Dk Mwinyi aipigia chapuo ‘Made in Tanzania’ Maonyesho ya Sabasaba

Dar es Salaam. Tanzania imezindua nembo maalumu ya ‘Made in Tanzania’ huku ikitajwa kuwa hatua muhimu ya maendeleo nchini na itaitambulisha Tanzania kimataifa kama Taifa lenye bidhaa zenye ubora, ubunifu na fahari ya Kiafrika.

Ndembo hiyo imezinduliwa leo Julai 7, 2025  na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba.

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Dk Mwinyi amesema ‘Made in Tanzania’ iwe chachu ya kukuza uzalendo wa kibiashara na kila Mtanzania atumie bidhaa za ndani.

“Nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kupenda na kuthamini bidhaa zetu ili kuzidi kuimarisha biashara na viwanda vyetu vya ndani na kuchangia ukuaji wa uchumi wetu,” amesema Dk Mwinyi.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akimkabidhi Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuunganisha na kutengeneza magari nchini  ya GFA, Ali Karmal tuzo ya mshindi wa jumla wa maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa, jijini Dar es Salaam.Kulia ni Waziri wa viawanda na Biashara Seleman Jafo. Picha na Said Khamis



Ameziagiza Wizara za Viwanda na Biashara katika pande zote mbili za nchi na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kuhakikisha elimu ya alama hiyo inawafikia wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

“Alama hii iwe chachu ya kukuza uzalendo wa kibiashara, kuhamasisha kila Mtanzania kujivunia, kutumia na kutangaza bidhaa zetu,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema kwa upande wa Serikali imekuwa ikichukua hatua za kimkakati ili kuhakikisha ukuaji wa sekta za viwanda na biashara unakwenda sambamba na dhamira ya Taifa ya maendeleo jumuishi.

Hatua hizi ni pamoja kurahisisha mazingira ya kufanya biashara, kukuza ubunifu, kushirikiana na sekta binafsi, kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali pamoja na kuandaa mifumo ya kutoa maoni na taarifa moja kwa moja ili kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.

 “Napenda niwahakikishie kuwa, Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi, sekta binafsi, wajasiriamali na wawekezaji katika kujenga mazingira wezeshi ya biashara,” amesema.

Amewataka watendaji wote wa umma katika taasisi wezeshi za biashara  kuhakikisha wanawezesha ukuaji wa biashara na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika shughuli zote za maendeleo.

Ameipongeza Tantrade kwa kupeperusha bendera ya Tanzania ikiwamo katika Maonyesho ya Osaka Japan akisema hadi wageni waliotembekea banda la Tanzania wamefikia milioni 4.7

Amesema ili kuunga mkono hilo, Tanzania inaendelea kutekeleza sera na mikakati ya kukuza bidhaa,  sera na huduma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mbali na kuzindua nembo ya ‘Made in Tanzania’ Dk Mwinyi pia amezindua rasmi Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba yaliyoanza Juni 28 mwaka huu na yanatarajiwa kukamilika Julai 13 mwaka huu.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema Tanzania imekuwa kinara katika uzalishaji wa bidhaa kiasi cha kuzidi mahitaji ya nchi, hali inayoashiria kuwa sasa ni wakati wa kuwa na nembo maalumu.

Baadhi ya bidhaa ambazo uzalishaji wake ni zaidi ya mahitaji ni saruji, vioo sambamba na bidhaa nyingine za wajasiriamali zinazouzwa masoko ya nje.

“Maonyesho haya yanabeba alama maalumu ya uzinduzi wa nembo ya ‘Made in Tanzania’ hiyo ni kwa ajili ya bidhaa za wawekezaji na wajasiriamali zinazokwenda masoko ya nje ili ziweze kutambuliwa kwa urahisi,” amesema Dk Jafo.

Amesema hiyo ni kwa sababu Tanzania imejipambanua kwa kuweka mazingira rafiki ya biashara ikiwamo kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali na kuandaa mpango wa blue print.

“Hilo limeenda sambamba na maboresho yaliyofanyika katika sekta mbalimbali ikiwamo upatikanaji wa umeme,” amesema Jafo.

Akizungumzia maonyesho ya mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Mohamed amesema maonyesho hayo 49 yanafanyika wakati wakijiandaa na kusherekea  Jubilee ya miaka 50 ya maonyesho hayo (Golden Jubilee).

“Ili kutimiza azma hiyo tumekuwa na kauli mbiu Jukwaa la Kimataifa la Sabasaba ‘Fahari ya Watanzania’ tunajivunia maonyesho haya kutimiza miaka 50, kwani nchi nyingi zimeshindwa kufanya hivyo kwa sababu ya kusuasua,” amesema Latifa.

Amesema maonyesho hayo ya 49  yamehudhuriwa na watu takribani 5,734 kutoka ndani na nje ya nchi na  kauli mbiu yake inahusu dijitali iliyokuja kutokana na mageuzi ya kitengo chao cha dijitali yanayofanywa na wataalamu wao.

“Wamebuni mfumo wa SabasabaApp, tuliounganisha na mifumo ya Serikali unaotuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi hadi kufikia Julai 6,20205, ulileta ufanisi mkubwa katika kupokea maombi na kutoa tiketi kwa washiriki,” amesema.

Amesema maonyesho ya safari hii kupata kitambulisho si tatizo tena, kwa wahitaji wanapata kupitia mifumo yao ya ndani iliyosaidia katika uwajibikaji na uwazi kwenye utendaji kazi.

“Kumekuwa na ongezeko la washiriki asilimia 10.6 ikilinganishwa na mwaka jana, tumerahisisha ununuzi wa tiketi kupitia mitandao yote na kutanua wigo wa watembeleaji kutoka 128959 hadi 29583 jana,” amesema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema maonyesho hayo kwa mkoa huo ni alama ya mkoa huo, kwa kuwa wamekuwa wakipokea wageni wengi.

“Bidhaa nyingi zinazooneshwa hapa zinazalishwa ndani ya mkoa wetu na nchi yoyote ili iweze kukua katika pato lake, huwezi kukwepa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ambazo wakati mwingine zinaweza kusafirishwa kwenda mataifa mengine,” amesema Chalamila.

Kwa mujibu wa Chalamila amesema Tanzania kupitia mkoa huo inahudumia nchi ambazo hazina bandari na ni kiashiria cha Dar es Salaam kukua kielelezo kwa Taifa  na hali ikiendelea hivyo pato la Taifa litazidi kukua.

Katika uzinduzi huo,  Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Biashara Afrika ya Mashariki (EACLC), Catty Wang amesema tangu mwaka 2021 wamekuwa wakiimarisha uhusiano wa biashara kati ya Tabxanis na China kwa kuwaleta wazalishaji wa bidhaa na wenye mitaji kuja Sabasaba

Kampuni hizo huja kutafuta mawakala na kuwekeza katika maeneo mbalimbali na hadi sasa mamia ya kampuni yamewekeza Tanzania kwa kufungua viwanda, kukuza ajira na kulipa kodi kwa serikali,” amesema Wang.

Related Posts