KAMA ulikuwa unadhani Heritier Makambo aliyekuwa Tabora United na kudaiwa ametimka ndo kaondoka kimoja? Umekosea, kwani jamaa bado yupo sana Bongo baada ya kudaiwa yupo hatua ya mwisho kujiunga na Namungo.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limepenyezewa ni kwamba uongozi wa Namungo uko katika mazungumzo ya kupata saini ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga baada ya mkataba wake na Tabora Utd aliyojiunga nayo Agosti 1, 2024 kumalizika huku kukiwa hakuna mpango wa kusaini mpya.
Makambo aliyejiunga na Tabora Utd akitokea Al Murooj ya Libya, ameachana na timu hiyo na sasa uongozi wa Namungo unamtaka akaongeze nguvu kwa ajili ya msimu ujao, huku mazungumzo baina ya pande zote mbili yakiendelea vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, alisema tayari wameanza maboresho ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao, ingawa taratibu za utambulisho wao zitafuata katika ukurasa rasmi wa timu hiyo, muda wowote kuanzia sasa.
“Mchezaji yeyote ambaye atapendekezwa na benchi la ufundi iwe ni kwa kumsajili au kuachana naye tutazingatia hilo. Wapo ambao tutaachana nao ili kupisha sura nyingine ambazo muda wowote tutazitambulisha katika kikosi chetu,” alisema Ally. Licha ya kauli hiyo ya Ally, ila Mwanaspoti linatambua Makambo aliyechezea timu mbalimbali zikiwezo za, DC Motema Pembe na Saint Eloi Lupopo za kwao DR Congo na Horoya AC ya Guinea, anakaribia kujiunga na kikosi cha ‘Wauaji wa Kusini’.
Mbali na Makambo anayekaribia kujiunga na timu hiyo, wengine ni Cyprian Kipenye kutoka Songea United, Abdulaziz Shahame (TMA FC) wote wakitokea Ligi ya Championship na kiungo mshambuliaji, Lucas Kikoti anayerejea tena akitoka Coastal Union.
Msimu wa 2024-2025, Makambo alihusika na mabao tisa Ligi Kuu Bara akiwa na Tabora United baada ya nyota huyo kufunga matano na kuasisti manne, akiiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya tano kwenye msimamo na pointi zake 38.