KAMA wewe ni shabiki wa Yanga au Simba elewa kwamba hii inakuhusu, kwani imepiga kotekote na kuna mambo ambayo hupaswi kuyakosa.
Lakini, nyuma ya yote kuna kile ambacho kimekuwa kikiwaumiza zaidi mashabiki wa Simba kwa misimu minne mfululizo ambayo watani zao, Yanga, wamebeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kutembea mitaani vifua mbele.
Na katikati ya hayo, kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema wala hashangazwi na kiwango alichoonyesha kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua kwani alishawahi kuwaambia mabosi wake wa zamani kwamba kikosi hicho kinahitaji staa kama huyo, huku akishauri kuhusu usajili ujao.
Robertinho ambaye alitua Simba Januari 3, 2023, aliondoka Novemba 9, 2023 siku chache baada ya kuchezea kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Robertinho alisema alichofanya Pacome msimu wa 2024/25 hakijamshangaza kabisa kwa sababu alishamuona tangu msimu wake wa kwanza alipofika.
Alisema kuwa alishawahi kuwaaambia mabosi wa timu hiyo kwamba ili Simba irudi kwenye makali yake inahitaji kiungo jasiri na mwenye kasi kama raia huyo wa Ivory Coast.
“Pacome akiwa na mpira ukiwa kocha wa timu pinzani unakuwa na presha mbili, kuomba akosee hesabu zake au wachezaji wako waongezeke kupambana naye kwa nguvu na wafanikiwe kumtibulia hesabu,” alisema kocha huyo raia wa Brazil.
Pacome katika msimu uliomalizika hivi karibuni, alionyesha kiwango kizuri kilichowavutia wengi na kumtaja kwamba ndiye anastahili kuwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu Bara ambapo alifunga mabao 12 na asisti tisa akiisaidia Yanga kubeba mataji matano ambayo ni Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
Kuelekea msimu ujao ambapo Simba inatajwa kuingia sokoni kuimarisha kikosi, Robertinho ametoa ushauri wa wachezaji wanaopaswa kusajili ili kuirudisha timu hiyo kwenye ushindani wa mataji.
“Kama Simba ikiendelea kuchukua wachezaji wa kawaida itakuwa ngumu kupindua ufalme wa Yanga. Kwenye kuchukua mataji kitu kinachoniumiza bado mashabiki wa Simba wanakosa raha mbele ya Yanga.
“Nakumbuka mimi ndiye kocha wa mwisho kushinda mbele ya mabingwa hao wa Tanzania na makocha waliofuatia wameishia kupata aibu tu mbele ya Yanga kutokana na kikosi kipana ilichonacho.”
Simba imeshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya Yanga mara nne mfululizo, huku msimu huu ikipanda kutoka kumaliza nafasi ya tatu uliopita mpaka ya pili.
Katika mechi tano mfululizo baina ya vigogo hao, Yanga imeshinda zote ambazo ni Simba 1-5 Yanga (Novemba 5, 2023), Yanga 2-1 Simba (Aprili 20, 2024), Yanga 1-0 Simba (Agosti 8, 2024), Simba 0-1 Simba (Oktoba 19, 2024) na Yanga 2-0 Simba (Juni 25, 2025). Mara ya mwisho Simba ilishinda kwa penalti 3-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 13, 2023. Wakati huo Kocha alikuwa Robertinho ambaye mechi iliyofuatia alipokea kichapo cha 5-1 kutoka kwa Yanga.