Njombe. Serikali imetakiwa kuunga mkono juhudi za wawekezaji ambao wameonyesha jitihada katika shughuli za maendeleo kwa kuboresha miundo mbinu muhimu inayoelekea katika maeneo ya uzalishaji ili kuwatia moyo na kuona kuwa wapo pamoja nao na wanaweza kuwekeza nchini.
Hayo yamesemwa leo Julai 9,2025 na mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka wakati akizindua barabara yenye urefu wa kilomita 8 inayoelekea eneo la uzalishaji wa parachichi pamoja na uzinduzi wa shamba lenye ekari 600 linalomilikiwa na Kostiv Tanzania Group lililopo kijiji cha Nundu huko wilayani Njombe.
Amesema muwekezaji ametoka nchi ya Marekani na kuacha kuwekeza kilimo cha parachichi katika nchi nyingine barani Afrika lakini ameamua kuwekeza Tanzania kwasababu ya amani na utulivu uliopo nchini.
Amesema Sh.108 milioni zimetumiwa na mwekezaji kwa ajili ya kutengeneza barabara inayoelekea kwenye mashamba ya parachichi kwasababu ya nia ya dhati ya kuwekeza mkoani Njombe hivyo jitihada hizo zinapaswa kuungwa mkono na serikali.
Amesema kwa kutambua mchango wa mwekezaji katika ujenzi wa barabara hiyo wakala wa barabara vijijini (TARURA) mkoani Njombe wameamua kuipa jina la Petro Kostiv road ikiwa ni kuonyesha thamani yake kwa wananchi wa mkoa huo.
Amesema kutokana na juhudi zilizoonyeshwa watendaji wa serikali wanatakiwa kuhakikisha wanasogeza huduma muhimu za miundo mbinu ya umeme , maji na barabara katika maeneo ya uzalishaji ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.

Amesema ni jambo la kushangaza kuona mkoa unaotegemea uchumi wa kilimo kwa kiasi kikubwa una barabara mbovu ,hauna maji na umeme maeneo ya uzalishaji jambo ambalo taasisi husika zimetakiwa kutafuta ufumbuzi ili wakulima wafikie masoko.
Amesema matamanio ya mheshimwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona miradi ya maji, barabara na umeme inakwenda katika maeneo ya uzalishaji na ndiyo sababu bajeti ya kilimo imezungumzia uchimbaji wa visima kwa ajili ya kuwezesha kilimo cha umwagiliaji.
“Tunapopanga hizi bajeti zetu za Tarura lazima akili yetu sisi Njombe tuanze kupeleka barabara huko ambapo pesa zinatoka kwasababu mapato ya halmashauri yanatokana na mazao ya misitu,parachichi na viazi” amesema Mtaka.
Mwekezaji kutoka kampuni ya Kostiv Tanzania Group Limited Petro Kostiv ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika kilimo ambayo yamemfanya kutoa fedha na kutengeneza barabara ili kufika eneo la uwekezaji linalogharimu zaidi ya Sh. 3 bilioni.
“Nafurahi kuwepo Tanzania na najisikia Njombe kama nyumbani kwangu na nitashirikiana na wananchi kama ambavyo nimefanya katika kuboresha miundombinu ya barabara” amesema Kostiv.
Meneja kituo cha uwekezaji (TIC) kanda ya Nyasa Deusdedit Hokororo amesema uwepo wa mwekezaji huyo ni fursa kwa wananchi wa mkoa wa Njombe kwakuwa ajira nyingi zitazalishwa kupitia shamba hilo la parachichi.
“Mwekezaji huyu atalima na kuchakata zao la parachichi hivyo ni fursa kwetu sisi wananjombe na jamii inayozunguka shamba hilo na mategemeo yetu uchumi utakuwa na uwekezaji huu kuleta tija” amesema Hokororo.
Mkurugenzi kampuni ya umwagiliaji ya Holly Green Agric Group Limited mhandisi Octavian Lasway ambaye ndiye amefanya usanifu na sasa kutekeleza mradi huo wa kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji katika shamba hilo amewataka wananchi mkoani Njombe kutumia fursa ya kilimo ili kukuza uchumi wao kwani ardhi iliyopo ina rutuba na inafaa kwa kilimo cha parachichi.
“Njombe ni eneo zuri kwa ajili ya kulima na kuuza parachichi na mazao mengine na tutakuwepo hapa na baada ya shamba hili kukamilika miundombinu tutawakaribisha kuja kujifunza namna mtakavyofanya kilimo cha kisasa” amesema Lasway.
Awali mkuu wa wilaya ya Njombe Juma Sweda amewataka wananchi wilayani humo kulinda miundombinu iliyowekwa na wawekezaji na kuacha tabia ya kuiba vitu vilivyokuwrpo katika maeneo hayo.
“Acha kwenda kuiba na kubomoa sehemu za watu ambazo wamejenga njoo shambani utapata mali kwahiyo tupambane udongo ni mali na ni pesa tukifanya kazi kwa nguvu na bidii tutafanikiwa” amesema Sweda.

Baadhi ya wakulima kutoka vijiji vya Nundu na Limage akiwemo Grace Mdendemi amemshukuru muwekezaji kwa kwa mradi huo wa barabara kwani umerahisisha usafitishaji wa mazao kutoka shambani kuelekea sokoni.
“Baada ya kutengenezwa barabara hii wakulima sasa wanapita na mazao yao bila ya shida tunashukuru sana kwa kuwepo muwekezaji huyu” amesema Mdendemi.