Kwa nini takrima ije sasa?

Vijana wa leo hasa wa mijini hawaufahamu utaratibu tuliokuwa nao zamani, au unaoendelea hadi leo huko vijijini ambako hakujaathirika na umagharibi. Familia zetu zilikuwa pana zikihusisha moja kwa moja ndugu wa baba na ndugu wa mama. Pia familia moja iliweza kuhesabu watoto, wajukuu, vilembwe, vilembwekeze hadi vining’ina. Hivi sasa “singo-maza” anahesabu mtoto mmoja, kwisha. Mtoto hamjui baba wala babu.

Enzi zetu tulikuwa tukipokea fedha kutoka kwa wazazi kila tulipokuwa tukienda shuleni. Fedha hiyo haikuzidi shilingi kumi na ilitosha kununua ubuyu, karanga, kashata na visheti.

Hatukuwa na haja ya kuuliza matumizi yake kwani ilijieleza wazi kwamba ni ya matumizi wakati wa mapumziko pale shuleni. Lakini siku tuliyopewa zaidi ya shilingi hamsini ilibidi tuulize ilikuwa ni ya matumizi yapi.

Vivyo hivyo tulipowatembelea baba wadogo na wajomba wakati wa mapumziko ya mwisho wa wiki, tulikuwa na kawaida ya kupokea zawadi za wastani uleule tuliokuwa tukipewa na wazazi. Kadhalika hatukuuliza kwani ilijieleza kuwa ni nauli na mchango wa matumizi ya kawaida kama ya shule.

Na hatukushangaa kwani kiasi kama hicho wazazi wetu waliwapa binamu zetu walipokuja kututembelea nyumbani.

Hata tulipokuwa katika Shule za Sekondari (hasa kwa tuliosoma shule za bweni) tuliendeleza utaratibu huo.

Wakati huo kiasi cha fedha kiliongezeka, na tulitumia kununulia pamba kali za kuwakoga watoto wa bush huko tuendako.

Hata siku moja hatukuwahi kuzawadiwa fedha iliyotosha kununua baiskeli, labda kwa maombi maalum. Zawadi ilipozidi tuliuliza kuepuka kula ada au madeni ya shule.

Kuna usemi wa waswahili kuwa mtu anapokupa kitu bila sababu basi kuna sababu. Wapo wazazi waliokosana na watu baada ya kugundua watu hao walikuwa wakiwapa vitu watoto wao. Haya yanaendana na mila na desturi za eneo husika, na utamaduni waliojipangia wakazi wake. Si vizuri kumzoesha mtoto wa mwenzako kula pizza wakati nyumbani kwao hata kupata mkate ni ishu kubwa.

Hatari hii inaonekana zaidi hapa nchini nyakati za uchaguzi. Anatokea mtu na gari lake lenye thamani ya kijiji kizima, nawakumbusha kuwa yeye ndiye yule mbunge mliyemchagua kwenye chaguzi zilizotangulia. Anawaambia kuwa amewamiss sana na amekuja kuwapa zawadi ndogo. Kwa kuwa mnaonekana kuvurugwa na njaa, mnashindwa kumwuliza inakuwaje kukumbukana kwenye misimu kama hii tu.

Huyu bwana mkubwa anawafanyia sherehe ya pilau, bia na nyamachoma ambayo hamjapata kuiona tangu mlipozaliwa.

Wanakijiji mnapata fulana, kofia, khanga na vitenge, bila kusahau bahasha zenye “Wekundu wa Msimbazi” wanaokaribia kuchana vifungashio. Kwa ufupi kila baada ya zaidi ya miaka minne ya njaa, inakuja siku moja yenye neema ya kufurisha ukame wa miaka yote hiyo.

Ningelikuwa Nabii Yusufu wa enzi hizi wala nisingepata taabu ya kutafsiri ndoto. Yeye alitafsiri ndoto ya Mfalme kuwa itaanza miaka saba ya neema itakayofuatiwa na miaka saba ya njaa.

Hivyo akamtaka aweke akiba kukabiliana na njaa. Kwa wakati huu mimi ningesema “inaanza miaka mitano ya njaa inayofuatiwa na siku moja ya shibe. Hivyo muweke akiba maana mzigo unaotoka siku hiyo moja unaweza kutosheleza awamu nzima”.

Viongozi wabovu huweza kuwaacha na njaa yenu ya muda mrefu, wakawasahaulisha kwa siku moja tu bila kufuata utaratibu.

Lengo ni kuwanyonya tena katika awamu inayofuata. Na njaa hizo elekezi, daima mwenye shibe humtumikisha aliye na njaa. Sio dhambi kumshukuru yule anayekunusuru dhidi ya adui njaa, lakini utaratibu ni lazima ufuatwe.

Mimi niliwahi kuishi jirani na familia mbili zilizokuwa na uwezo tofauti sana.

Familia moja ilikuwa na ukwasi wa kuwapeleka watoto shuleni kwa magari, lakini ile ingine haikuwa na uwezo wa kusomesha watoto wao. Hawa masikini walikuwa na mtoto aliyekuwa akilia pindi alipowaona wenzake wakienda shuleni. Alikuwa akigoma kuswaga mifugo malishoni kwa kudai elimu, na mara zote aliishia kuchapwa viboko.

Yule mzee tajiri alikuwa msomi na aliielewa sana hali ile kwani naye alisomea kijijini. Ilibidi afanye urafiki na yule mzee masikini.

Urafiki wao ulifikia hatua ya udugu, wakaafikiana kusaidiana ili mtoto huyu mdogo aende shuleni. Hivyo huyu mtoto akawa akishinda kule kwa matajiri wakati wote mara atokapo shuleni. Alinunuliwa sare na vifaa vingine sawasawa na watoto wa tajiri.

Hii sio hatari bali ni sehemu ya maendeleo. Mtoto huyu akikua ataikomboa familia yake kutoka kwenye majanga ya ujinga na umasikini.

Hatari ingekuja pale tajiri angekuwa akimsaidia mtoto bila kufuata utaratibu. Kwa mfano angemzoesha zawadi, mtoto masikini angepatwa na uraibu.

Angehitaji zawadi hizo wakati wazazi wake hawana uwezo wa kumpatia, hivyo angezitafuta kwa njia haramu. Watanzania wote tuwe na utaratibu wa kuhoji tunavyopewa. Kapuku anaweza kupokea kutoka kwa mkwasi, lakini kwa utaratibu maalum. Ule usemi wa “kuleni rushwa zao kisha msiwapigie kura” ufutwe kabisa.

Hata ibadilishwe na kuitwa majina mazuri kama zawadi au takrima, rushwa inabaki kuwa adui wa haki; mtoaji na mpokeaji wote ni wadhambi. Kama zawadi tuelezane kwa nini iwe sasa na si wakati mwingine?

Related Posts