KATIBU MKUU MASWI AIPONGEZA OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI USIMAMIZI WA MASHAURI

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imepongezwa kwa kuendelea kusimamia kwa weledi mashauri ya madai na usuluhishi hatua ambayo imesaidia Serikali kuongeza kasi katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakim Maswi alipotembelea banda la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Ndugu Maswi alisema kuwa uwepo wa weledi na ufanisi katika uendeshaji wa mashauri ya madai, usuluhishi, Katiba, Haki za Binadamu na Uchaguzi katika Ofisi hiyo umeongeza kasi katika kupunguza na kutatua migogoro ya kisheria kwa njia ya majadiliano badala ya kutumia muda mrefu kusikiliza shauri hilo mahakamani.

Ameongeza kuwa fedha zinazookolewa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zimekuwa zikitumika kujenga miradi mikubwa ya maendeleo ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuwarahisishia wananchi kote nchini katika kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo kwa urahisi.

Akiitaja miradi mikubwa inayotekelezwa nchini, ndugu Maswi amesema kuwa miradi hiyo ni pamoja na bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha takribani megawati 2,115 lililojengwa mto Rufiji, reli ya kisasa ya SGR, bwawa la kidunda, vituo vya afya, miradi ya barabara, elimu, ujenzi wa meli Ziwa Victoria pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa unaojengwa Msalato Jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa miradi hii kutachochea kasi ya wananchi katika kujiletea maendeleo kwenye nyanja ya uchumi na kijamii kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Aidha, Maswi ameipongeza Ofisi hiyo kwa kuendelea kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi wanaotembelea banda la Ofisi hiyo katika Maonesho ya Sabasaba kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuelewa haki zao na namna ya kuzitekeleza kupitia mfumo wa kisheria ikiwemo mashauri ya madai, usuluhishi, mashauri ya katiba, haki za binadamu na uchaguzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti Ubora wa Ofisi hiyo, Bi. Mercy Kyamba amesema kuwa ushiriki wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye Maonesho haya ya Sabasaba ni mwendelezo wa Ofisi hii kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuendelea kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi wanaotembelea banda la Ofisi hiyo.

Bi. Kyamba ameongeza kuwa Maonesho ya Sabasaba yatasaidia kujenga na kuongeza mahusiano na wadau hatua itakayosaidia kutangaza majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa taasisi za Serikali ambazo ndio wadau muhimu katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi.

Maonesho ya 49 ya kimataifa ya Kibiashara yalianza tarehe 28 Juni 2025 na kufunguliwa tarehe 7 Julai, 2025 na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakimu Maswi akimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Mashauri na Uthibiti Ubora wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Mercy Kyamba alipotembelea banda la Ofisi hiyo wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakimu Maswi akipitia Jarida la Wakili Mkuu alipotembelea banda la Ofisi hiyo wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakimu Maswi akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakiwa ndani ya banda la Maonesho la Ofisi hiyo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wanaotembelea banda hilo wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Mkaguzi wa Ndani wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Salma Mgaya akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Ofisi hiyo wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Msadizi Idara ya Usimamizi wa Mashauri na Udhibiti Ubora wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Mercy Kyamba akitoa maelezo kuhusu majukumu ya Ofisi hiyo kwa mwananchi aliyetembelea banda hilo wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Related Posts