Wataalamu serikalini kutathmini uendeshaji bora bandari ya uvuvi Kilwa

Lindi. Wakati Bandari ya Uvuvi Kilwa ikitarajiwa kukamilika mwaka huu, wataalamu kutoka Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wameunda kamati ndogo ya wataalamu kutafuta mbinu bora ya uendeshaji wa bandari hiyo.

Uendeshaji bora wa bandari hiyo utasaidia kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kutoka tani 40,721.53 hadi tani 52,937.99 kulingana na takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza katika ziara ya kutembelea bandari ya Kilwa leo Julai 8  iliyoandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), 2025, Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi kutoka Wizara ya Uchukuzi, Biseko Chiganga amesema timu hiyo ya wataalamu ikikamilisha kazi yake itatoa mwelekeo ya namna ya uendeshaji wa bandari.

Biseko amesema timu hiyo ya wataalamu imejumuisha wataalamu wa Tasac, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja Mkoa wa Lindi.

“Tumetembelea mradi na tumefanya kikao cha pamoja kuangalia kabla ya mradi kukamilika tuangalie changamoto zilizopo na namna ya kuendesha bandari hii kwa ngazi ya wataalamu.


“Yapo mambo ya kitaalamu kwa ngazi ya awali, hizi kamati za kitaalamu zikikamilisha kazi yake ndio utatoa mwelekeo wa uendeshaji wa bandari,” amesema.

Mkurugenzi Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Usafiri Majini, Nelson Mlali amesema wametembelea kujionea ujenzi wa bandari hiyo ili kujipanga namna ya uendeshaji wake mradi utakapokamilika.

“Sisi kama wadhibiti wa usafiri wa njia ya maji tumewaeleza wadau majukumu yetu mradi utakapokamilika, mradi huu ukikamilika unakuwa bandari na bandari na bandari ni moja ya wadau unaodhibiti huduma zake kwa hiyo tumeeleza namna ambavyo tutaisimamia bandari hii,” amesema.

Mlali amesema miongoni mwa majukumu yao bandari hiyo ikikamilika ni kuwapa elimu mabaharia watakaoendesha huduma za uvuvi, usimamizi wa mawakala wa meli, forodha pamoja na kampuni ndogo ndogo za kusimamia huduma za vyakula.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Jackson Ally, mkazi wa Kilwa Masoko amesema madereva bodaboda na vijana watakuza uchumi.

“Bandari hii kwetu tunaiona kama faraja yetu, mazao ya uvuvi yataongezeka kwasababu uvuvi utakuwa wa kisasa, tutapata ajira na vijana wengi wataondoka vijiweni,” amesema.

Mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa, kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, hadi kukamilika kwake utatumia takribani Sh250 bilioni na matarajio ni mradi huo kukamilika mwaka huu.

Kukamilika kwa bandari hiyo kutawezesha meli za uvuvi zinazovua ukanda wa uchumi wa bahari ya Tanzania na bahari kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Pia, uwepo wa bandari hiyo utachochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi.

Aidha, bandari hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira kwa Watanzania takriban 30,000 huku katika hatua za awali za ujenzi, jumla ya ajira za muda mfupi 278 zimetolewa ambapo kati ya hizo, ajira 106 sawa na asilimia 38 zimetolewa kwa wakazi wa Wilaya za Mkoa wa Lindi.


Bandari hiyo utahusisha, pia,  ujenzi wa jengo la utawala, eneo la maandalizi ya samaki kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi, kituo cha umeme wa kuhudumia uendeshaji wa bandari na kituo cha maji safi kwa ajili ya kuhudumia bandari.

Related Posts