Unguja. Watu sita wamefikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, wakishtakiwa kwa tuhuma za kumuua Sheikh Jabir Haidar Jabir.
Akiwasomea mashitaka yao leo Julai 9, 2025 mbele ya Jaji Khadija Shamte Mzee, Wakili kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Anuwar Saaduni amedai washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la mauaji ya kukusudia ya Sheikh Jabir Haidar.
Amewataja washtakiwa hao ni Salum Manja Ame (23), Idrisa Kijaz Kasim (41), Ali Mohamed Ali (30), Ali Machano Haji (52), Zahor Khamis Ali (54) na Mohamed Hassan Jongo (38) wote ni wakazi wa Zanzibar.
Amesema washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kumuua Sheikh Jabir kinyume na kifungu namba 179 na 180 vya sheria ya adhabu namba sita ya mwaka 2018.
Washatakiwa kwa pamoja wamekana kosa lao na Jaji Khadija ameamuru wapelekwe rumande na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 16 mwaka huu itakapotajwa tena.
Mwili wa Sheikh Jabir uliokotwa kando mwa barabara usiku wa kuamkia Mei 28, 2025 eneo la Kizimbani, Bumbwisudi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika taarifa ya polisi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu kwa vyombo vya habari Mei 28, alisema mazingira ulipokutwa mwili huo hayakuonyesha dalili zozote za vurugu, hivyo huenda alipata madhara sehemu nyingine akabebwa na kupelekwa pale.
Alisema kabla ya tukio hilo, jana yake Mei 27 saa 12:00 jioni sheikh huyo akiwa nyumbani kwake Fuoni alitembelewa na kijana ambaye alionyesha kufahamiana naye na walikaa kwa muda sebuleni wakizungumza wakati kijana wake wa kazi alikuwa ndani.
“Sheikh Jabir alizungumza na kijana huyo kama nusu saa wakatokea watu wengine watano ambao walijiunga pamoja na ilipofika saa 2:30 usiku waliondoka naye, kabla ya kuondoka hausiboi alimuuliza bosi wake (Sheikh Jabir) anapokwenda, akamjibu atamjuza baadaye, hivyo haikufahamika anakwenda wapi hadi mwili wake ulipookotwa,” alisema Kamanda Mchomvu.