Vifaranga milioni 2.5 vya matango bahari, samaki vyazalishwa kuchochea uchumi wa buluu

Unguja. Katika kuhakikisha rasilimali za uchumi wa buluu zinakuwa na kunufaisha wananchi, vifaranga milioni 2.5 vya samaki na matango bahari vimezalishwa visiwani Zanzibar.

Kati ya vifaranga hivyo, milioni moja vimezalishwa Pemba na milioni 1.5 vimezalishwa Unguja na tayari 26,000 vimeshatolewa kwa wafugaji 310.

Vifaranga hivyo vimezalishwa na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Mwambao kupitia kituo walichoanzisha cha kutotolea vifaranga vya samaki bahari kilichopo kisiwani Pemba.

Hayo yameelezwa leo Julai 8, 2025 na Mratibu wa wizara hiyo, Omar Saleh Mohamed wakati akizungumza na mwananchi digital.

Omar amesema kupitia Kampuni ya Zanzibar Marine Hatchery ambayo wizara ni mbia wake  wanashirikiana katika kuendesha kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki, kaa na matango bahari kwa upande wa Unguja.

“Vifaranga 22,000 vya majongoo vimeshagawiwa kwa wananchi mbalimbali kisiwani Unguja na vifaranga vya samaki 4,000 vimeshagawiwa kwa upande wa Pemba kwa wafugaji 310,” amesema Omar.

Amesema lengo kuu la wizara hiyo ni kusimamia utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar (2022) kwa kuimarisha matumizi endelevu ya bahari na kuwawezesha wajasiriamali kupata elimu kuhusiana na fursa za uchumi huo ili kukuza ubunifu na uwezo wa kupata zana za ujasiriamali.

Amefafanua kuwa katika kuimarisha maeneo ya hifadhi za bahari na kuendeleza maeneo ya utalii wa bahari, wizara imekamilisha mpango wa usimamizi wa maeneo ya hifadhi ikiwemo Mimca, Menai, Pecca, Tumca na Chabamca, huku mipango mikakati ya doria za baharini ikiendelea.


Pia, amesema wizara imefanikiwa kuandaa mwongozo wa kusimamia uwekezaji ndani ya hifadhi za bahari, katika kipindi cha miezi sita na miradi minne imepewa vibali kwa ajili hiyo.

“Mafanikio hayo ni matokeo ya uwezeshaji wa wananchi uliofanywa na wizara kwa kushirikiana na kampuni ya uvuvi (Zafico), pamoja na Benki ya CRDB kupitia programu ya inuka na Uchumi wa Buluu Zanzibar kwa kuwakopesha wavuvi boti 1,031 kati ya boti hizo 227 ni za mita nane ambazo hutumika kuvulia kwenye maji makubwa,” amesema Omar

Naye, Mtaalamu wa kuzalisha vifaranga vya majongoo bahari, kaa na samaki, Khamis Hassan Ali amesema licha ya kuwepo kwa bahari nzuri katika maeneo ya Zanzibar lakini ufugaji wa samaki unahitaji bahari iliyokuwa na topetope.

Amefafanua kuwa katika kujitayarisha ufugaji huo ni lazima upate baadhi ya vifaa ikiwemo nyavu , miti au paipu kwa ajili ya kuongeza uzio ili wasitoke.

“Ufugaji wa majongoo bahari lazima uwe katika sehemu zenye maji ya chumvi na sio maji ya mito,” amesema

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, iwapo wananchi wa Zanzibar watafuga matango bahari na samaki aina ya kolekole, tasi na kaa tope watainuka zaidi kiuchumi kwa vile mazao hayo yamekuwa biashara kubwa katika soko la dunia hivi sasa.

Yussuf Haji ni mmoja wa wafugaji wa majongoo bahari, amesema licha ya kwamba bado hajaanza kuuza mazao hayo lakini ana matumaini makubwa yatamsaidia kuinua uchumi wake.

Akifafanua juu ya uzalishaji wa mwani kisiwani hapo, Omar amesema uzalishaji wake umeongezeka kwa asilimia 124.6 kutoka tani 8,785 zenye thamani ya Sh5.3 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia tani 19,716 zenye thamani ya Sh16.1 bilioni kwa mwaka 2024.

Amesema, mafanikio haya yametokana na juhudi za Serikali za kuwapatia boti 500 na vifaa vya ukulima wa mwani wakulima 5,000 Unguja na Pemba na wizara imekamilisha ufugaji wa makaushio ya mwani yanayotumia jua na chanja katika maeneo ya Muungoni, Bweleo kwa Unguja na Kiuyu kwa Pemba.

Vilevile, wajasiriamali 4,000 wamepatiwa mafunzo juu ya ufugaji, uvuvi na ukulima wa mwani kupitia programu ya ahueni ya Uviko-19 na wa watendaji 50 wa wizara walipata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji wa mazao ya baharini ikiwemo mwani na majongoo nchini Korea na China

Related Posts