Mwekezaji mwendokasi Mbagala kumaliza kero abiria kupandia madirishani

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku chache kuanza kwa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) maarufu ‘mwendokasi’ katika Barabara ya Gereza-Mbagala, Kampuni ya Mofat iliyopewa zabuni ya kutoa huduma hiyo, imeeleza namna ilivyojipanga kukabiliana na changamoto zilizoonekana wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo.

Changamoto hizo ni pamoja na abiria kukaa muda mrefu vituoni kusubiri usafiri na kusongamana kwa abiria vituoni na ndani ya mabasi.

Wakati awali mradi huo ilikuwa ni mtu asikae zaidi ya dakika tano kituoni, lakini kutokana na uhaba wa mabasi uliopo sasa inachukua hadi saa mbili kwa abiria kusubiri usafiri na kuondoa maana nzima ya mabasi yaendayo haraka.

Mwananchi, liliwahi kuripoti kuhusu adha zinazowakabili abiria wanapokwenda kupanda usafiri huo, ikiwemo kutumia muda mrefu vituoni, kupambania nafasi ya kupanda basi na hata kusongamana ndani ya basi hususan nyakati za asubuhi na jioni.

Mkakati wa kuepuka changamoto

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika jana Jumanne, Julai 8, 2025, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Kampuni ya Mofat, Mabrouk Masasi amesema tayari wamejifunza kutokana na changamoto zilizoshuhudiwa katika awamu ya kwanza, iliyohusisha barabara ya Morogoro.

“Ni kweli watu wamekuwa wakilalamika kukaa muda mrefu vituoni kusubiri usafiri, lakini sisi katika mikakati yetu ni kuona kila baada ya dakika mbili hadi tatu basi linafika kituoni ambapo hilo litafanikiwa kutokana na kuwa na mfumo wa ufuatiliaji magari (ITS) na pia kuwa na control room (chumba cha uthibiti) yetu ambayo tutaiweka katika kituo kikuu kilichopo Mbagala.

“Tutafanya hivi tukiamini kutaondoa adha ya watu pia kusukumana kwa lengo la kugombea wakati wa kupanda kwa kuwa wana uhakika baada ya dakika chache litafika basi jingine,” amesema Masasi.

Amesema tathmini ya aina ya abiria imeshafanyika na wamehakikisha mabasi yanayotumika ni imara zaidi ili yasiharibike ndani ya muda mfupi.

Ndani ya basi hilo jipya, amesema vitatumika viyoyozi na hakutakuwa na utaratibu wa kufungua madirisha kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari.

Amesema anaelewa uhalisia wa aina ya abiria hasa wa Mbagala, lakini ana hakika kadri siku zinavyokwenda wataelemika na kupanda kistaarabu kwa kuwa hata maeneo ambayo watu wanadhani abiria wake wamestaarabika bado wanapanda usafiri wa umma kwa vurugu.

“Katika hili tutajitahidi mara kwa mara kutoa elimu, lakini pia kwa kuwa magari yatakuwa megi hatuamini kwamba changamoto hizo zitajitokeza za mara watu wamedandia madirishani au kusukumana,” amesema.

Zaidi ya 5,000 wajitokeza kuwaomba ajira

Anasema watu zaidi ya 5,000 wamejitokeza kuomba ajira, baada ya tangazo walilolitoa linaloisha Juni 30, 2025.

Anaeleza katika tangazo idadi kubwa ya nafasi zaidi zilizotangazwa ni udereva ambapo 255 wanatakiwa ikifuatiwa na wahudumu katika vituo vya abiria (nafasi 158).

Idadi hiyo ya madereva ni sawa na idadi ya mabasi yatakayoletwa na Mofat, licha ya kuwa kwa barabara ya Mbagala pekee Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), umesema unahitaji mabasi 700.

Akizungumzia mwitikio huo, Masasi amesema ukweli ni kwamba hawawezi kuwaajiri watu wengi kwa sasa, kwa kuwa nao wanategemea kadri mabasi yatakapofika ndipo watakapoongeza watu ambapo katika awamu ya kwanza mabasi 100 yanatarajiwa kuwasili hadi ifikapo Agosti 15 na hayo yatakapofika tutaanza kuingia nayo barabarani kufanya kazi .

“Pia, hadi kufika Septemba mwaka huu mwanzoni tutakuwa tumemaliza kuleta magari mengine 155 yatakayokuwa yamesalia na hivyo kukamilisha idadi ya mabasi 255 tunayotakiwa kuyaleta,”amesema.

Amesema wameweka zaidi ya dola milioni 76 sawa na zaidi ya Sh197 milioni, fedha zitakazotumika katika ufungaji mifumo yakiwemo mageti janja kwa ajili ya ukusanyaji nauli na shughuli nyingine za uendeshaji.

Wakitoa maoni yao kuhusu hilo, wakazi wa Mbagala akiwemo Maimuna Shabani mkazi wa Mbagala Kuu, amesema kwa sasa hawezi kuwa na meneno ya kusema kwa kuwa ahadi zimekuwa nyingi kuliko utekelezaji.

“Mimi nitafute nikupe maoni siku ambayo nitayaona mabasi yameingia barabarani na kupanda, kwani haya hatujaanza kuahidiwa leo, zimekuwa kama hadithi, acha tuone yakapokuja ndio tuongee,” amesema Maimuna.

Naye, Feruzi Kilangali mkazi wa Chamazi amesema huduma hiyo imekuja wakati muafaka kwani eneo la Mbagala kwa sasa imekuwa kama kituo kikubwa cha watu kukutana wakitoka maeneo ya pembezoni ikiwemo Chanika, Mbande,Chamazi, Kisemvule, Vikindu na baadhi wakitokea mkoa wa Pwani ikiwemo Mkuranga na Rufiji.

Pamoja na hilo, Feruzi amesema hakuna gari za Karikaoo zinazoanzia hapo, na hivyo abiria kulazimika kusubiri gari zinazotoka pembezoni mwa mji ambazo nazo zikishafika hapo tayari zinakuwa zimejaa na hivyo watu kupata tabu ya usafiri.

“Ni kutokana na hilo, Kariakoo ambayo haizidi dakika kumi unatakiwa uwe umefika lakini mtu hatumia hadi zaidi ya saa moja. Hivyo ujio wa mabasi hayo sio neema tu kwa abiria wa kawaida lakini pia wafanyabiashara ambao wamekuwa wakienda Kariakoo kuchukua bidhaa,”amesema Furuzi.

Juni 3, 2025, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuma Kihamia amesema suala la uwekezaji unaoendelea lengo ni kuhakikisha suala la hali ya usafiri wa kugombania au kusubiria muda mrefu:”Sasa litakuwa historia, na wazawa wenye uwezo wa kimitaji na kiuendeshaji wanashauriwa kuchangamkia zabuni hizi kwani bado zinaendelea kwa barabara za Mwenge hadi Tegeta na zile za Gongo la mboto hadi mjini na pia na nyinginezo kadri zitakavyotangazwa.”

Walichokisema Uwamada, Darcoboa

Umoja wa madereva na Makondakta Mkoa wa Dar es Salaam (Uwamada), wamepongeza hatua hiyo huku akishauri wakati mwekezaji huyo akianza kazi kutengenezwe mfumo mzuri na wao kupata kazi hiyo.

Mwenyekiti wa Uwamada, Shukuru Mlawa amesema:”Sisi tayari ni madereva wenye uzoefu wa muda mrefu wa kupakia abiria hususan wa Jiji la Dar es Salaam na kinachoongezeka hapo ni mabasi ya kwenda haraka lakini abiria ni walewale, kikubwa tupewe mafunzo mafupi tuweze kuingia barabarani,”amesema Mlawa.

Akijibu hilo, Ofisa wa Mofat amesema wao walitoa tangazo hadharani hivyo ana imani wapo madereva kati yao walioomba na endapo watakuwa na sifa zinazotakiwa wataajiriwa.

Kwa mujibu wa tangazo liliotolewa na kampuni hiyo ambalo Mwananchi imeliona moja ya vigezo ni mwombaji awe na elimu ya kuanzia kidato cha nne na kuendelea.

Kuhusu kukosa ajira endapo mwendokasi itaanza safari katika njia hiyo, Mlawa amesema hakuna kitu kama hicho, kwani usafirishaji abiria bado unahitajika maeneo mbalimbali katika jiji hilo na kuongeza kwamba ndio maana hata katika barabara ya Morogoro kila wakati Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) umekuwa ukiitaka watu kupeleka daladala.

Mpaka sasa Latra ishatangaza zaidi ya mara mbili kuingizwa kwa daladala katika barabara ya Morogoro ikiwemo ruti ya kutokea Mbezi hadi Mwananyamala na Mbezi kwenda Mnazi Mmoja, lengo likiwa kukabiliana na uchache wa mabasi ya mwendokasi ambapo huwalizimu abiria kuchukua muda mrefu kusubiri vituoni.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk amesema kuongezeka kwa mwekezaji huyo ni njia ya wao kuendelea kujifunza katika utoaji wa huduma za usafiri.

“Ujio wa mwekezaji huyo unatupasa na sisi wamiliki tuchukue hatua ya kubadilika ili kuendana na wakati kwa kuwa katika safari hiyo ya usafirishaji tumepitia mengi kuanzia kusafirisgakwa kutumia gari aina ya hiece maarufu vipanya, ikaja DCM, Tata, Hier na sasa mwendokasi,” amesema Mabrouk.

Related Posts