CBE na SWUFE ya China wasaini ushirkiano katika tafiti na masomo

Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimesaini makubaliano na Chuo Kikuu cha Fedha na Uchumi cha Kusini Magharibi mwa China (SWUFE) kuimarisha ubadilishanaji wa ujuzi, utafiti wa pamoja, na fursa za mafunzo kwa wanafunzi na wafanyakazi wa pande zote mbili.

Mkataba huo ulisainiwa jana jijini Dar es Salaam baina ya Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga na Mwenyekiti wa Bodi y SWUFE, Zhao Jian Jun.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Profesa Lwoga alisema wamesaini mkataba huo ambao utawawezesha watumishi wa chuo hicho kuendelea kufanya shahada za uzamivu nchini China.

Alisema wanatarajia kuanza kutoa shahada ya kwanza kwenye uongozi wa biashara ambayo mwanafunzi atasoma miaka miwili akiwa CBE na miaka miwili atakwenda chuo cha SWUFE China kumalizia shahada yake.

“Mwanafunzi huyo akihitimu atakuwa na shahada inayotambuliwa na CBE na SWUFE, program hii itakuwa na msaada kubwa sana hasa wale ambao wangependa kwenda kusoma China wataanzia hapa CBE na mkataba huu pia utatusaidia kwenye masuala ya tafiti,” alisema

Alisema ushirikiano huo tayari umeisaidia CBE kuwa na kituo cha kukusanya data za uchumi na kuwezesha wanafunzi kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya fedha na uchumi. “Nafurahi kuona leo tumepiga hatua kubwa na ya muhimu kwa CBE kufungua milango ya kimataifa kwa maendeleo endelevu ya elimu ya biashara, fedha na TEHAMA na tumekubaliana kunzisha programu ya double degree katika Usimamizi wa Biashara (Business Administration) kuanzia mwaka wa masomo 2025/2026,” alisema

Aidha, alisema kupitia program hiyo wanafunzi watafaidika kwa kupata shahada mbili kwa pamoja moja kutoka CBE na nyingine kutoka SWUFE.

Profesa Lwoga alisema mpango huo utaongeza ushindani wa kimataifa kwa wahitimu wa CBE na kuwapa fursa ya kujifunza katika mazingira ya kimataifa.

“CBE tunajivunia kuwa mwenyeji wa tukio hili la kihistoria linalolenga kuimarisha mahusiano ya kimataifa na kukuza ubora wa elimu nchini Tanzania na tunaamini kuwa mkataba utanufaisha pande zote mbili,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa alisema ushirikiano huo utakuwa na msaada mkubwa kwa maendeleo ya chuo hicho kutokana na nchi hiyo kuendelea kwa kiwango kikubwa katika nyanja mbalimbali hasa katika masuala ya teknolojia.

Alisema mkataba na chuo hicho utaisaidia kuwawezesha wahadhiri wa chuo hicho kuongeza ujuzi nchini China na kuleta ujuzi huo kusaidia kwenye ujenzi wa Tanzania ya viwanda ambayo inahitaji rasilimali watu yenye utaalamu wa hali ya juu katika teknolojia.

“China imepiga hatua kubwa sana kiviwanda, leo hii tunashuhudia nguo na bidhaa mbalimbali kutoka Guanzghzoua China sasa je sisi tumepigwa marufuku kupeleka bidhaa zetu. Nasisi tutegeneze bidhaa za kuwapelekea kwenye masoko yao huko huko China, Marekani, Uingerea, Canada na kwingineko,” alisema

“Ushirikiano huo utawapa maarifa makubwa sana walimu yatakayowasasaidia katika kufundisha lakini pia ushirikiano huo utaisaidia nchi kupiga hatua katika eneo la viwanda kwa kupata wataalamu wengi,” alisema

Alisema chuo cha SWUFE kimebobea kwenye masuala ya uchumi na biashara

Ujumbe wa chuo hicho ulitembelea miundombinu ya CBE ikiwa ni pamoja na maktaba, maabara za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na idara za kitaaluma.






Related Posts