Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele amesema ratiba ya uchaguzi mkuu 2025, wanatarajia kuiweka hadharani kati ya Julai 25 na Julai 26, 2025.
Amesema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa hotuba ya kuahirisha shughuli za Bunge la 12, Juni 27, 2025, INEC wameanza kuiandaa ratiba hiyo itakayojikita kuangazia matukio yote hadi kufanyika uchaguzi wenyewe.
Rais Samia amesema kwa mamlaka aliyonayo, Bunge atalivunja rasmi Agosti 3, 2025.
Hayo yanajiri huku vyama 18, vilivyosaini kanuni za uchaguzi huo vikiendelea kupambana kwenye michakato yake ya ndani kusaka wagombea wenye sifa wanaoweza kushindana na washindani na kuibuka na ushindi baada ya kuuza sera zao kwa wananchi.
Akizungumza na Mwananchi, leo Jumatano, Julai 9, 2025, Jaji Mwabegele amesema:” Tarehe ya uchaguzi tunatarajia kuiweka hadharani mwishoni mwa mwezi huu. Inaweza kuwa kati ya Julai 25 au Julai 26, 2025, hapo tutaweka hadharani ratiba ya uchaguzi.”
Kuhusu watendaji kwa maana ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kwenye vituo vya uchaguzi amesema tayari wameshatoa tangazo.
“Mwisho wa tangazo lile ni Julai 11, 2025 (kesho kutwa) na hapo tutawatangaza hadharani baada ya kuwateua,” amesema Jaji Mwabegele alipoulizwa hasa maandalizi yanavyokwenda ikiwemo tarehe ya uchaguzi mkuu.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Chadema kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi ili kiweze kushiriki uchaguzi huo, Jaji Mwabegele amesema labda wapate amri kutoka mahakamani lakini zaidi ya hapo ambaye hajasaini kanuni za uchaguzi huo hawezi kushiriki.
Aprili 12, 2025, vyama 18 vilisaini kanuni hizo jijini Dodoma huku Chadema ikiwa chama pekee chenye usajili wa kudumu hakikushiriki kwa madai wanataka kwanza mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ifanyike.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, John Heche amejibu hana mamlaka hayo ya kisheria na kikanuni ya kuwaamuria ni wakati gani? wanapaswa kwenda kusaini kanuni hizo.
“Hata hizo kanuni ambazo wao wanazisimamia hazimpi yeye mamlaka ya kutuambia tusaini lini au tusisaini. Tunachojua kanuni hizo mtu yeyote anaweza kusaini muda na siku yeyote anayotaka kabla ya uchaguzi ndivyo kanuni zinavyosema. Ingawa hadi sasa msimamo wetu, No reforms no election (Bila mabadiliko hakuna Uchaguzi),”amesema John Heche alipoulizwa baada ya maelezo ya Jaji Mwabegele.
Katika maelezo yake, Jaji Mwabegele amefafanua kuwa shughuli ya kusaini kanuni ilishapita tangu Aprili 12, 2025 na pande tatu zilisaini, yaani vyama vya siasa vyenye usajili kamili 18 vilikwepo, Serikali na INEC tulisaini kukamilisha hatua hiyo na tulishatangaza kwenye gazeti la Serikali.
“Wao walisema hawataki kusaini, unajua ni ninyi mnawasemea, kwanza hawajasema popote kama wanataka kusaini na msimamo wao ni No reforms no election na hawatashiriki uchaguzi, ndiyo maana hawatasaini,” amesema Jaji Mwabegele
Katika maelezo yake Heche, amesema Chadema hawana la kusema zaidi ya msimamo wao walioutoa mwanzo ni No reforms no election.
” INEC wanaposimamia hilo wanatakiwa kusema ni kanuni zipi na kifungu kipi kinawapa nguvu ya kuwapa wasaini au wasisaini,” amesema.