MWENGE WA UHURU WAWAVUTIA WATALII NGORONGORO

Na Mwandishi wetu Ngorongoro.

Baadhi  ya watalii waliokuwa katika safari zao za kawaida kwenye eneo la hifadhi ya Ngorongoro leo jumatano  tarehe 9 Julai 2025 walijikuta katika furaha baada ya kushuhudia   Mwenge wa Uhuru ukiingia wilayani Karatu kutokea wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha.

Watalii hao walionekana wakisimamisha magari yao ili kushuhudia namna Mwenge wa Uhuru   ambao ni alama ya Taifa unavyokimbizwa katika eneo hilo huku wakimbiza mwenge wakiwa katika hali ya furaha na kutoa hamasa kwa wananchi.

“Leo nimepata faraja kubwa kuuona kwa macho yangu Mwenge wa Uhuru nikiwa Tanzania, nimekuwa nikisoma historia na simulizi za mwenge huu na namna unavyowaunganisha watanzania, binafsi naona ni jambo jema na lenye mafunzo hasa kuona Watanzania kwa umoja wao wanaunganishwa na kitu chenye historia kwa nchi yao“,alisema Bi Gracay Anderson kutoka nchini Hungary.

Jambo kubwa lililowafurahisha  watalii hao ni kuona jinsi mamia ya wananchi walivyojitokeza katika eneo la njia panda Karatu kuupokea Mwenge na kuukimbiza Katika Wilaya ya Karatu wakiongozwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa, dini pamoja na wasanii kutoka makabila ya wamasai, wadatoga na wahadzabe.

“Nimependa kuona watanzania katika umoja wao wanakimbiza mwenge huu, sisi kwetu tunasoma tu habari za Tanzania na vivutio vyake lakini leo nimeamini kwamba tunaposikia hii ni nchi ya amani kweli inadhihirika wazi kuwa viongozi wenu wamefanya kazi kubwa kuwafanya kuwa na umoja na mshikamano”,alisema Bwana Lionel Greenwich kutoka Uingereza.

Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa sasa limekuwa likipokea idadi kubwa ya watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani ambapo katika kipindi hiki kumekuwa na hamasa kubwa ya wageni hao kutembelea eneo hilo kufuatia jitihada za serikali na wadau wa Sekta binafsi kutangaza vivutio vya utalii duniani.


Related Posts