti ya Mwananchi pindi alipoulizwa kuhusiana na vipaji vya watoto wake na maoni mbalimbali.

Kati ya Exclusive aliyowahi kuitoa kwa Mwanaspoti ilikuwa ni kuhusiana na ndoa ya kijana wake Mbwana Samatta aliyofunga mwaka 2021 na mkewe Naima Mgange.

Siku mbili kabla ya harusi ya Mbwana, mzee huyo alinitumia ujumbe katika simu yangu ukisema ndani ya wiki hii nitakupa taarifa kubwa na kweli ilipofika siku ya tukio ilikuwa jioni akanitumia ujumbe mwingine akisema ndugu yako anaoa (Mbwana), lakini hataki vyombo vya habari ila njoo moja kwa moja hadi nyumbani Mbagala utapanda gari la familia.

Baada ya kufika katika tukio la harusi yenyewe nikiwa na wanahabari wenzangu wawili tukazuiwa na watu ni kama walikuwa mabaunsa ambao hawakutaka kiandikwe chochote, ndipo yule mzee akasimama kifua mbele na kunitetea kwamba yeye ni mzazi ana haki ya kufanya kile anachokitaka kwa kijana wake, ndipo tukaendelea na kazi zetu.

MZ 04


Exclusive nyingine ilikuwa ni kuhusiana na msikiti ambao Mbwana ameujenga Vikindu Wilaya Mkuranga uliyo na uwezo wa kuingiza waumini 500, jumba lake la kifahari lilipo maeneo ya Kibada Wilayani Kigamboni, ofisi zake za utalii, kuwakataza vijana wake kupiga penalti pamoja na usajili wa Mbwana ukiwemo ule wa kwenda Aston Villa mwaka 2020.

Pia alikuwa anasisitiza kwa nini anapenda kumzungumzia Mbwana ni kutokana na ukimya wa kijana wake huyo, ambao baadhi ya watu walikuwa wanatumia kama fimbo ya kumkandamiza na mazuri yake aliyokuwa anayafanya yashindwe kuonekana, hivyo hakutaka kukubali unyonge aliamua kukaa mbele ili kuhakikisha kijana wake anapata heshima inayotakiwa.

Ukiachana na hilo, aliwahi kunishangaza katika mambo kadha, moja ni kukataa kwenda kuishi katika mjengo ambao kijana wake aliujenga alitamani zaidi kuona anapopita mtaani kwake Mbagala anataniwa na watoto njiani ambao alikuwa ana kawaida ya kuwapa pesa za kununua pipi, kachori na kuamini hiyo ni baraka kwake.

Pia aliwahi kusema alitamani angekuwa hai mama yake Mbwana ili ayaone mafanikio ya kijana wake, lakini kitu alichokifanya kama kumbukumbu ni kumbukusha kwenda kuwasaidia ndugu wa mama yake.

Kiufupi nitamuombea kwa Mwenyezi Mungu apumzike kwa amani na kuyafanyia kazi mambo aliyowahi kunishauri katika kazi yangu.

Maana sitapata tena fursa ya kuzungumza naye, kwani mwili wake unaenda kuhifadhiwa leo katika maskani yake ya milele huko Kibiti, Pwani. Inaumiza!

MZ 05


Mzee Ally Samatta alizaliwa mwaka 1943, Pwani na enzi zake aliwahi kuwa muajiriwa wa Jeshi la Polisi na akitamba katika soka kama mshambuliaji namba 10.

Baadhi ya timu alizozitumikia ni Polisi Moro aliyocheza mwaka 1962- 1963 kisha kukipiga Canada Dry (1963-1964) kabla ya kusajiliwa na Simba enzi ikifahamika kama Sundeland aliyoitumikia kuanzia mwaka 1964-1965. Amekipiga pia timu za West Lake (iliyokuja kubadilishwa majina kadhaa hadi kuwa Kagera Sugar), Polisi Dar es Salaam na timu ya Mkoa wa Dar es Salaam (Mzizima United). Pia amewahi kukipiga Cosmopolitan na timu za taifa kuanzia ile ya Tanzania Bara hadi Taifa Stars. Buriani!

Related Posts