Dar es Salaam. Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania (SDA) limeshinda rufaa dhidi ya waliokuwa wanakwaya wa Kanisa la SDA Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kuhusiana na hakimiliki ya nyimbo walizoshiriki kuziimba.
Kanisa hilo limeshinda rufaa hiyo baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kubatilisha hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, iliyowapa ushindi wanakwaya hao waliofutwa ushirika wa kanisa hilo, katika kesi ya msingi waliyoifungua.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 30, 2025 na Jaji Anold Kirekiano, baada ya kukubaliana na sababu za rufaa hiyo ya 2024, ilitokana na hukumu ya kesi ya msingi ya 2019 iliyofunguliwa na wanakwaya na pia washiriki wa kanisa hilo.
Kesi hiyo ya msingi ilifunguliwa na Barnabas Thomas, Mwita Katikiro na David Maiba, dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania, Mwenyekiti wa Kanisa la SDA, jimbo dogo la Kusini Mashariki mwa Tanzania na Mchungaji wa kanisa la SDA Kinondoni.
Walikuwa wakimlalamikia mchungaji wa kanisa hilo la SDA Kinondoni kukiuka haki zao katika nyimbo 20 za injili walizoshiriki kuzirekodi katika mfumo wa sauti (CD).
Walidai mlalamikiwa wa tatu (mchungaji wa Kanisa la Kinondoni SDA) alizirekodi katika mfumo wa picha jongefu (video) katika santuri aina ya DVD kwa kuwatumia watu wengine walioigiza kuimba sauti zao na kuziuza bila ridhaa yao.
Hivyo waliiomba mahakama itamke uamuzi wao kutafuta nafuu katika Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota) haukuwa utovu wa nidhamu kinyume cha maadili ya kanisa hilo, kwamba mdaiwa wa tatu (mchungaji) alikiuka haki zao kutumia sauti zao katika video bila ridhaa yao.
Pia, waliomba mahakama hiyo iamuru DVD zenye nyimbo hizo ni batili kwa kutokuwa na ridhaa yao na iamuru walipwe fidia ya hasara ya jumla ya Sh150 milioni, walalamikiwa wazuiliwe kuzalisha, kusambaza na kuziuza, na walalamikiwa walipe gharama za kesi hiyo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, wadai walidai mwaka 2017 walishiriki wakiwa ni sehemu ya wanakwaya wa kwaya hiyo, kuimba na kurekodi albamu ya nyimbo za kwaya yenye nyimbo 20 katika mfumo wa sauti, iliyoitwa ‘Wanadamu’.
Hata hivyo, usimamizi wa nyimbo hizo uliibua mzozo baina yao na mdaiwa wa tatu, mchungaji wa kanisa hilo la Kinondoni, jambo lililolazimu walalamikaji kuwasilisha malalamiko yao Cosota.
Walidai kuwa mwaka 2018, Mchungaji aliwafuta ushirika wa kanisa hilo (kwa madai ya utovu wa nidhamu), kisha alizirekodi nyimbo hizo katika video (DVD akiwatumia watu wengine ambao waliigiza kuimba sauti zao walizozirekodi katika nyimbo hizo.
Wadaiwa hao pamoja na mambo mengine walidai kuwa mmiliki wa nyimbo hizo ni kwaya ambayo iko chini ya kanisa hivyo nyimbo hizo 20 zinamilikiwa na kanisa na kwaya hiyo imesajiliwa Cosota na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).
Mahakama ya Wilaya katika hukumu yake iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Amosi Rweikiza, Desemba 3, 2024, ilikubaliana na walalamikaji kuwa haki zao zilikiukwa katika nyimbo hizo, lakini ikaamuru walipwe fidia ya Sh75 milioni badala ya Sh150 milioni walizokuwa wameziomba.
Walalamikiwa walikata rufaa, wakiwasilisha sababu 15 na mawakili kutoka kampuni ya Global Company and Advocates, Gadi Kabhele, John James Ismail na Mariam Kakungurume, huku wajibu rufaa waliwakilishwa na wakili Octavian Kamugisha.
Katika hukumu hiyo, Jaji Kirekiano amesema kuwa mahakama hiyo katika kesi ya biashara kati ya RSA Ltd dhidi ya Hanspaul Automech Ltd & mwenzake ya Mahakama Kuu ya 2014 iliyoamuliwa na Jaji Stephen Magoiga, ilijadili ulinzi wa hakimiliki ambapo ilisema kuwa,
“Ili kazi ilindwe na hakimiliki chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki (Sura 218 Toleo la 2002), mdai lazima athibitishe kwamba kazi hiyo ni ya asili na ni yake.”
Hoja kuu iliyolalamikiwa ilikuwa kama haki zao zilivunjwa katika nyimbo walizoshiriki kuziimba baada ya kuondolewa kwenye kwaya ya kanisa.
Wakili Kabhele, wa warufani (Kanisa) alidai mahakama ilifikia uamuzi usio wa haki kwani hakimu alishindwa kuonesha ushahidi wowote unaothibitisha umiliki sahihi wa nyimbo hizo kati ya kanisa na walalamikaji, ambao alidai hawakuwa wanachama waliosajiliwa wa Cosota kama ilivyothibitishwa na mlalamikaji wa tatu, Maiba.
Jaji Kirekiano amesema kuwa baada ya kupitia Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, anakubaliana wa warufani kabla ya kuhitimisha kuwa haki za walalamikaji zilivunjwa, umiliki wa nyimbo hizo ulipaswa kuthibitishwa kwanza.
“Ukweli kwamba walikuwa waimbaji wa kwaya ya kanisa hakuwapi moja kwa moja haki za umiliki juu ya nyimbo hizo”, amesema Jaji Kirekiano na kurejea kunukuu sehemu ya ushahidi wa mlalamikaji wa tatu, Maiba, alipohojiwa na wakili wa utetezi (kanisa), ambapo amesema kuwa, “Nilikuwa namuimbia Bwana Mungu. Sikuwa na haki ya umiliki. Nilikuwa na haki za kimaadili kwa kushiriki katika maandalizi ya nyimbo hizo, haki hizo zinapatikana kama raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haki hizo zinapatikana kwenye Biblia na katika mwongozo wa Kanisa.”
Jaji Kirekiano amesema kuwa kwa msingi huo, hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha kwamba walalamikaji walikuwa na umiliki wa moja kwa moja au walikuwa watunzi wa zile nyimbo 20, hali ambayo ingeweza kuwapa haki ya kudai ukiukwaji haki zao.
“Ni wazi kwamba waliimba kwa ajili ya kwaya na kwaya ilifanya kazi chini ya kanisa”, amesema Jaji Kirekiano.
Amsema kuwa katika muktadha huo, Mahakama Kuu katika kesi ya madai ya 2020, Tanzania – China Friendship Textile Company Limited dhidi ya Nida Textile Mills (T) LTD, iliamua kuwa, “inafaa kuzingatiwa kwamba hata pale ambapo mwandishi (mtunzi) au muumbaji wa kazi ya sanaa au fasihi ni mfanyakazi, mwajiri bado anachukuliwa kuwa ndiye mmiliki wa haki hizo.
Hii ndiyo inajulikana kwa kawaida, Marekani na Uingereza, kama kazi kwa mkataba.”
Amesema kuwa hivyo katika kesi ya Community for Creative Non-Violence v. Reed, 490 U.S. 730 (1989), Mahakama Kuu ya Marekani ilitoa kauli ya kuvutia kwamba:
“Kama kazi imetengenezwa chini ya mkataba wa ajira, mwajiri anachukuliwa kama mwandishi/mtunzi hata kama mfanyakazi ndiye aliyeiumba kazi hiyo wakati wa ajira yake.”
Jaji Kirekiano amesema kuwa kwa ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu, hakuna ubishi kwamba kwaya ni ya Kanisa la SDA Kinondoni, na walalamikaji wenyewe walithibitisha kwamba waliimba kwa ajili ya Bwana.
“Kwa kuzingatia upungufu huo wa ushahidi, naona kuna mashiko katika hoja za rufaa namba 2, 7, 8, 12 na 13 na hivyo zinakubaliwa. Mwisho, rufaa hii inakubaliwa kwa gharama. Hukumu na amri ya mahakama ya awali zinafutwa.”
Awali Kesi hiyo ilisikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Denice Mlashani ambaye katika hukumu yake Agosti 21, 2022, alitupilia mbali madai ya walalamikaji akisema kuwa hawakuwa na madai ya haki katika nyimbo hizo.
Walalamikaji walikata rufaa namba mwaka 2021, iliyotolewa na Jaji Juliana Masabo, Oktoba 7, 2022, ilitengua hukumu ya Wilaya ya Kinondoni, akaelekeza jalada lirudishwe Kinondoni hukumu hiyo iandikwe upya na pande zote zisikilizwe upya.
Mara hii kesi hiyo ilisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Rahim Mushi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni, ambaye alikubaliana na madai na nafuu zote walizoziomba walalamikaji, huku akiamuru walipwe fidia ya Sh90 milioni.
Walalamikiwa (Kanisa) nao walikata rufaa tena Mahakama Kuu ambayo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Elizabeth Mkwizu, ambaye katika hukumu yake aliyoitoa Desemba 15, 2023, alitengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Hivyo kesi hiyo ilirudishwa tena Mahakama ya Wilaya ikaamuriwa na Hakimu Rweikiza aliyewapa ushindi walalamikaji, hukumu iliyoibua rufaa hii ambayo Mahakama Kuu imelipa ushindi kanisa hilo.