LEO Kituo cha Michezo na Shule za Alliance za jijini Mwanza zimesherehekea miaka 25 tangu kuanzishwa kwake na kuenzi miezi sita ya kifo cha muasisi wake, James Bwire katika bonanza la Alliance Day.
Bonanza hilo limefanyika katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza likijumuisha shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na kuhitimishwa kwa mchezo wa hisani kati ya timu ya wachezaji waliowahi kupita Alliance (team Israel Mwenda) dhidi ya kikosi cha Kombaini ya wachezaji wa timu za Ligi Kuu wakiwemo wa Simba, Yanga, Azam na JKT Tanzania (team Maxi Nzengeli).
Bonanza hilo lilitumika pia kuchangisha Sh100 milioni za kusadia kuendeleza vipaji, kusomesha na kuwalea vijana 200 wenye vipaji kutoka familia duni wanaolelewa katika kituo cha Alliance, na kuboresha miundombinu ya viwanja na kusaidia maandalizi ya Alliance FC inayokusudia kupanda Ligi ya Championship.
Umati mkubwa wa mashabiki na wadau wa Soka jijini Mwanza ulijitokeza kwenye Uwanja wa Nyamagana kuwashuhudia wanasoka mbalimbali wakiongozwa na Mwenda, Maxi na Kibwana Shomari.
Katika mchezo huo uliopigwa kuanzia saa 10:44 jioni, kikosi cha mastaa wa Ligi Kuu kikiongozwa na Maxi kimeibuka na ushindi wa penalti 4-2 mbele ya kikosi cha Alliance All Stars baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 2-2.
Alliance All Stars ilipata mabao yake kupitia kwa David Ulomi dakika ya 27 akimalizia krosi ya Israel Mwenda, huku Hassan Kachwele akifunga bao la pili dakika ya 50 kwa shuti kali nje ya eneo la 18.
Mabao ya mastaa wa Ligi Kuu, yamefungwa na Habib Kyombo dakika ya 37 na Said Ndemla dakika ya 39 akifunga kwa shuti kali nje ya 18 likimshinda Kipa Amos Tiba na kukaa wavuni.
Kikosi cha Kombaini ya wachezaji wa Ligi Kuu kilichoanza ni pamoja na Abubakar Khomeiny (Yanga), Kibwana Shomari (Yanga), Nickson Kibabage (Yanga), Hussein Kazi (Simba), Bakari Mwamnyeto (Yanga), Said Ndemla (JKT Tanzania), Himid Mao (Azam), Hassan Dilunga (JKT Tanzania), Max Nzengeli (Yanga), Habib Kyombo (Pamba Jiji) na Mwana Kibuta (Dodoma Jiji).
Kikosi cha Alliance All Stars kilichoanza kwenye mchezo huo ni Amos Tiber, Israel Mwenda, Dickson Mabundo, Joseph Majagi, Zabona Mayombya, Mourice Abraham, Juma Nyangi, Siraji Juma, David Uromi, Martin Kiggi na Deusdedith Okoyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda
amesema taasisi ya Alliance imekuwa na mchango chanya katika sekta ya elimu na michezo na leo jamii na taifa limevuna matunda ya uwekezaji ambayo yalifanywa na James Bwire kwa miaka 25.
Amesema Bwire alikuwa ni kiongozi imara na katika mkoa wa Mwanza ni mmoja kati ya watu ambao wana mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya michezo na Tanzania ka ujumla.
”Tunawapongeza kwa kubuni tamasha hili, wito wangu muendeee hivyo najua mna timu ya wanawake iko Ligi Kuu mjiandae kwenye ligi msiwe wasindikizaji. Wito wangu kwa wananchi wa Mwanza na wadau wa michezo kuendelea kusapoti timu za Mwanza ambazo ziko kwenye mashindano mbalimbali,” amesema Mtanda.
Mtanda pia amewapongeza wachezaji waliojitokeza kunogesha tamasha hilo kwani linaonyesha wanavyojaliana na kushirikiana, huku akimpongeza Israel Mwenda kwa kuhamasisha wachezaji wenzake wa Yanga kuja Alliance Day.
”Niwapongeze wachezaji wote ambao mmeamua kuja na kumuunga mkono mwenzenu Israel (Mwenda), hii inaonyesha muunganiko nyie ni mfano mzuri kwa jamii yetu,” amesema Mtanda na kuongeza;
”Hii inatuma ujumbe kamba nyinyi wenyewe mnashirikiana na mnapendana, mmeacha kazi zenu na majukumu yenu hivi ndivyo inavyotakiwa kuwa.”
Mkurugenzi wa Shule za Alliance, Esther Marwa amesema tamasha hilo linawakalisha historia ya uwepo wa taasisi ya Alliance ambapo wanaenzi na kukiendeleza alichokiacha James Bwire aliyefariki Januari 26, 2015.
Amesema Bwire alikuwa ni mwalimu aliyejitoa kuhakikisha watoto wanaotoka familia duni wanaishi ndoto zao, ambapo wanatumia tamasha hilo kusaidia watoto zaidi ya vijana 200 wasiojiweza wenye vipaji kuwasomesha, kuwapa vifaa vya michezo na malezi bora ili kufikia ndoto zao.
”Tunaamini kwa umoja wetu tutalinda urithi wa mwalimu James Bwire na tunaomba wadau kuendelea kutuunga mkono katika kulea watoto wenye vipaji kufikia ndoto zao,” amesema Esther.
Amewasihi wazazi kujifunza kwa Bwire kwa kujitoa na kusaidia na kuendelea kuziamini shule na kituo cha Alliance kwa kuleta watoto wenye vipaji wafikie ndoto zao kitaaluma na michezo leta watoto katika shule hiyo ili wafikie ndoto zao. Amesisitiza tamasha hilo litakuwa kubwa na mwaka ujao litafanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Khalid Bitebo, amekipongeza kituo hicho kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya soka la mkoa huo, huku Mwenyekiti wa Alliance, Stephano Nyaitati akiahidi kuhakikisha wanaendeleza na kuyaishi kwa vitendo mambo aliyoyaacha James Bwire kwani hata tamasha hilo ni miongozo wake aliouacha.