Dar es Salaam. Katika mfululizo wa mapitio ya hukumu ya kesi hii ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Mahakama inajibu hoja ya utata wa mahali mauaji yalikofanyika na muda, hoj iliyobuliwa na baadhi ya washtakiwa, pamoja na mawakili wao.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) na Nicholous Kisinza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Marco Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi, John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi )na Salim Mbalu alikuwa Koplo.
Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara.
Kabla ya kuingia kwenye uchambuzi wa ushahidi uliowasilishwa na pande zote ili kujibu swali iwapo upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake dhidi ya washtakiwa kiasi cha kuwatia hatiani au la, Jaji Hamidu Mwanga anajielekeza kujibu hoja zilizoibuliwa na washtakiwa wanne na mawakili wao.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka na ushahidi wa upande wa mashtaka, mauaji ya Mussa yalifanyika, Januari 5, 2022 katika Kituo cha Polisi Mitengo, wilayani Mtwara.
Hata hivyo, katika utetezi wao, mshtakiwa wa kwanza Kalanje, wa pili Onyango, wa tatu Kisinza na wa sita Mkupa pamoja na mawakili wao katika hoja zao za mwisho, walikanusha kuwepo Kituo cha Polisi Mitengo.
Walidai kuwa, kwa mujibu wa Mwongozo wa Utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO), namba 13, hakuna Kituo cha Polisi Mkoa wa Mtwara au nchini Tanzania kinachoitwa Kituo cha Polisi Mitengo, hivyo walidai mauaji yanayodaiwa yalitokea katika kituo kisichokuwepo kisheria.
Kwa sababu hiyo, walidai kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na kasoro za kisheria kwa madai kuwa, kuna utofauti kati ya hati ya mashtaka na ushahidi uliotolewa.
Kwa kuwa upande wa mashtaka haukufanya marekebisho kwenye hati ya mashtaka, hati hiyo ina dosari kubwa, hivyo tiba yake ni kufuta mashtaka kwa kuwa kasoro hiyo iliathiri uwezo wa washtakiwa kujitetea ipasavyo kutokana na utata wa eneo husika na kosa lilikodaiwa kutendeka.
Jamhuri kupitia waendesha mashtaka wa kesi hiyo, walieleza kuwa, waliwasilisha ushahidi unaoonesha kuwa kuna Kituo cha Polisi cha Mikindani ambacho pia hujulikana kama Kituo cha Polisi cha Mitengo, ingawa jina la Mitengo halipo kwenye PGO.
Walirejea ushahidi wa shahidi wa tatu, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa Mtwara wakati wa tukio hilo, kwa sasa Kamanda wa Polisi Mkoa Ilala, Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Yustino Mgonja.
Ushahidi mwingine waliourejea ni wa shahidi wa pili ambaye ni mjomba wa marehemu Mussa, aliyemsindikiza kituoni hapo Januari 5, 2022, alipoitwa kwenda kuchukua mali zake walizozichukua na shahidi wa tano upande wa mashtaka, ambaye ni mshtakiwa tano, Inspekta Msuya.
Waendesha mashtaka hao walidai kuwa, kituo hicho kutokutajwa katika PGO hakuhusiani na ubora wa maelezo au hati ya mashtaka iliyowasilishwa.
Wadai kuwa, kuna maelezo dhidi ya washtakiwa yanakidhi masharti yote ya Kifungu cha 132 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Marejeo ya 2022, kinachoeleza kuwa, hati ya mashtaka itakuwa sahihi ikiwa itabeba maelezo ya kosa au makosa anayoshitakiwa nayo mshitakiwa.
Jaji alivyoamua ubishi wa kisheria
Katika kuamua hoja hiyo inayoibua masuala muhimu ya kisheria yanayogusa msingi wa kesi hiyo, Jaji Mwanga alisema: “Ni kweli, ninaunga mkono hoja za mawakili wa washtakiwa kwamba Kituo cha Polisi cha Mitengo hakijatajwa katika PGO.”
“Hata hivyo, ninatofautiana nao kuhusu dai kuwa, kuna utofauti kati ya hati ya mashtaka na ushahidi, kwa kuwa hati ya mashtaka na ushahidi vyote vinaonesha kuwa mauaji yalitokea Kituo cha Polisi cha Mitengo.”
“Kuhusu madai kuwa Kituo cha Polisi cha Mitengo hakipo, pia mtazamo wangu unatofautiana na ule wa mawakili,”alieleza Jaji Mwanga.
“Kwa maoni yangu, mawakili hawa mahiri na washtakiwa, ambao wanadhaniwa kuwa na uelewa mpana zaidi kuhusu masuala kama haya, wanaonekana kupotoka kuhusu nini kinachofanya hati ya mashtaka kuwa na dosari.”
Akifafanua zaidi, Jaji Mwanga alisema: “Kifungu cha 2 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, kinafafanua kituo cha polisi kama ifuatavyo:
“Kituo cha polisi maana yake ni sehemu yoyote iliyoteuliwa na Inspekta Jenerali (IGP) kuwa kituo cha polisi na inajumuisha eneo lolote la karibu linalohudumiwa na kituo hicho.”
“Hii inamaanisha kwamba, sehemu yoyote iliyoainishwa waziwazi kama kituo cha polisi, pamoja na eneo linalohudumiwa na askari wa kituo hicho, inahesabika kama sehemu ya kituo hicho cha polisi.
“Katika kesi hii, Kituo cha Polisi cha Mikindani ndicho chenye jukumu la kutoa huduma za kipolisi katika eneo la Mitengo, ambalo baadhi ya mashahidi wamelitaja kama Kituo Kidogo cha Polisi cha Mitengo,” alisema Jaji Mwanga.
“Kama inavyooneshwa na ushahidi kuwa eneo la Mitengo liko ndani ya mamlaka ya Kituo cha Polisi cha Mikindani.
“Eneo hilo lina kiongozi wa kituo, ambaye kwa wakati wa tukio alikuwa ni shahidi wa 25 upande wa mashtaka, Paulo Kiula na kama alivyoeleza shahidi huyu, lina vitabu vyote vya rejista vinavyohitajika kwa ajili ya kituo cha polisi,”alisema Jaji Mwanga.
“Hivyo basi, kwangu mimi, kutokuwepo kwa jina la Mitengo kama kituo cha polisi katika PGO hakufanyi kuwa ni dosari mbaya ya kisheria. Hata hivyo, kiini cha hati ya mashtaka kilikuwa ni tendo la mauaji, jina la marehemu, tarehe na eneo mahsusi (Mitengo).
“Ni eneo linalojulikana vyema kwa washtakiwa kwa kuwa, liko ndani ya mamlaka yao kama askari wa Kituo cha Polisi cha Mikindani na wamekuwa wakifanya kazi katika eneo hilo mara kwa mara.
“Kwa maneno mengine, kwa kuwa watuhumiwa walifahamishwa kuhusu eneo halisi la tukio la uhalifu, hoja ya kwamba hati ya mashtaka ina dosari kwa sababu tu ya jina la kiutawala la kituo haiwezi kukubalika,”alisisitiza Jaji Mwanga.
“Zaidi ya hayo, upande wa utetezi haukuonesha namna ya kutaja vibaya kituo hicho kulisababisha madhara makubwa au mkanganyiko kwao wakati wa kujitetea. Hivyo, madai yao hayana mashiko na hayana msingi wowote,”alisema Jaji Mwanga.
Hoja ya muda kosa lilipotendeka
Jaji Mwanga alisema wakati wa usikilizaji wa kesi, hasa wakati wa ushahidi wa moja kwa moja, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, alilalamika kwamba, hati ya mashtaka haijaainisha muda wa kutendeka kwa kosa hilo.
“Ni kweli kuwa hati ya mashtaka inataja maelezo mengine ila haielezi muda. Kwa maoni yangu, hati ya mashtaka haiwezi kusemwa kuwa ina dosari kwa sababu tu haijaonesha muda wa kutendeka kwa kosa.
“Ingekuwa ni hoja kama hati ya mashtaka ingetamka muda wa tukio, lakini ushahidi uliowasilishwa haukuthibitisha au kuuonesha muda huo,”alieleza Jaji Mwanga.
“Zaidi ya hayo, mazingira yaliyosababisha kifo hicho hayawezi kuruhusu kubaini muda halisi wa tukio.”
Katika sehemu inayofuata, tutawaletea uchambuzi wa ushahidi kuelekea hitimisho la hukumu hii, usikose.