Katika hatua ya kihistoria kwa maendeleo ya miundombinu nchini, serikali ilishakamilisha ujenzi wa Daraja la JP Magufuli maarufu Kigongo–Busisi, ambalo ni refu zaidi kwa nchi za Afrika Mashariki.
Daraja hili lina urefu wa zaidi ya kilomita 3.2, upana wa mita 28 na linauwezo wa kubeba tani 180 na magari 1600 kwa mara moja. Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekamilisha mradi huo mkubwa uliogharimu Sh700 bilioni 700, fedha zilizotolewa na serikali ya Tanzania.
Kupitia mradi huu, serikali imepunguza muda wa kusafiri kutoka saa tatu kwa kutumia feri hadi dakika nne kwa magari na watembea kwa miguu. Daraja hili si tu linaboresha usafirishaji na biashara baina ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, bali pia linafungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakulima, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida, hakika ni neema kwa wananchi
Kwa tafsiri pana, serikali inaonesha sasa dhamira ya kweli ya kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo ile iliyoanzishwa na Hayati Rais John Magufuli. Kwa mtazamo wangu, ufunguzi wa daraja hili ni ushahidi wa mshikamano wa uongozi, uzalendo na maono ya kujenga Tanzania mpya yenye miundombinu imara na maendeleo yanayogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania.
Ujenzi wa daraja hili umejengwa juu ya msingi wa dira ya maendeleo na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan. Licha ya changamoto mbalimbali ambazo nchi inapitia, ameonesha uthubutu, uvumilivu na uamuzi wa dhati kuhakikisha mradi unakamilika kwa kiwango cha juu na kwa wakati.
Katika wakati huu, ni wazi kwamba daraja hili ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Ni sehemu ya barabara kuu ya Geita–Mwanza, ambayo ni njia muhimu ya kiuchumi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na sehemu ya mtandao wa barabara za kimataifa zinazounganisha Tanzania na nchi jirani kama Uganda, Rwanda na Burundi.
Kupitia daraja la JP Magufuli, wananchi sasa watanufaika uwekezaji kwa sababu muda wa kusafirisha bidhaa umepungua. Gari lililokuwa likisubiri kivuko kwa saa 2 hadi 3 sasa linavuka kwa dakika chache tu. Hakuna tena gharama za kivuko, wala gharama kubwa za mafuta wala hatari ya bidhaa kuharibika kutokana na ucheleweshaji. Hii itakuza soko la ndani wakulima wa Mwanza na Geita wanaweza kuuza mazao yao kwa haraka na kwa ufanisi zaidi bila kuhofia kuozea njiani.
Daraja hili pia linafungua fursa za viwanda kwa kuboresha usafirishaji wa malighafi kama dhahabu, pamba na mazao ya chakula. Wagonjwa wanaweza kusafirishwa kwa haraka kutoka vijijini hadi hospitali kubwa za Mwanza au Geita. Huduma za dharura kama zimamoto, polisi na usafiri wa misaada zinapatikana kwa haraka zaidi. Vilevile, watoto wanaweza kufika shuleni kwa wakati na watumishi wa umma, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla wananufaika na miundombinu hii bora ya usafiri.
Kupitia daraja hili, usafirishaji wa bidhaa kutoka Mwanza kwenda Geita, Bukombe, Chato na maeneo mengine umeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu serikali imewawezesha wananchi kuuza bidhaa zao kwa bei nzuri kutokana na uhakika wa kulifikia soko tofauti na ilivyokuwa zamani.
Zile safari kati ya Busisi na Kigongo zilitegemea kivuko cha majini ambacho kilichukua hadi saa 3 kusubiri, gari moja lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Geita ilibidi lisubiri kivuko hadi magari mengine yasafirishwe.
Hali hii ilisababisha foleni kubwa hasa wakati wa mvua lakini sasa baada ya daraja kukamilika, magari na watu wanapita muda wote bila kusubiri. Na tukumbuke kwamba daraja hili linaunganisha barabara kuu ya Mwanza – Geita, sehemu muhimu ya barabara kuu ya kimkakati ya Mwanza – Bukoba – Kigali (Rwanda) na hata kwenda Uganda kupitia Mutukula.
Daraja linatoa uunganisho wa haraka na wa moja kwa moja kati ya mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kupitia Mkoa wa Kigoma. Hii imekuwa fursa muhimu kwa wananchi kuendeleza shughuli za uzalishaji na biashara na mataifa jirani. Zaidi ya mradi wa miundombinu, daraja hili ni alama ya matumaini, maendeleo na mshikamano wa kitaifa.
Ni zawadi kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na urithi ambao Rais Samia atakumbukwa nao kwa vizazi vingi. Uzalendo wake umejidhihirisha kwa vitendo kwa kujenga Tanzania ya kisasa inayounganisha watu, huduma na fursa.
Kwa muda mrefu, wananchi wa Kanda ya Ziwa hususan mikoa ya Mwanza na Geita walitegemea vivuko vya Kigongo na Busisi kuvuka Ziwa Victoria.
Safari hizi ingawa muhimu, zilikuwa na changamoto nyingi. Leo hali hiyo imebadilika. Kupitia uongozi wa Rais Samia, ndoto ya kuwa na daraja la kudumu imetimia.
Dk Bravious Kahyoza ni Mchumi Mtafiti, Mtaalamu wa Ubia kati ya sekta binafsi na ya umma. O626525757