Arusha. Ikiwa jirani yako ana jambo fulani ambalo wewe huna, na ikiwa kwamba jambo hilo ni zuri, si dhambi, tena ni busara, ukajifunza kutokana na hilo.
Ukijifunza, bila shaka utaweka mikakati ya kulifanya jambo hilo nyumbani kwako.
Nasema hivi kwa sababu katika makala haya napenda kujadili hoja kwamba kama taifa tuweke nguvu za makusudi ili tujenge maktaba za jamii katika kila wilaya na mwishowe hata katika kila kata (community library).
Hapa mkoani Arusha, kwa mfano, tunayo maktaba moja tu ya jamii iliyopo jijini Arusha. Ipo nyingine moja ninayoifahamu. Lakini hiyo imejengwa na mtu binafsi aliye sasa nje ya nchi. Ukitembelea maktaba hizi mbili utakutana na mafuriko ya wasomaji, hasa watoto wa shule.
Ukifika maktabani humo siku ya Jumamosi, hutapata nafasi ya kukaa, na hutapata kitabu cha kusoma au kompyuta ya kufanyia kazi kwa sababu wasomaji ni wengi, nafasi ya kukaa ni haba, na vifaa kama vitabu ni vichache. Hatuwezi kujenga Taifa linalopenda kusoma na kujiendeleza kielimu na kitaaluma kwa staili ya namna hii.
Sasa nirudi kwa wazo nililoanza nalo kwamba ukiona jambo zuri kwa jirani yako ni busara nawe ukajipanga kulipata la kwako.
Nimeona maktaba nyingi za jamii huko Marekani na katika nchi zote za Ulaya nilizotembelea. Kule Marekani nimeona maktaba ya jamii katika kila kata nilipoishi. Watoto wetu kila jioni walikwenda maktaba iliyokuwa jirani na kule walijisomea vitabu mbalimbali na kutumia vifaa vingine vya kujielimisha kama vile kompyuta mpakato, kompyuta za mezani na vitaa vingine vya kielimu.
Maktaba hizo zilifunguliwa asubuhi na kufungwa saa nne usiku ili kuwapa nafazi wasomaji na hasa wanafunzi kusoma na kufanya kazi zao za shule (homework).
Saa za asubuhi na mchana watu wazima walikuwa wengi, hasa wastaafu na wengine, na jioni wanafunzi walikuwa wengi zaidi.
Kwa kufanya hivyo nchi hiyo na nyingine kama hiyo, imejenga jamii inayopenda kusoma, kufanya utafiti na kujiendeleza kielimu na kitaaluma.
Hali ilivyo hapa kwetu
Hebu siku moja uchukue basi au treni utoke Arusha kwenda Dar es Salaam. Utaona wananchi wenzetu wamelala muda wote au wanachati katika simu zao.
Huoni mtu anayesoma hata gazeti. Kusoma kitabu ndiyo kabisa hutaona. Na ukiona mtu anasoma kitabu huyo ni mgeni kutoka Ulaya, Marekani au mahali pengine.
Kwa hali hii hatujajenga Taifa linalotamani kusoma na kujiendeleza kielimu na kitaaluma. Tumejenga taifa linalotamani kupata cheti au shahada na safari ya kujielimisha inaishia hapo.
Pale Marekani tulipoishi na familia, maktaba ya jamii ilikuwa si zaidi ya umbali wa dakika kumi kutembea kwa miguu.
Maktaba hiyo iliendeshwa na serikali ya kata kwa kodi za wananchi wa kata hiyo na msaada kidogo kutoka serikali ya mkoa na serikali kuu. Lakini mara nyingi zaidi maktaba hizo zilijengwa, kumilikiwa na kuendeshwa na serikali ya kata ikishirikiana na serikali za wilaya na mkoa. Watoto wetu walipokuwa shule za msingi na sekondari, walikwenda kila jioni kujisomea katika maktaba iliyokuwa jirani na nyumbani kwetu.
Humo walifanya kazi walizopewa shuleni (homework), na pia wakapata fursa ya kujifunza kutumia kompyuta mpakato na kompyuta za mezani.

Mhudumu wa maktaba hiyo alikuwa na wajibu wa kuwasaidia wasomaji wote kujipatia walichohitaji na pia alikuwa na uwezo wa kuwasaidia wanafunzi katika kazi zao za shule na shughuli nyingine za kujielimisha.
Maktaba hiyo iliwakaribisha wastaafu, kina mama na kina baba.Wapo wengi wastaafu wanaojiteloea saa mbili au tatu mara kwa mara ili wawasaidie wasomaji hasa wanafunzi wa msingi na sekondari.
Hiyo kweli ni jamii ya wasomaji na jamii ya watu walio tayari kutoa muda wao kuwasaidia wengine bila malipo.
Huu ni mfano mzuri ambao sisi hapa Tanzania tunapaswa kuuiga na kuutekeleza katika mazingira yetu. Hizi maktaba za mikoa ambazo zipo sasa hazitoshi kabisa.
Kwa miaka hii 63 ya uhuru wetu, tungepaswa kuwa tumejenga walau maktaba za jamii kila wilaya kama si kila kata.
Hapa jijini Arusha naamini tungeweza kuwa na maktaba nyingi zaidi kama tungejipanga vizuri. Lakini hatutaweza kufanya hivyo hadi pale tutakapoamka usingizini na kuona faida ya maktaba hizi za jamii.
Maktaba nilizoona kwa wenzetu si za gharama kubwa. Jengo hili si kubwa sana. Lina chumba cha kujisomea ambacho kina vitabu na kompyuta kadhaa; kuna ofisi ya wahudumu, kuna stoo moja na vyumba vichache vya choo.
Hapa Arusha tunatumia takriban Sh20 milioni kujenga darasa moja na kwa kweli tumejenga madarasa lukuki katika hii miaka michache iliyopita.
Tunashindwaje kujenga maktaba ya jamii katika kila kata? Tunaweza kuanza polepole na baada ya miaka 10 tutakuwa na maktaba katika kata zote 25 za jiji la Arusha.
Tunahitaji tu jambo moja; utashi wa kisiasa na utambuzi mpana kwamba elimu haina mwisho na elimu ni bahari.
Ushauri wangu
Pendekezo langu ni kwamba viongozi wa wizara zinazohusika, hasa za elimu na tawala za mikoa, waone umuhumu wa kuwa na hizi maktaba za jamii walau kila wilaya kwa kuanzia, na wajitahidi kuongeza bajeti ya elimu ili jambo hili liwezekane.
Mwalimu Julius Nyerere alisema tunapigana na maadui watatu: ujinga, magonjwa na umaskini. Inaonekana hatujafaulu sana katika vita hii.
Njia mojawapo ya kupata wapiganaji wazuri wa maadui wote watatu ni kuwapa wananchi elimu bora, ambayo ni pamoja na kujenga maktaba nyingi zaidi za jamii katika wilaya zetu na kata zetu.
Nimeandika gazetini humu kuhusu huduma za jamii zinazotolewa na wanachama wa Rotary duniani. Wapo wanachama 1, 400,000 duniani kwa sasa.
Hapa Tanzania tuna wanachama 800. Huko Uganda wana wanachama zaidi ya 4,000. Kenya hali kadhalika. Tawi letu la Rotary la Njiro Arusha tuna ndoto ya kujenga maktaba ya jamii hapa kwetu.
Kama umeguswa na makala haya na ungependa kutusaidia kukamilisha ndoto hii, tafadhali nipigie simu. Ni wakati Watanzania tuanze kuchangamkia ujenzi wa hizi maktaba za jamii. Hatujachelewa sana.