Tanga. Biashara ya samaki mkoani Tanga imekuwa ngumu baada ya bidhaa hiyo kuadimika, huku wafanyabiashara wakilia kutokana na bei nayo kuongezeka kila kukicha.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti katika soko la samaki la Mwalo wa Deep Sea jijini Tanga leo Jumatano Julai 9, 2025 wafanyabiashara hao wamesema samaki hawapatikani kwa wingi, hali inayosababisha wachache wanaopatikana kuuzwa kwa bei ya juu.
Mfanyabiashara wa samaki kutoka Wilaya ya Muheza, Mwanahamisi Athumani amesema hali ni ngumu na wanashinda sokoni hapo kutwa nzima, ila hawapati mzigo wa uhakika na wakati mwingine inawabidi kuondoka kwanza.
Amesema kutokana na hilo bei pia zimekuwa juu kiasi cha kuwabana wale ambao wanakwenda kuuza mtaani, kwani ndoo ndogo ya lita 10 walikuwa wakinunua kwa Sh30,000 ila sasa ni Sh60,000.
Ameongeza kuwa kutokana na bei hizo inawapa wakati mgumu kwao kuanzia kwenye kununua hadi kuuza sokoni, kwani mwananchi akiulizia na kuona bei ipo juu anaacha na kuondoka, hivyo kuwabidi kuuza kwa bei ya hasara.

Mfanyabiashara wa dagaa aina ya Uono Fatuma Almasi akinunua bidhaa hiyo kwa mchuuzi ambae ni mvuvi Khalid Ahmed katika soko la Samaki la Mwalo wa Deep Sea jijini Tanga. Picha na Rajabu Athumani.
Aidha Mariam Jumbe mfanyabiashara kutoka eneo la Magomeni jijini Tanga, amesema kwa sasa fungu moja la dagaa inawabidi kuuza Sh5,000 badala ya Sh2,000 ya awali na fungu la Sh5,000 wanauza kwa Sh10,000 ili kuendana na hali ya sokoni.
“Samaki mmoja wale wakubwa kwa sasa anauzwa kuanzia Sh100,000 hadi Sh190,000 je, wewe mfanyabiashara utakwenda kuuza bei gani ili upate faida, hapa tunatafuta hela ya kula tu hadi pale hali ya hewa itakapokuwa vizuri,” amesema Mariam.
Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Mkoa wa Tanga, Bahelo Wazio amesema sababu ya uwepo wa uhaba wa samaki ni mabadiliko ya misimu ambapo kwa sasa ni msimu wa kusi ambapo kunakuwa na upepo mkali baharini.
Amesema kutokana na uwepo wa upepo na baridi samaki hushuka chini ya bahari hivyo ni ngumu wavuvi kupata mzigo wa kutosha, kipindi hicho kitaendelea mpaka kufika msimu wa joto na hapo samaki wataanza kupanda juu.
“Hali hii inasababisha vyombo kushindwa kuingia baharini, mfano jana kiliingia kimoja tu ambacho kilitoka na samaki ndoo moja ambayo kawaida inatakiwa kuuzwa Sh100,000 ila iliuzwa na Sh220,000 kwa sababu wateja wengi walikuwa wakihitaji mzigo,” amesema Wazio.
Msimamizi wa Soko la Samaki la Mwalo wa Deep Sea kutoka ofisi ya Ofisa Uvuvi jiji la Tanga, Hamisi Kitogo amesema hali hiyo ina athari hata kwa upande wao kwani inasababisha hata kushuka kwa mapato.
Amesema tegemeo lao ni kuingia baharini boti za uvuvi kuanzia kumi na kuendelea, hali hiyo inasaidia hadi kuongezeka kwa mapato ila hivi sasa kwa siku inaweza kuingia boti moja tu.
Takwimu zinaonyesha kuwa Mkoa wa Tanga una jumla ya wavuvi 13,336 na vyombo vya uvuvi vilivyosajiliwa 1,922 katika wilaya za Tanga, Pangani, Mkinga na Muheza.