Dar es Salaam. Wakati makada wa Chama cha Wananchi (CUF) wakiendelea kujitokeza kuchukua fomu kuomba ridhaa za chama chao kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais chama hicho kimesema kinatarajia kufanya mkutano mkuu mwanzoni mwa Agosti 2025.
Katika mkutano mkuu huo maalumu yatapitishwa majina ya wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na unatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Agosti 2025 kwenye tarehe itakayotangazwa baadaye.
Chama hicho kinaoongozwa na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alipitishwa kwa kura 756 kati ya 789 kuwa mgombea wa urais kwa upande wa Tanzania bara katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020 huku aligombea urais kwa mara tano, kwa sasa kinashuhudia uchukuaji na urejeshaji fomu katika nafasi hizo tatu.
Hadi sasa wanachama wa chama hicho kutoka maeneo mbalimbali nchini wanaendelea na mchakato huo baada ya pazia hilo kufunguliwa rasmi Julai Mosi, 2025 huku likitarajiwa kufungwa Julai 15, 2025.
Baadhi ya makada hao kama Chifu Yemba aliyechukua fomu Jumanne Julai Mosi, 2025 kuomba ridhaa kwa chama chake kuwania nafasi ya urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu. Mwingine aliyechukua fomu kuwania nafasi hiyo ni Kiwale Mkungutila.
Akizungumza na Mwananchi, leo Julai 8, 2025, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano CUF, Mohamed Ngulangwa amesema vikao vya kuchuja wagombea na kura za maoni vitafanyika kwenye kata (kwa udiwani) na kwenye wilaya (kwa ubunge).
“Mkutano mkuu maalumu wa kumpitisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar unatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Agosti, kwenye tarehe itakayotangazwa baadaye,” amesema Ngulangwa.
Amesema, “ifikapo saa 10 jioni Julai 15 tutaweka hadharani orodha ya wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” ameongeza.
Amesema fomu zinachukuliwa kwa kasi kubwa na ni haki ya kila mwanachama kugombea nafasi yoyote kwa kuzingatia sheria za nchi.
“Tunatoa wito kwa wanachama wetu nchi nzima waendelee kujitokeza kwa wingi zaidi kugombea kila nafasi.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CUF, Husna Mohamed Abdallah amesema hadi sasa nafasi za chini fomu zimechukuliwa kwa wingi huku kwa upande wa Zanzibar, fomu zimechukuliwa kwa asilimia 98.
Amesema milango haijafungwa na yeyote anayehisi ana sifa za kugombea kupitia chama cha siasa anakaribishwa huku akisema hadi sasa hakuna nafasi yenye pengo.
Kuhusu Lipumba kurejea kwenye kinyang’anyiro cha urais Husna amesema hadi sasa Profesa Lipumba bado hajatangaza nia ya kugombea ingawa muda bado upo hadi Julai 15.
Alipoulizwa na mwandishi kama CUF inaweza kupata mgombea mpya wa urais amesema, “tunatarajia hivyo, lakini hii ni demokrasia. Hadi sasa hajatangaza nia,” amesema.