NMB Yapewa Tuzo Maalum na WCF kwa Uzingatiaji Bora wa Uwasilishaji wa Michango ya Wafanyakazi

 

Dar es Salaam

Benki ya NMB imeendelea kuthibitisha uongozi wake katika masuala ya rasilimali watu baada ya kutunukiwa tuzo maalum na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kuzingatia kikamilifu kanuni na uwasilishaji wa michango kwa wakati.

Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya WCF yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, yakihusisha viongozi wa serikali, wadau wa ajira, waajiri na mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka sekta mbalimbali nchini.

Tuzo kwa NMB ilipokelewa kwa niaba ya benki hiyo na Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Onesmo Kabeho.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), aliipongeza menejimenti ya WCF kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake kwa kipindi cha miaka 10. Alimpongeza pia Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, kwa kuendelea kuiongoza taasisi hiyo kwa weledi na mafanikio tangu kuanzishwa kwake.

Mhe. Majaliwa alisisitiza kuwa huduma za fidia kwa wafanyakazi si suala la hiari bali ni haki ya msingi inayopaswa kulindwa na kusimamiwa kwa uwajibikaji wa hali ya juu. Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanya maboresho ya maslahi ya wafanyakazi ili kuhakikisha haki na usawa mahali pa kazi vinaimarika zaidi.

Kaulimbiu ya mwaka huu, “Miaka 10 ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi: Kazi Iendelee,” ilielezwa na Waziri Mkuu kuwa inaakisi mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha muongo mmoja.

Kupitia tuzo hii, NMB imedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kuwa mwajiri anayeongoza kwa kuzingatia haki, ustawi na usalama wa wafanyakazi wake, sambamba na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.



Related Posts