Dodoma. Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imeeleza namna huduma za mawasiliano na fedha kidijitali zitakavyoboresha kilimo ambacho kinachangia asilimia 30 ya pato la Taifa.
Imeelezwa kuwa wakulima walio wengi bado hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha katika shughuli zao ikiwemo ununuzi wa pembejeo.
Hivyo, tume hiyo imesaini makubaliano ya kuingia katika ushirikiano wa kimkakati na Airtel Money Tanzania kwa lengo la kuboresha sekta ya kilimo kupitia huduma za mawasiliano na fedha kidijitali.
Ushirikiano huo unalenga kuwawezesha wakulima kupata huduma salama na za haraka za malipo, kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na kupanua upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu, hususan katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza wakati wa kutangaza ushirikiano huo jana Jumatatu Julai 7,2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Andrew Rugamba amesema, “kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), kilimo kinachangia takriban asilimia 30 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania.”
Amesema hata hivyo, bado wakulima wengi wadogo hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha. Kupitia ushirikiano huu, Airtel Money itatoa suluhisho la malipo ya kidijitali kwa wakulima na vyama vya ushirika, kuwezesha ununuzi wa pembejeo, upatikanaji wa simu janja za bei nafuu, pamoja na kujenga historia ya matumizi ya kifedha. Pia tutatoa elimu ya fedha na huduma kwa wateja kupitia mtandao wetu mpana wa mawakala.”
Amesema ushirikiano unafikiwa kutokana na mafanikio ya majaribio yaliyofanyika na Airtel kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika vya Masoko ya Mazao (AMCOS), mkoani Morogoro.
“Matokeo ya awali yalionesha mafanikio makubwa kwa kuongeza uwazi, ufanisi, na upatikanaji wa huduma kwa wakulima wadogo, huku yakipunguza changamoto za kifedha zilizokuwa kikwazo kwa maendeleo yao,” amesema.
“Kupitia ushirikiano huu, tunaweza kupanua huduma hizi na kuwafikia maelfu ya wakulima nchini kote. Tunajibu moja kwa moja wito wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alioutoa Desemba 2023, akiitaka sekta binafsi kushirikiana kwa karibu na wakulima wadogo ambao wengi wao hulima chini ya ekari 2.5, na wanahitaji msaada wa kubadilika kibiashara.” amesema.
Kwa upande wake, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dk Benson Ndiege amesema, “Makubaliano haya yanaashiria hatua muhimu katika kuimarisha maendeleo ya sekta ya ushirika na kilimo nchini.”
Kwa kushirikiana na Airtel Money, tunatoa fursa kwa wakulima wetu kustawi na kuendelea kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.”
“Kwa kuweka malipo ya wakulima kwenye mfumo wa kidijitali, na kutoa elimu na nyenzo za kifedha, ushirikiano huu kati ya Airtel Money na TCDC unatarajiwa kubadilisha maisha ya wakulima wa vijijini, kuongeza tija ya kilimo, na kuchochea mabadiliko ya kweli katika mustakabali wa sekta ya kilimo nchini Tanzania,” amesema Dk Ndiege.