Kwa Raizin simu zinaita sana

STRAIKA na kinara wa mabao katika Championship msimu uliopita, Raizin Hafidh amesema licha ya kupokea simu nyingi kutoka timu kadhaa kuhitaji huduma yake, lakini bado hajaamua huku akitaja dau ili kunasa saini yake.

Nyota huyo mwenye rekodi ya kupandisha timu Ligi Kuu, alikuwa mfungaji bora Championship akitupia mabao 22 katika mashindano yote na kuirejesha Mtibwa Sugar Ligi Kuu.

Hafidh aliyewahi kutamba na timu kadhaa, anakumbukwa kwa kuipandisha Coastal Union, Gwambina, huku aking’ara na Dodoma Jiji na Mbeya Kwanza kwa misimu tofauti hadi kuzitoa umate timu nyingine kuhitaji huduma yake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Straika huyo amesema tangu amalize Championship simu zimekuwa nyingi, lakini hakuna alipothibitisha akisubiri dau alilojiwekea kutimia aweze kuamua.

Amesema zipo timu zaidi ya sita ikiwamo mojawapo iliyotuma pesa kwenye akaunti na kuamua kuzirejesha, huku akifichua yeyote anayetaka huduma yake msimu ujao aweke Sh100 milioni za usajili na mshahara usiopungua Sh3.5 milioni.

“Sina haraka na maisha, pia hii ndio kazi yangu, simu napokea nyingi ila sijaamua, kuna timu imetuma hela kiasi fulani (Mwanaspoti inajua) lakini nimezirudisha.”

“Timu yenye nia kupata saini yangu nahitaji Sh100 milioni za usajili na mshahara usipungue Sh3.5 milioni, sitaki yajirudie yaliyowahi kunikuta huko nyuma, majukumu kwa sasa ni mengi,” amesema staa huyo.

Ameongeza licha ya kwamba amefikia kiwango cha juu kucheza soka la ushindani hasa Ligi Kuu, lakini yeye anachoangalia ni masilahi kwanza, hivyo hata Championship kwake ni freshi.

“Kwa jumla ligi ilikuwa ngumu, lakini kwa mipango ya Mungu niliweza kufanya vizuri, kupandisha timu ni mwendelezo wangu ikiwamo Coastal Union, Gwambina na sasa Mtibwa Sugar,” ametamba mkali huyo wa nyavu.

Related Posts