Kibano malipo YouTube chaja, wategemea AI ‘mmekwisha’

Dar es Salaam. Mtandao wa YouTube umetangaza kuja na sera mpya itakayogusa hadi eneo la malipo ambapo ili upate pesa lazima utengeneze video za uhalisia na sio za ubunifu kama za Akili Mnemba (AI).

Ikumbukwe kwa watu wenye akaunti za YouTube wenye sifa za kulipwa ni wale walio na watu 1,000 waliojisajili (Subscribers) na saa 4,000 za muda wa kutazama katika miezi 12 iliyopita.

Sera hiyo itakayoanza kutumika kuanzia Julai 15, 2025 YouTube imebadilisha namna ya kupata pesa na sasa ili kufuzu kwenye YouTube Partner Program (YPP), lazima utengeneze maudhui ya asili ikiwemo sauti halisi.

Kwa maana hiyo, video zenye sauti za AI na zisizo na ubunifu hazitapata tena pesa. Ikumbukwe baadhi ya wamiliki wa akaunti za YouTube wamekuwa wakiweka video za AI zisizo halisi.

Kufuatia sera hiyo sasa YouTube inakataza sauti za AI (AI-generated voices), maudhui yaliyorejewa au kurudiwarudiwa (reused/repetitive content) pamoja na video za automated au zisizo na uso (faceless/automated videos).

YouTube itatekeleza sheria hizo mpya katika sera zake za mapato ndani ya YPP, zinazolenga kuondoa maudhui yanayorudiwarudia ya kiotomatiki na yenye thamani ya chini. Mfumo unabainisha kuwa hatua hiyo inalenga kulinda watayarishaji halisi na kuinua ubora wa maudhui.

Kwa mujibu wa The Economic Times, sera hiyo inakuja ambapo kwa upande mwingine itapunguza mapato ya akaunti zinazochapisha video zilizozalishwa kwa wingi, zinazorudiwarudiwa au za gharama nafuu.

Imeelezwa watayarishaji sasa lazima waongeze thamani ya video zao, maoni au uhariri kwenye maudhui yaliyotumika ili kuepuka mkono wa sera hiyo.

Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia hilo, Mwanamaudhui wa YouTube nchini Tanzania, Rashid Mansa amesema hatua hiyo ina faida na hasara. Amefafanua kwa upande wa faida zitarudisha thamani ya kazi. Akitolea mfano waliokuwa wanaandaa kazi zao kupitia AI kuna namna walikuwa wanawadharau wasiotumia, pia itaondoa kurubuniwa kutazama maudhui ya uongo.

Kwa upande wa hasara amesema,  itarudisha ugumu wa kazi kwa wale waliokuwa wanatumia AI kwa nia njema kurahisisha kazi zao, pia kurudi nyuma kiteknolojia,” amesema Mansa.

Hata hivyo, YouTube inataka kuepusha tabia za kuchapisha aina moja ya video mara kwa mara bila tofauti au ubunifu. Maudhui yaliyohaririwa juujuu ili kuonekana mapya (mfano, kubadilisha rangi, kukatakata matukio, bila kuongeza thamani.

Aidha, Sera hiyo imeweka msisitizo kuwa maudhui yanayotegemea zaidi vipengele vinavyozalishwa na AI hayakatazwi, lakini waandaaji lazima waongeze thamani muhimu ya kibinadamu kupitia uchambuzi, tafsiri, au ubinafsishaji ili kustahiki kupata mapato.

Imeelezwa kutakuwa na ukaguzi mkali hata kama chaneli inatimiza masharti ya idadi ya waliojisajili na muda wa kutazama kwa YPP, YouTube sasa itakagua zaidi uhalisi wa chaneli husika kabla ya kuidhinishwa (verified).

Chaneli zinazoonekana kurudiarudia, zinazozalishwa kwa wingi, au zisizo halisi zitahatarisha kukataliwa kutoka YPP au kuondolewa ikiwa tayari zimejiandikisha. Lengo ikiwa ni kulinda waandaaji halisi na kuinua ubora wa jumla wa maudhui.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wake rasmi YouTube imesema ili kupata pesa sasa inataka watengenezaji wa maudhui kuweka maudhui ‘halisi’ na ‘ya kweli’.

“Kuanzia Julai 15, 2025 YouTube inahusisha (updates) miongozo yetu ili kubaini vyema maudhui yanayozalishwa kwa wingi na yanayojirudia.

Maudhui yaliyochukuliwa kutoka vyanzo vingine lazima yabadilishwe kwa kiasi kikubwa ili yaonekane kuwa halisi.

Sera hiyo pia inatarajiwa kuathiri maudhui ya clickbait, yaliyoundwa kwa kutumia templeti, na yaliyozalishwa na AI, hasa video zinazotumia sauti zinazozalishwa na AI au zinazotumia tena nyenzo za watengenezaji wengine wa maudhui kwa uhariri.

Hata hivyo, YouTube haijabainisha wazi ni adhabu gani watengenezaji wa maudhui wanaweza kukabiliana nazo kwa kukiuka sheria mpya.

Related Posts