Kesi ya Nyundo na wenzake, shahidi aitwa tena mahakamani

Dodoma. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imemwita tena shahidi wa kwanza kwenye kesi ya kubaka kwa kundi na kumlawiti binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es salaam ili aje atoe maelezo ya muda sahihi walioutumia washtakiwa hao wakiwa na mwathirika kwa kutumia DVD zilizopokelewa mahakamani kama ushahidi.

Shahidi huyo ni mtaalamu wa kompyuta na simu kutoka Jeshi la Polisi, ambaye alisaidia kubaini wahusika kwa kutumia vielelezo vya kidijitali. Maombi ya kuitwa tena kwa shahidi huyo yaliwasilishwa na upande wa Jamhuri, wakieleza kuwa muda sahihi unaopatikana kupitia DVD hizo ni kiungo muhimu katika kuelewa mazingira ya tukio hilo.

Hata hivyo, upande wa waleta rufaa, ukiongozwa na Wakili Godfrey Wasonga, ulipinga ombi hilo kwa hoja kuwa sheria hairuhusu shahidi kuja kutoa ushahidi tena kwenye ngazi ya rufaa.

Baada ya mabishano hayo, Jaji anayesikiliza kesi hiyo Amir Mruma aliomba muda wa kupitia sheria ya ushahidi ili kutoa uamuzi kama shahidi huyo aletwe mahakamani kwa ajili ya kucheza DVD zilizopokelewa mahakamani kama ushahidi au laa.

Akitoa uamuzi mdogo leo Jumatano Julai 9, 2025 kuhusu kama shahidi huyo aje mahakamani au mtaalamu mwingine yeyote mwenye ujuzi wa kucheza DVD, Jaji Mruma ameagiza shahidi huyo au mtaalamu mwingine kuja mahakamani ili kucheza DVD hiyo.

“Nimefikiria maombi haya kwa makini kwa jinsi nilivyoweza lakini vilevile na hoja zilizoletwa na waleta rufani na ni dhahiri kwamba hoja iliyoko mbele yangu iwapo maombi hayo yakubalike au la, na kama yakikubalika ni kwamba yakubalike ili shahidi wa kwanza aitwe aje kuchezesha hii DVD ambayo imetolewa kama ushahidi hapa mahakamani.

Akitoa uamuzi mdogo kuhusu hoja hiyo, Jaji Amir Mruma alisema mahakama ina mamlaka ya kumuita shahidi aliyewahi kutoa ushahidi au mtaalam mwingine kwa mujibu wa Kifungu cha 147(4) cha Sheria ya Ushahidi.

“Kifungu hicho kinasema mahakama inaweza kuruhusu shahidi yeyote kuitwa tena kwa ajili ya kuhojiwa zaidi au kuulizwa maswali ya dodoso, na pande zote zina haki ya kufanya hivyo. Hii inatoa msingi wa kisheria wa shahidi huyo kuitwa tena,” amesema Jaji Mruma.

Amefafanua kuwa muktadha wa kesi hii ni tofauti kwani shahidi hatarudi kwa ajili ya kuhojiwa, bali kwa madhumuni ya kucheza DVD kama sehemu ya ushahidi muhimu unaotakiwa kupitiwa na Mahakama na pande zote katika mchakato wa rufaa.

Jaji Mruma amesema kuwa mahakama ya kwanza ya rufaa ina jukumu la kuipitia upya kesi na kutathmini ushahidi uliotolewa awali, na si tu kujiegemeza kwenye uamuzi wa mahakama ya chini. Kwa msingi huo, mawakili wa pande zote wana wajibu wa kupitia upya ushahidi na kuisaidia mahakama kufikia uamuzi wa haki.

“Sheria haijabana mamlaka ya mahakama ya rufani ya kwanza wala ya pili, bali imetaja tu ‘mahakama’ kuwa na uwezo wa kumwita shahidi au mtu yeyote atakayesaidia katika kutenda haki,” ameongeza.

Amesisitiza kuwa lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha kuwa haki inatendeka, hasa pale panapojitokeza ushahidi muhimu ambao haukuwepo awali au haukuzingatiwa ipasavyo.

Kwa msingi huo, Mahakama imeridhia ombi la Jamhuri na kuelekeza kwamba shahidi wa kwanza au mtaalamu yeyote aliyehitimu na kuthibitishwa katika Tehama aitwe mahakamani ili kucheza DVD hiyo mbele ya mahakama, upande wa rufaa na wajibu rufani. Hii itawawezesha wote kutoa hoja zao kwa usahihi kabla ya mahakama kufikia uamuzi wake wa mwisho.

“Lengo letu ni moja tu, kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote,” amehitimisha Jaji Mruma.

Wakata rufaa kwenye kesi hiyo ni MT. 140105 askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) Clinton Damas maarufu kwa jina la Nyundo, Amini Lema (Kindamba), Nickson Jackson (Machuche) na C. 1693 WDR askari Magereza, Praygod Mushi

Baada ya kutoa uamuzi huo mdogo pande zote mbili zilikubaliana na uamuzi huo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 5, 2025 ambapo shahidi huyo au mtaalamu mwingine atakuja mahakamani kucheza DVD hizo.

Related Posts