Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu raia wa Congo DRC, Gabriel Mahdera (27) kulipa faini ya Sh250,000 au jela mwaka mmoja, baada ya kupatikana na hatia kuwepo nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne, Julai 8, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, baada ya washtakiwa hao kukiri shitaka lao.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameshindwa kulipa faini hiyo na hivyo amepelekwa gerezani ili aanze kutumikia kifungo hicho.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Lyamuya amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa, baada ya kukiri shitaka lake.
Hakimu Lyamuya amesema kwa kuwa mshtakiwa ni kosa lake la kwanza na kwa kuwa amekiri mwenyewe bila kulazimishwa, Mahakama hiyo inamuhukumu kulipa faini ya Sh250,000 na akishindwa kulipa faini hiyo atatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Raphael Mpuya akisaidiana na Mohamed Mlumba waliomba Mahakama hiyo itoe adhabu kwa mujibu wa sheria.
Mahdera alipopewa nafasi ya kujitetea na Mahakama aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na hatorudia tena.
Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza shufaa za mshtakiwa alikubaliana na ombi hilo na kumuhukumu kulipa faini.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai ya mwaka 2025 yenye shitaka moja la kuwepo nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Anadaiwa kutenda makosa hayo Juni 19, 2025 eneo la Kivukoni, wilaya ya Ilala.
Mahdera anadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, alikamatwa na maofisa wa uhamiaji kwa kosa la kuwepo nchini bila kuwa kibali, wakati akijua kuwa ni kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.