Fountain Gate yabaki Ligi Kuu, Stand United ijipange tena

Timu ya Fountain Gate imefanikiwa kubaki Ligi Kuu Bara baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Stand United kwenye mchezo wa ‘play off’ ya pili uliopigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, huku Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye akiwapongeza.

Hii ina maana kuwa, Fountain imefanikiwa kubaki Ligi Kuu kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1 baada ya kushinda 3-1 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

Katika mchezo huu, iliwalazimu mashabiki kusubiri hadi dakika ya 52 kushuhudia bao baada ya kipindi cha kwanza kumaliza kwa suluhu.

Mchezaji tegemeo wa Fountain Gate Eli Mukono, ndiye aliyepeleka kilio Stand baada ya kufunga bao safi kwa shuti kali kutoka nje ya 18 na kuwaamsha mashabiki wengi wa Manyara na mikoa ya jirani waliokuwa wamejazana kwenye uwanja huo.

Bao la pili la Fountain liliwekwa kiminia na Edgar Wiliam kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 90 ya mchezo huo.

Hata hivyo, kipindi cha pili Stand ilionyesha kiwango cha juu na kukosa nafasi kadhaa za wazi za kufunga mabao.

Fountain ilifika hapa baada ya kukusanya pointi 29 kwenye michezo 30 ya Ligi Kuu ambapo ilishika nafasi ya 14 kwenye msimamo.

Ilicheza mchezo wa kwanza wa mtoano na kupoteza kwa jumla ya  mabao 4-1 dhidi ya Prisons, baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza na ilipokwenda Mbeya ikalala 3-1. 

Hii ina maana kuwa timu mbili pekee ndiyo zimepanda kutoka Ligi ya Championship ambazo ni wakongwe Mbeya City pamoja na Mtibwa, sawa na msimu uliopita ambapo zilipanda timu za Pamba na KenGold ambayo imeshashuka tena.

Sasa itawalazimu Stand ambao awali walicheza mchezo wa mtoano na Geita Gold na kushinda kwa matokeo ya jumla ya mabao 4-2 kupambana tena kwenye Ligi ya Championship msimu ujao ili kutafuta nafasi ya kupanda daraja.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye alisema anawapongeza Fountain kwa kupata ushindi kwenye mchezo huo na kubaki kwenye Ligi Kuu kwa ajili ya msimu ujao.

“Niwapongeze wachezaji wa Fountain Gate kwa kiwango cha juu ambacho wameonyesha, kwetu hili ni jambo zuri, lakini pia napenda kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuhakikisha Ligi Kuu inachezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Manyara, tumekuwa tukiziona Simba na Yanga zikija kwenye uwanja huu, hili ni jambo zuri sana na linawafanya vijana wetu nao kutamani kucheza mchezo huu.

“Tunataka kumhakikishia kila mmoja kuwa tutahakikisha hapa mkoani kunakuwa na usalama wa kutosha kwa kila anayeingia na kutoka,” alisema Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka 10, awamu ya tatu.

Related Posts