‘Uandishi wa sheria za uchaguzi ulizingatia demokrasia’

Dar es Salaam. Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCDP), Onorius Njole, amesema mfumo wa sheria za uchaguzi nchini ni mzuri na umezingatia misingi ya kidemokrasia.

Mfumo huo sasa unatoa fursa sawa kwa wanaotaka kugombea nafasi yoyote na kuchagua kiongozi wanaomtaka.

Amesema hayo alipozungumza na Mwananchi katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema hayo wakati ambapo Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani Oktoba mwaka huu, uchaguzi ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano.

Njole amesema mchakato mzima wa sheria zinazokwenda kusimamia uchaguzi ulikuwa wa ushirikishwaji na umezingatia mahitaji yote ya demokrasia ya sasa, na unatoa uhakika wa ushiriki kamilifu kwa anayechaguliwa na anayekwenda kuchagua.

“Ninawahamasisha wananchi watumie fursa yao ya kikatiba na ya kisheria ya kuchagua na kuchaguliwa, kwani inatokea kila baada ya miaka mitano, na ukiikosa sasa maana yake utaikosa kwa miaka mitano na hautakuwa umeitendea haki nafsi yako, jamii na familia. Watu wajitokeze, tuna mifumo mizuri na inayotoa haki ipasavyo,” amesema.

Pia amesema kuwa wakati wa uandishi wa sheria hizo, ilitolewa fursa sawa kwa kuzingatia jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali, si tu kwa kutoa nafasi ya kugombea bali pia kuwezesha ushiriki wa watu katika kuchagua wanaowataka.

“Wakati sheria hizi zinapitishwa, moja ya mambo ya msingi yanayozingatiwa ni kutoa fursa ya ushiriki kwa watu wa mahitaji maalumu, na kwa mara ya kwanza fomu za wagombea na za kujiandikisha kwa ajili ya kuwachagua wagombea zimezingatia mahitaji maalumu ya makundi hayo,” amesema.

Akielezea namna wanavyoshirikisha wananchi, Mwandishi huyo wa sheria amesema kuwa wananchi huelezwa juu ya mchakato mzima.

Hiyo ni kwa sababu sheria zinazotungwa hugusa maisha ya kila siku na shughuli za kijamii na kiuchumi.

“Hivyo, ni muhimu sisi kama wadau wa utekelezaji wa shughuli za kijamii, kiuchumi na uwekezaji, tukajua mchakato wa utungaji sheria na kuwa sehemu ya mchakato huo, ili kujua ni lini tunakuwa na fursa ya kutoa maoni katika uandaaji wa muswada na kutoa maoni katika mchakato wa uandaaji wa sheria ndogo,” amesema.

Amesema kuwa mara zote sheria inatakiwa kuakisi mahitaji ya jamii na kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hizo, na hilo litawezekana ikiwa wananchi watashiriki kikamilifu katika uandaaji wa sheria hizo.

Akizungumzia urekebishaji wa sheria unaoendelea, amesema tayari toleo la urekebishaji wa sheria zote za nchi limeanza kutumika tangu Julai mosi 2025, na amewataka wananchi kuwasilisha maoni yao endapo wanaona kuna changamoto yoyote.

Rehema Katuga, kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, amesema kuwa hadi Agosti 2025, sheria ambazo zimetafsiriwa zitakuwa zinapatikana kwa wananchi.

“Hii itasaidia wananchi waelewe haki zao na kushiriki katika shughuli mbalimbali za nchi, ikiwemo za uchaguzi,” amesema.

Related Posts