AZAM FC haina utani baada ya kutambulisha kocha mpya, Florent Ibenge na nyota watatu wazawa Aishi Manula, Lameck Lawi na Muhsin Malima, lakini kwa sasa mabosi wa klabu hiyo wanadaiwa wameanza mazungumzo ya kuipata saini ya winga wa Al Hilal ya Sudan, Yaser Muzmel Muhamed Altayeb ikiwa ni pendekezo la Ibenge aliyewahi kufanya naye pia kazi.
Nyota huyo anakumbukwa zaidi na mashabiki wa Yanga wa 2024-2025 wakati alipofunga bao la pili la dakika ya 90 katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, hivyo kuiwezesha Al Hilal kushinda mabao 2-0, Novemba 26, 2024.
Mechi hiyo ya kundi A iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Muzmel alifunga bao hilo dakika ya 90 na kuizima Yanga iliyokuwa inapambana kusawazisha baada ya Adama Coulibaly kuitanguliza Al Hilal dakika ya 63. Katika kundi hilo, Al Hilal ilimaliza vinara wa kundi A na pointi 10 nyuma ya MC Alger ya Algeria iliyomaliza ya pili na pointi tisa, wakati Yanga ilimaliza ya tatu na pointi nane huku TP Mazembe ya DR Congo ikiburuza mkia na pointi tano.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza nyota huyo amekubali kujiunga na Azam ili kuungana tena na Kocha, Ibenge aliyefanya naye kazi, ingawa kinachoendelea kwa sasa ni makubaliano baina ya klabu hizo kwa ajili ya dili la nyota huyo. “Tutaendelea na maboresho ya nyota wapya kama ambavyo tumekuwa tukitangaza kwa wale ambao tumenasa saini zao, Muzmel ni mchezaji mzuri ambaye ni pendekezo la benchi la ufundi na tayari tunayafanyia kazi kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, wakati Ibenge anatambulishwa kuifundisha timu hiyo Julai 5, 2025, akichukua nafasi ya Rachid Taoussi raia wa Morocco, alisema wachezaji waliopo kikosini ni wazuri, ingawa tayari ameanza kutoa mapendekezo ya nyota anaowataka.
Muzmel aliyezaliwa Aprili 15, 1993, huku akiichezea pia Mouais SC na Al-Ahly Shendi zote za kwao Sudan, ni miongoni mwa nyota wenye uwezo mkubwa wa kucheza winga ya kulia kwa ufasaha, huku akicheza pia akitokea kulia na kushoto.
Azam iliyokata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao imemsajili aliyekuwa kipa wa kikosi hicho Aishi Manula kutoka Simba, beki wa kati Lameck Lawi kutoka Coastal Union na kiungo Muhsin Malima aliyetoka ZED FC ya Misri.