Siku 22 za Camara Simba SC

ILIKUWA miezi, wiki na sasa ni siku tu, kwani mabosi wa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Bara wapo bize kwelikweli wakisuka mitambo kwa ajili ya msimu ujao, huku maandalizi mengine kama kambi yakiwa katika hatua za mwisho mwisho kwenda kujifua.

Lakini, wakati hilo likiwa bado katika mazingira ya sintofahamu, kuna mambo mengine yanaendelea chinichini, huku usajili ukiwa umeshaanza na timu zingine zikivizia wachezaji watakaoachwa na wapinzani wao kwenye mashindano hayo ili ziweze kuwatumia kwa ajili ya kujitetea msimu ujao.

Wakati ukitafakari hayo, elewa kwamba kuanzia Julai 9, 2025 hadi Julai 31, 2025 ni kipindi cha takribani siku 22 ambapo hapo kati ndiyo kuna hatma ya kipa Moussa Camara kuwepo ndani ya Simba.

Ipo hivi; mabosi wa kikosi hicho bado wako kwenye hesabu kali za kukisuka zaidi baada ya msimu uliomalizika kumaliza bila ya taji lolote huku mashabiki wakiona wamefeli.

Wakati presha ikiwa kubwa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo waliomisi kuona mataji yakibebwa na chama lao, mabosi wapo bize kusaka wachezaji wa kuimarisha kikosi.

Kati ya sehemu ambazo Simba inazipigia hesabu kuboresha ni eneo la golini ambapo Camara alikuwa kipa namba moja msimu uliomalizika akiwapiga benchi Ally Salim, Hussein Abel na Aishi Manula aliyemaliza mkataba Juni 30 na taarifa zikidai ametimkia Azam.

Camara alitambulishwa Simba Agosti Mosi 2024 akiwa miongoni mwa machaguo ya kocha Fadlu Davids, huku Wekundu wakimpa mkataba wa mwaka mmoja wenye makubaliano ya kuongeza mwingine. Mkataba wake wa mwaka mmoja, unafikia tamati Julai 31, mwaka huu.

Camara mpaka kufikia Julai 31 mkataba wake wa mwaka mmoja utakuwa umefikia ukingoni, hivyo Simba ina kazi ya kufanya uamuzi kabla ya huo muda kama haimtaki msimu ujao. Taarifa za ndani kutoka Simba zililiambia Mwanaspoti kuwa: “Kipa huyo bado hajapewa mkono wa kwaheri na mabosi wa klabu, hivyo mpaka kufikia Julai 31 mwaka huu kama atakuwepo basi maana yake bado ni mchezaji wa Simba.

“Lakini hadi kufikia tarehe hiyo mambo yakiwa kimya kisha baadaye ndiyo wakaachana naye, itawalazimu wamlipe kwa kigezo cha kumvunjia mkataba, hivyo kama ni kumuondoka ni ndani ya siku hizi chache zilizobaki kabla ya mwezi huu kumalizika.”

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, mkataba wa Camara na Simba ambao alisaini kwa mwaka mmoja kukiwa na kipengele cha kuongeza, unambeba mchezaji kama hakutakuwa kauli ya uongozi juu ya mustakabali wake.

Ipo hivi; mkataba huo unaomalizika Julai 31, ikifika Agosti Mosi bila ya Simba kusema chochote juu ya Camara, maana yake kipa huyo moja kwa moja ataendelea kusalia kikosini hapo kumalizia mwaka mwingine wa mwisho katika makubaliano yao ya awali.

Licha ya kuonyesha kiwango bora na kumaliza Ligi Kuu Bara akiwa kinara wa clean sheet akifikisha 19, lakini kuna makosa aliyoyafanya kipa huyo katika baadhi ya mechi yaliyoonekana kuigharimu Simba na kujikuta ikiendelea kuukosa ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa nne mfululizo ambapo safari hii imeachwa na bingwa, Yanga kwa tofauti ya pointi nne.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa: “Makosa ya Camara hata mabosi wameyaona na ndio yaliyofanya benchi la ufundi kutafutiwa kipa bora zaidi kwa ajili ya msimu ujao.

“Lakini kama atakosekana kipa mwingine ambaye atakuwa bora zaidi, basi hakutakuwa na namna Camara ataendelea kuitumikia Simba kwa msimu ujao lakini lazima abadilike.”

Camara ambaye alicheza mechi zote za kimataifa msimu ulioisha ambapo Simba ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco, amekuwa akitajwa kufanya makosa yaliyoigharimu hasa mechi za Ligi Kuu Bara.

Katika ligi, kipa huyo aliyecheza mechi 28 kwa dakika 2,520 kati ya mechi 30, ndiye ameibuka kinara wa clean sheet akimaliza nazo 19 huku akiruhusu mabao 13.

Miongoni mwa makosa aliyofanya yaliyoigharimu Simba kupoteza ni mechi mbili za ligi dhidi ya Yanga ambapo Oktoba 19, 2024, mpira wa faulo uliopigwa na Clatous Chama dakika ya 86 ukionekana kwenda nje aliufuata na kujikuta anaurudisha ndani Maxi Nzengeli akaupiga kwa haraka Kelvin Kijili akajifunga bao pekee lililoipa Yanga ushindi wa 1-0. Pia Juni 25, 2025 alitoka golini na kwenda kumfanyia faulo Pacome Zouzoua kwenye eneo la hatari, Simba ikaruhusu bao la kwanza na kupoteza kwa mabao 2-0.

Kabla ya hapo sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union Oktoba 4, 2024 alifanya makosa mawili yaliyozaa mabao wakati Simba ikiwa mbele kwa 2-0, mwisho ikaisha sare ya 2-2.

Related Posts