Arusha. Vijana 700 waliofaulu kwa kiwango cha juu katika masomo ya sayansi kwenye matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa jana watanufaika na ufadhili wa masomo ya vyuo vikuu ndani na nje ya nchi yatakayofadhiliwa na Serikali kupitia programu ya ‘Samia Extended Scholarship DS/AI+ kwa asilimia 100’.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizindua programu hiyo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) leo Jumanne Julai 8, 2025 amesema mpango huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuiwezesha nchi kuwa na wabobezi wa kimataifa.
Amesema waombaji ambao ni wahitimu wa kidato cha sita waliotambuliwa kulingana na sifa za ufaulu wao wa masomo ya sayansi, hisabati, Tehama, sayansi asilia wanaruhusiwa kufanya maombi ya ufadhili ili kunufaika na programu hiyo kuanzia kesho Julai 9, 2025
”Hii ni fursa adhimu kwa vijana wetu wa Kitanzania, ambayo inadhihirisha dhamira ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwa makusudi kwenye maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa manufaa ya Taifa letu,” amesema

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Profesa Adolf Mkenda (kulia) akimsikiliza Muadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST), Dk Devotha Nyambo (kushoto)katika ziara yake leo mkoa wa Arusha, katikati ni Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Maulilio Kipanyula. Picha na Filbert Rweyemamu
Amesema serikali imedhamiria kuwekeza kwenye sayansi data, akili unde na sayansi shirikishi kutokana na dunia ya sasa inaendeshwa na taarifa pamoja na maarifa ambazo ni nyenzo kuu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili afya, kilimo, elimu, mazingira, biashara na usalama.
Amesema kama Taifa haliwezi kuwa watazamaji hivyo ni lazima liwe sehemu ya wanaounda suluhisho za kisasa kupitia maarifa hayo mapya, ambapo kupitia uwekezaji huo iwe chachu ya kuandaa kizazi cha Watanzania watakaoshiriki kikamilifu katika mapinduzi ya nne ya viwanda.
Kuhusu muundo wa programu hiyo amesema katika awamu hiyo ya ufadhili, jumla ya wanafunzi 50 watachaguliwa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao wamefanya vizuri kwenye masomo ya sayansi kwenye tahususi za sayansi asili na zenye somo la hisabati ya Juu.
Aidha, amesema wanafunzi hao wanapaswa kuwa tayari kushiriki kambi ya mafunzo kwa muda wa miezi 10 katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kwa ufadhili wa Serikali ili kuwaandaa kimaarifa, kisaikolojia, kizalendo na kitaaluma ili wawe tayari kuomba na kujiunga na vyuo vikuu bora vinavyoongoza duniani katika masomo ya shahada ya kwanza katika fani hizo.
Amefafanua kuwa kwa ngazi ya uzamili fursa u za ufadhili pia zinapatikana kwa vijana wa Kitanzania kusoma katika vyuo mahiri vya ndani ambavyo ni Indian Institute of Technology (IIT) Madras Zanzibar na Chuo cha NM-AIST kwa wale wanaotaka kuendeleza taaluma zao katika maeneo ya kimkakati
Profesa Mkenda amesema dhumuni la programu hiyo sio tu kuwaandaa vijana kwa ajili ya kusoma nje, bali ni kuijenga Tanzania yenye rasilimali watu yenye uwezo wa kuchangia katika sekta ya viwanda na uchumi wa kidijitali ndani na nje ya nchi.
”Kama tulivyoahidi wakati wa kuhitimisha hoja katika hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2025/26 kuwa Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa matumizi ya Akili Unde katika ufundishaji na ujifunzaji kwa makundi mbalimbali nchini ikiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalumu,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema kwa kutambua hilo Serikali inafanya mageuzi makubwa kwenye elimu hasa kupitia utekelezaji wa sera na mitaala iliyoboreshwa, imeandaa na kuidhinisha Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Akili Unde katika Elimu wa mwaka 2025 ambao utawafanya wahitimu kushindana kimataifa.
Profesa Mkenda ameongeza kuwa mwongozo huo pamoja na maeneo mengine, umeainisha matumizi bora na salama ya teknolojia husika kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
”Serikali imeandaa na kuidhinisha Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika elimu ambapo pamoja na vipaumbele vingine, mkakati huo unasisitiza utafiti na ubunifu katika teknolojia zinazoibukia ikiwemo Akili Unde,” amesema Profesa Mkenda.
Awali Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo hicho, Dk Amos Nungu amesema mpango huo ni wa kipekee unaotekelezwa kuwawezesha vijana waliojikita katika masomo ya sayansi kupata ufadhili utakaochangia kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.
Amesema wanafunzi 650 watapatiwa ufadhili katika vyuo vya hapa nchini kulingana na maeneo watakayoyachagua ya tahasusi zilizoanishwa kwenye programu ya ufadhili huo.