ACT Wazalendo yailima barua Polisi kuhusu taarifa za watiania, yajibu

Dar/Tunduru. Wakati Chama cha ACT-Wazalendo kikidai kimemuandikia barua Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura kumtaka kusimamisha amri aliyoitoa kwenda kwa makamanda wa Polisi wa Wilaya ya kukusanya taarifa za wagombea wao wa ubunge na udiwani, jeshi hilo limejibu likisema hakuna barua iliyomfikia IGP.

Jeshi hilo limesema, iwapo barua hiyo itamfikia mku huyo wa Jeshi la Polisi, itafanyiwa kazi haraka ili kupata ukweli wake na mawasiliano hayo yametoka wapi na yametolewa na nani.

ACT Wazalendo, kimelalamikia hatua hiyo ya Jeshi la Polisi ya kuwasiliana na viongozi wake kuomba taarifa hizo, kwanza ni ghiriba na kinyume na sheria na kanuni za uchaguzi huo, hivyo kinachofanywa ni mwanzo na mkakati wa kuvuruga mchakato wa uchaguzi kwa kuanza kutengeneza mazingira ya kuengua majina ya wagombea wao.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ameeleza hayo leo Alhamisi Julai 10, 2025 akizungumza na wanahabari akisema chama hicho kimechukizwa na kitendo hicho na ndio maana kimemuandikia IGP Wambura kuhusu mchakato huo.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime, amesema barua hiyo bado haijamfikia IGP Wambura.

“Endapo itamfikia barua hiyo maudhui yake yatafanyiwa kazi kwa haraka ili kupata ukweli wake na mawasiliano hayo yametoka wapi na yametolewa na nani,” amesema Misime kupitia taarifa kwa umma.

Lakini, katika maelezo yake, Shaibu amedai ” “tunaamini makamanda amewatuma na kama hajawatuma awape amri waache mara moja huo mchezo,” amesema Shaibu.

Kwa mujibu wa Shaibu, baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na kadhia hiyo ni Kilwa (Lindi), Kigamboni na Kinondoni (Dar es Salaam), Magu (Mwanza), na Tarime (Mara).

Ameeleza kuwa mawasiliano hayo kutoka kwa Jeshi la Polisi ni kinyume na sheria, kwa kuwa si sahihi kuwahoji wagombea juu ya taarifa zao wakati huu ambapo majina yao yanatakiwa kuwasilishwa rasmi kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na siyo kwa Jeshi la Polisi.

” OCD Tarime anaenda hadi kuwagongea viongozi wetu wa wilaya milango wawapatie majina ya watia nia na wagombea wetu wa udiwani na wabunge wao wanataka ya nini? kama sio njama na mipango ya kutaka kuengua wagombea wetu kwenye uchaguzi,” amedai Shaibu.

Katika hatua nyingine, Shaibu amesema ACT Wazalendo kimemuandikia barua Msajili wa Vyama Vya siasa kuhusu madai hayo.

“Ni muda mrefu Msajili amejikita kuangalia namna vyama vinavyotekeleza sheria, lakini tuna toa rai kwake wajibu wa Msajili usiishe kuangalia utekelezaji wa sheria iko wapi haki ya vyama vya siasa. Je, Msajili hana wajibu wa kuvitetea na kuvilinda vyama katika haki zake? amehoji.

Mwananchi limezungumza Msajili Msaidizi wa Vyama Vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema anafuatilia kujua barua ya madai hayo kama kweli imetumwa katika Ofisi hiyo na waanze kuyafanyia kazi.

“Nimekuja ofisini nilikuwa safarini ngoja nifuatilie kujua barua yao kama imefika niweze kuisoma. Ni kweli tuna vilea vyama kisheria tutapima kilicholetwa,” amesema Sisty Nyahoza.

Vilevile, Shaibu amesema kuwa chama hicho kimeiandikia barua INEC, wakiitaka itoe tamko rasmi kulikemea Jeshi la Polisi kuacha kuingilia mchakato wa ndani wa uchaguzi.

Amesisitiza kuwa msimamo wa ACT Wazalendo ni kwamba Jeshi la Polisi liondokane na tabia ya kuwasiliana na viongozi wa majimbo kuhitaji taarifa za wagombea, kwa kuwa hatua hiyo ni kinyume na sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uchaguzi nchini.

“Chama chetu kimeamua kushiriki uchaguzi huu na hujuma zozote zitawekwa bayana kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki na wa kuaminika,” amesema.

Akiwahutubia wananchi wa Tunduru (Ruvuma) katika mwendelezo wa ziara ya operesheni Majimaji Oktoba Linda kura, kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema polisi hawahusiki na mchakato wa uchaguzi bali kulinda raia na mali zake.

“Polisi wanapaswa kutulinda sisi si kuingilia mchakato wa uchaguzi, sasa hao maofisa wanaowapigia simu viongozi wetu kujua wagombea wa udiwani na ubunge waache mara moja. Hivi wana mamlaka gani ya kufanya hivyo? amehoji Zitto.

“Polisi hawana mamlaka yoyote ya kupewa taarifa za viongozi wetu, namwambia IGP polisi hawana nafasi yeyote kwenye mchakato huu wala DC (Mkuu wa Wilaya). Mwenye haki ni Mkurugenzi wa INEC,” amesema Zitto.

Zitto amesema endapo polisi wanahitaji mawasiliano kuhusu wagombea wa ACT Wazalendo wawasiliane na Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima.

Amesema ACT Wazalendo ni chama kinachopenda amani na utulivu, ndio maana ni nadra kutukana watu hivyo wamelisihi Jeshi la Polisi kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kiongozi huyo mstaafu, alieleza hayo mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja wa Baraza la Eid katika jimbo la Tunduru Kaskazini ambalo Shaibu ametia nia kuwania ubunge akiwaomba wananchi wa wilaya hiyo kumuunga mkono.

Mkutano huo wa hadhara ni sehemu ya ziara ya Zitto aliyeambatana na viongozi na wajumbe wa kamati kuu ya chama katika operesheni Majimaji Linda Kura yenye lengo la kuwaamsha Watanzania kujitokeza kupiga kura na kuzilinda.

Wakati huo huo, akiwa wilayani Same mkoani Kilimanjaro, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo, Abdul Nondo aliyesema umefika wakati thamani ya wanyama hao inawazidi binadamu.

Kauli yake hiyo, inatokana na kile alichofafanua, katika eneo hilo tembo anapoharibu makazi ya binadamu na kuuawa, raia ama anatozwa mabilioni au kufungwa jela.

Lakini, unapofanywa uharibifu na wanyama hao, amesema raia ama alipwe fidia kiduchu au asilipwe kabisa, licha ya kuathiriwa mazao.

“Umehangaika kulima shamba lako, umenunua mbolea, umegharamika, tembo akila zao lako fidia unayopewa ni Sh100,000 kwa ekari moja,” amesema.

Ameeleza kulipaswa kuwa na mizania sawa ya ulipwaji wa fidia kuendana na kiwango cha uharibifu unaofanywa

Akizungumza katika mkutano huo, mtia nia ya ubunge kupitia chama hicho Same Mashariki, Naghenjwa Kaboyoka amesema hatua yake ya kuchukua fomu ndio utakaokuwa mwisho wa wakazi wa eneo hilo kushangaa barabara.

Related Posts