Nairobi. Watu 10 wameuawa na wengine 29 wakijeruhiwa katika maeneo mbalimbali Kenya wakati taifa hilo likiadhimisha miaka 35 ya Siku ya Sabasaba.
Maandamano hayo yaliyofanyika kaunti 17 ni kumbukumbu ya yale yaliyofanyika Julai 7, 1990 katika Uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi, Kenya wananchi walikuwa wakidai uchaguzi huru wakati wa utawala wa Rais Daniel Arap Moi.
Sasa ni miaka 35 imepita huku Gen Z wakiadhimisha siku hiyo kwa kufanya maandamano.
Jana, saa 12:30 jioni, Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNHRC) ilikuwa imerekodi matukio mawili ya utekaji nyara watu 37 katika kaunti zilizoathirika na maandamano hayo.
Maandamano yaliripotiwa katika kaunti za Nairobi, Kiambu, Kisii, Nakuru, Embu, Kajiado, Nyeri, Narok, Laikipia, Murang’a, Meru, Machakos, Kirinyaga, Uasin Gishu, Makueni, Kakamega na Nyandarua.
Kwa mujibu wa tume hiyo ya serikali, polisi waliweka vizuizi barabarani kwenye maeneo muhimu ya kuingia na kutoka, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa wa usafiri hasa jijini Nairobi. Vizuizi vingine viliripotiwa katika kaunti za Kiambu, Meru, Kisii, Nyeri, Nakuru na Embu.
“Wakenya wengi walishindwa kufika kazini licha ya agizo la Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, alilolitoa jana akiwataka wafanyakazi wote wa serikali kufika kazini bila kukosa,” inaeleza KNHRC.
Tume hiyo pia ilikosoa polisi kwa kukaidi agizo la Mahakama Kuu lililowataka maofisa wote wanaosimamia maandamano kuvaa sare rasmi na kuwa na vitambulisho wakati wote.
“Maofisa wengi waliovaa kofia na mavazi ya kiraia waliokuwa wakitumia magari yasiyo na alama wakifanya doria katika kaunti za Nairobi, Kajiado na Nakuru. Aidha, magenge ya wahalifu waliokuwa wamejihami kwa silaha butu kama mijeledi, marungu, mapanga, mikuki na pinde yalionekana Nairobi, Kiambu, Kajiado na Eldoret.
“Nairobi na Eldoret, magenge haya yalionekana yakishirikiana na polisi,” amesema Naibu Mwenyekiti wa KNHRC, Raymond Nyeris.
Katika eneo la Kangemi, maandamano yaligeuka vurugu baada ya mwandamanaji mmoja kupigwa risasi na kuuawa kando ya Barabara ya Waiyaki. Mwili wake uliachwa barabarani.
Kitengela, hali ya wasiwasi ilitanda polisi walipokabiliana na waandamanaji na kuwasukuma hadi maeneo ya vichochoro katika Barabara ya Old Namanga.
Mmoja wa waathiriwa, Brian Kimutai mwendesha bodaboda mwenye umri wa miaka 21, alipigwa risasi na polisi na alithibitishwa kufariki alipowasili katika Hospitali Ndogo ya Kitengela.
“Yeye ni mdogo wangu. Alikuwa amenyanyua mikono juu kama ishara ya kujisalimisha. Alikuwa mfanyakazi mjini. Wamemuua. Tunataka haki itendeke,” amesema Antonella Ashava (26), dada wa Kimutai katika mahojiano na Daily Nation.
Wakati biashara nyingi zikifungwa, baadhi ya vijana walitumia fursa hiyo kupora maduka katika Mtaa wa Mwireri, Kitengela.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Nyandarua Kati, Sammy Kamau alithibitisha kwamba, ofisa mmoja wa polisi alijeruhiwa katika mapambano hayo.
Katika Hospitali ya JM Memorial, Msimamizi Mkuu wa Matibabu, Dk Beatrice Mugure amethibitisha mgonjwa mmoja alilazwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).
“Tumepokea mgonjwa mmoja anayehitaji uangalizi maalumu. Kwa sasa hana taarifa zaidi, anapokea matibabu ya dharura,” amesema Dk Mugure.
Huko Thika, mtu mmoja alijeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na polisi, ingawa Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Thika Magharibi, Lawrence Muchangi amepinga taarifa kwamba alifariki kwa risasi.
“Sijapokea taarifa rasmi, hivyo siwezi kuthibitisha kifo chochote kwa sasa,” amesema Muchangi kwa njia ya simu.
Hali ya taharuki iliendelea kutanda Thika huku biashara nyingi zikiwa zimefungwa kwa hofu ya uporaji. Wakazi wa eneo hilo waliilaumu Serikali kwa mauaji ya kiholela na ufisadi waliodai unachangia ukosefu wa ajira.
Kaunti ya Kiambu, hali ilikuwa kama hiyo, polisi walipokabiliana na waandamanaji. Mmoja alijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Kiambu Level 5. Biashara zilifungwa na usafiri wa umma ulisitishwa.
Huko, Murang’a mtu mmoja aliripotiwa kufariki kwa mujibu wa Ofisa Mkuu wa Afya katika Kaunti hiyo, Eliud Maina.
Maina ameiambia Daily Nation jioni ya Julai 7, 2025 kuwa, watu 140 walijeruhiwa katika makabiliano ya polisi na waandamanaji, saba wakiwa ni maofisa wa polisi.
Amesema eneo la Kangari, Jimbo la Kigumo, lilikuwa kiini cha mapambano majeruhi wengi walitokea huko.
Amesema Hospitali ya Taifa ya Kenyatta (KNH) imelemewa na idadi ya wagonjwa, hivyo walikataa kupokea rufaa za wagonjwa wawili waliokuwa mahututi.
“Uongozi wa KNH ulituambia wamelemewa na hawana nafasi wala rasilimali watu ya kuwapokea,” amesema Maina.
Asilimia 90 ya waliojeruhiwa walikuwa wanaume, huku mwenye umri mdogo akiwa na mwaka mmoja na mkubwa zaidi akiwa na miaka 75.
Huko Githurai 45, vijana walifunga barabara huku polisi wakikabiliana nao. Thika Road Mall ilifungwa kuzuia wizi.
Kisii, watu wasiopungua watano walijeruhiwa kwa mishale na kupelekwa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii. Ofisa wa matibabu aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake, alisema majeraha mengi yalikuwa mikononi.
“Tumepokea wagonjwa watano waliochomwa mishale mikononi. Tumeweza kutoa mishale hiyo salama,” alisema.
Waandamanaji Kisii walidai kuwa wanasiasa wa eneo hilo waliwaajiri wahuni kuvuruga maandamano ya amani.
Nyeri, maandamano yaligeuka mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya biashara fulani. Waandamanaji walijaribu kupora mali za duka la Khetia, lakini walizuiwa na polisi.
Baada ya kushindwa, walielekeza hasira kwa biashara ndogo ndogo kama mgahawa, duka la simu, klabu ya usiku, duka la nguo na ofisi ya Well Fargo mjini humo.
Mashuhuda walisema machafuko hayo yalionekana kuwa ya kupangwa, si ya ghafla.
Wakati huohuo, Kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga amesema vizuizi vya polisi jijini Nairobi ndio sababu iliyomfanya ashindwe kufika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 35 ya maandamano ya Sabasaba.
Odinga alikuwa amewahimiza Wakenya kukusanyika katika Uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi kuadhimisha kumbukumbu ya maandamano ya kihistoria ya Sabasaba.