Tunduru. Kuvuna tembo na kupitia upya mipaka ya hifadhi ni miongoni mwa mambo yatakayotekelezwa na Chama cha ACT –Wazalendo, ili kupunguza changamoto ya uharibifu wa mazao na madhara kwa binadamu inayosababishwa na wanyama hao.
Masuala hayo yatafanyika endapo ACT- Wazalendo itafanikiwa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ambapo chama hicho kimewaomba Watanzania kuwaunga mkono katika mchakato huo.
Mambo hayo yameelezwa jana Jumatano Julai 9, 2025 na kiongozi mstaafu wa ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini mkoani Ruvuma, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Namasakata wilayani Tunduru.
Mkutano huo wa hadhara ni sehemu ya ziara ya Zitto aliyeambatana na viongozi na wajumbe wa kamati kuu ya chama katika operesheni Majimaji Linda Kura, yenye lengo la kuwaamsha Watanzania kujitokeza kupiga kura na kuzilinda.

Viongozi wa ACT Wazalendo wakiwahutubia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini mkoani Ruvuma katika mwendelezo ya ziara ya operesheni majimaji Oktoba Linda Kura
Kabla ya kueleza hayo, Zitto aliwaambia wananchi wa Tunduru Kusini kuwa jana alikuwa Namtumbo ambapo alipokea kilio cha tembo kutoka kwa wananchi wa wilaya hiyo.
“Nilikuwa nasoma gazeti la Mwananchi la Desemba 12,2024 na mwandishi anaitwa Kalunde Jamal aliyeandika makala kuhusu namna ambavyo tembo wanavyoharibu mazao na kuleta madhara kwa wananchi katika mikoa ya Kilimanjaro na Singida,” amesema Zitto.
Ripoti maalumu iliyofanywa na Mwananchi mwaka 2024 ilibainia athari kubwa zinazotokana na wanyama hao, katika mikoa ya Singida na Kilimanjaro. Pia ilibaini tembo si kuharibu mazao pekee, bali pia wanasababisha vifo na majeraha kwa wakazi wa maeneo hayo.
Katika ripoti hiyo maalumu iliyofanyika kwenye mikoa hiyo ilibaini madhila yanayowakumba wakazi wa maeneo ya Same, mkoani Kilimanjaro kutokana na tembo kuwa tatizo kubwa, wakifanya vitendo visivyotarajiwa na binadamu.
Wanyama hao sasa wanazurura mitaani, wakila vyakula, kunywa maziwa, matikiti, pumba za mahindi, kuharibu mashamba na hata kula katani.
Ripoti maalumu ya Mwananchi imebaini athari kubwa zinazotokana na wanyama hao katika mikoa ya Kilimanjaro na Singida. Tembo si tu wanaharibu mazao, bali pia wanasababisha vifo na majeraha kwa wakazi wa maeneo hayo. Fisi pia wamekuwa tishio, wakijeruhi wananchi.
Miongoni mwa waliokumbwa na shambulio la fisi ni Emmanuel Jackson, mkazi wa Doroto, Wilaya ya Manyoni, Julai 14, akiwa anakwenda kuchota maji bwawani.
Hamisi Babasungu, aliyeishi kijiji cha Doroto tangu mwaka 1984, alisema amekuwa akipata hasara kubwa kutokana na tembo kula mazao yake, akieleza kuwa hali hiyo imeongezeka katika miaka mitano ya karibuni.
“Ningepata Sh2.2 milioni kutoka kwenye shamba langu la ekari saba, lakini yote yanaishia mdomoni mwa tembo. Tembo hawa wamekuwa sugu. Ukimpigia tochi, anakupa mgongo na kuendelea na shughuli zake,” anasema Hamisi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kandoto, Theopista Seleman, alisema kitongoji hicho kipo umbali wa kilomita 25-30 kutoka Hifadhi ya Mkomazi na kinakumbwa na uharibifu mkubwa, hasa na tembo. “Malalamiko yangu ni kwamba malipo ni kidogo mno, mtu akiharibiwa kuanzia nusu eka halipwi hadi iwe eka moja.”
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisima, Gabriel Mzava, alisema malipo ya wanyama wanaoharibu mazao ni ya chini, inapaswa kutungiwa mipango ya miradi inayowanufaisha wananchi, kama matumizi ya mizinga ya nyuki kufukuza tembo.
“Hiyo sehemu wanayopitia tembo ikizibwa hawatafika kwa wananchi,” anashauri Mzava.
Samwel Mbugu, alisema juhudi za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) hazitoshi kutokana na upungufu wa magari na rasilimali. “Walikuja nyumbani kwangu, walikula kila kitu, walirudi Mbugu, akionyesha hali ngumu wanayoishi.
Rajabu Mgonja kutoka Kijiji cha Masandare alisema tembo wameharibu mabomba ya maji na mazao yao.
“Tembo wanang’oa mabomba ya maji kila kukicha, wanashirikiana kufukia mashimo tuliyochimba,” anasema Mgonja.
Athumani Juma, mkazi wa Masandare, anasema: “Hatukuwa na shida na wanyama, lakini sasa hali ni mbaya. Miti inang’olewa na mazao yanaharibiwa.”
Kutokana na hilo, Zitto amesema ACT- Wazalendo ikishinda uchaguzi mkuu itaweka utaratibu wa kuwavuna tembo ili kuwapunguza, akisema njia hiyo ni sayansi inayoelekeza hivyo kila baada ya muda ili kuwapunguza.
“Wakipungua, watapunguza uharibifu wa mazao na madhara kwa binadamu. Jambo jingine tutakalolifanya lazima tupitie upya mipaka ili kuwapa wananchi maeneo makubwa zaidi ya kufanya shughuli zao za kiuchumi na kuweka hifadhi mbali.
“Tutahakikisha kunakuwa na uvunaji wa tembo, sasa hivi kila maeneo tembo, tembo…lakini kubwa kuliko zote ni kuiondoa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba,” amesema Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini.
Awali, Katibu wa ACT- Wazalendo mkoa wa kichama Selous, Mtutura Abdallah ambaye ni mtia nia ya ubunge wa Jimbo la Tunduru Kusini amesema kumekuwa na changamoto ya tembo katika Wilaya ya Tunduru na kusababisha uharibifu wa mazao.
Mbali na hilo, Mtutura aliyewahi kuwa mbunge Tundura kwa tiketi ya CCM, amewaomba wananchi wa wilaya hiyo kukichagua chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba ili wakakatue changamoto za uharibifu wa mazao ya wananchi.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT- Wazalendo, Halima Nabalang’anya amesema wananchi wa Tunduru wamekuwa washiriki wazuri katika chaguzi mbalimbali lakini changamoto inakuwa katika umaliziaji.

Viongozi wa ACT Wazalendo wakiwahutubia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini mkoani Ruvuma katika mwendelezo ya ziara ya operesheni majimaji Oktoba Linda Kura
“Tatizo ni umaliziaji tu, lakini safari hii, ACT- Wazalendo tumejipanga ipasavyo na tutahakikisha anayeshinda anatangazwa,” amesema Nabalang’anya ambaye ni waziri kivuli wa uchukuzi katika chama hicho.