Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus, Constantinos Kombos amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu akilenga kufanya mazungumzo muhimu na serikali ya Tanzania kuhusu demokrasia, haki za binadamu, na uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba.
Kombos anafanya ziara hiyo kwa niaba ya Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya wa Masuala ya Kigeni na Sera ya Usalama na Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya, Kaja Kallas.
Ziara hiyo imekuja kukiwa na azimio lililopitishwa na Wabunge wa Bunge la Ulaya (MEPs) Mei mwaka huu, wakilaani mashtaka ya uhaini dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Tundu Lissu ambaye ndiye kiongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Katika hotuba yake ya Juni 18, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Uswisi, Balozi Abdallah Possi alihutubia Baraza la Haki za Binadamu, akikanusha taarifa iliyowasilishwa na wataalamu wa UN kuhusu matukio ya utekaji na watu kutoweka nchini. Alisema Tanzania inaheshimu kikamilifu wajibu wake unaotokana na Katiba na mikataba ya kikanda na kimataifa ya haki za binadamu na kuwa wananchi wana uhuru wa kujieleza na kutoa maoni hata kama ni kinyume cha msimamo wa Serikali.

Alisema kuwa, kama mzungumzaji alivyoonekana kukiri; Tanzania ina demokrasia iliyokomaa, ikiwa imeshafanya chaguzi saba huru, za haki na za amani chini ya mfumo wa vyama vingi. “Tanzania haijawahi kukosa kufanya uchaguzi kama inavyotakiwa na Katiba na ikiwa mwenendo wa kihistoria utaendelea, hali hiyo inatarajiwa pia wakati huu,” alisema.Dk Possi alisema uwezo wa Tanzania kudumisha amani katika jamii yenye tofauti kubwa za makabila, imani na itikadi za kisiasa unatokana na uzingatiaji wake wa utawala wa sheria.
Alisema uzingatiaji wa utawala wa sheria unahakikisha wananchi wote wanatendewa haki kwa usawa, wakiwamo waliotajwa na mwakilishi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, ambao ameeleza kwa bahati mbaya walishindwa kutangaza kwa uwazi madhumuni yao halisi ya kuingia Tanzania -ambayo ni hitaji la kawaida katika sheria za uhamiaji za mataifa mengi.
Balozi Possi alisema ingawa madai hayo bado hayajathibitishwa kwa uchunguzi huru, Tanzania inazichukua kwa uzito tuhuma zilizotolewa za mateso, ukatili wa kijinsia na ukiukwaji wa maadili. Alisema ndiyo sababu Tanzania inafanya uchunguzi na iwapo ukweli utabainika, waliohusika watawajibishwa.
Kombos ambaye ameambatana na ujumbe wa watu sita kutoka katika Wizara ya Mambo ya nje ya Cyprus, mabalozi na wawakilishi kutoka Idara Siasa na Afrika anatarajiwa kuwepo nchini hadi Julai 10.
Akiwa nchini, Kombos atakutana viongozi wa kadhaa na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Wawili hawa watazungumzia maendeleo ya kisiasa nchini Tanzania, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, na hali ya usalama katika kanda, hususan eneo la Maziwa Makuu.
Pia, atashiriki mkutano wa pande mbili kati ya Tanzania na Cyprus na atatia saini hati za makubaliano ya ushirikiano kuhusu mashauriano ya kisiasa na ushirikiano katika masuala ya mabaharia.
Kombos pia atashiriki katika majadiliano ya meza ya pamoja kati ya Jumuiya ya Biashara ya Ulaya na Chemba ya Biashara Tanzania.
Wakati wa ziara yake nchini Tanzania, ofisa huyo wa juu wa EU atakutana pia na wanachama wa asasi za kiraia, viongozi wa biashara, na wadau wengine muhimu.
Aprili mwaka huu, Waziri Kombo alifanya ziara katika makao makuu ya EU jijini Brussels, ambako alikutana Kallas, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa Koen Doens, pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), Thomas Östros, ili kuendeleza mazungumzo ya kisiasa, uwekezaji, na maendeleo endelevu.
Mei mwaka huu, Bunge la Ulaya lilipitisha azimio kulaani kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini dhidi ya Tundu Lissu.
Wabunge hao walieleza wasiwasi wao kuhusu mashtaka yenye taswira ya kisiasa ambayo yanaweza kumpelekea Tundu Lissu kuhukumiwa adhabu ya kifo.
Bunge hilo liliitaka Serikali ya Tanzania kurudisha ushiriki kamili wa Chadema katika uchaguzi wa Oktoba 2025, kuanzisha mazungumzo na vyama vyote vya siasa kuhusu mageuzi ya uchaguzi, kuheshimu haki za vyama vya siasa, na kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.
Azimio hilo pia lililaani ongezeko la vitendo vya ukandamizaji nchini Tanzania, ikiwemo ukamatwaji holela na unyanyasaji wa wanasiasa wa upinzani na watetezi wa haki za binadamu.
Wabunge wa Ulaya walitaka Tanzania kufuta adhabu ya kifo na kubadili hukumu zote za aina hiyo, na kutaka ushirikiano wa maendeleo kati ya EU na Tanzania, hasa chini ya mpango wa Global Gateway, kuhakikisha unalingana na kukuza haki za binadamu, uhuru wa kujieleza, na viwango vya haki katika mwenendo wa kesi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazonufaika zaidi na misaada ya kigeni kutoka Umoja wa Ulaya katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kupitia mkakati wa Global Gateway wa EU (2021–2027), Ulaya imejitolea kutoa euro milioni 990 ambazo ni zaidi ya Sh3 trilioni za Kitanzania kusaidia sekta ya nishati ya Tanzania, pamoja na maeneo mengine.