Aga Khan kutoa huduma za saratani kwa mamilioni Tanzania na Kenya

Dodoma. Takriban watu milioni 7.4 wanatarajiwa kufikiwa kupitia mpango wa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani katika nchi za Tanzania na Kenya, kupitia kampeni inayoongozwa na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN).

Takwimu hizo zimetolewa leo, Alhamisi, Julai 10, 2025 na Mratibu wa Mradi Mtambuka wa East Africa Comprehensive Cancer Project (EA-CCP), Dk Sara Maongezi, wakati wa utambulisho wa mpango huo utakaofanyika kwa kipindi cha miaka minne kwa gharama ya euro milioni 10.2.

Dk Maongezi amesema mradi huo unahusika na uchunguzi na huduma za awali kwa wagonjwa wa saratani, ambapo unalenga mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro na Zanzibar; wakati Kenya watafanya kazi hiyo kwenye maeneo ya Mombasa, Kisumu, Kilifi na Homa Bay.

Hii ni awamu ya pili kwa mradi huo baada ya kuonesha awali kwamba walifanya vizuri, jambo lililowavutia wafadhili ambao ni Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) waliosaini kufanya kazi na Serikali.

“Sehemu kubwa ya mradi huu itahusisha afua za kijamii, zikiwemo kampeni ya kuelimisha kuhusu saratani na upimaji kwa wanawake 400,000 kwa saratani ya matiti na mlango wa kizazi katika nchi za Kenya na Tanzania,” amesema Dk Maongezi.

Amesema katika mradi huo wametenga kiasi cha fedha zitakazosaidia watu watakaobainika kuwa na tatizo, lakini hawatakuwa na fedha za kuanzia matibabu kwa wakati huo, na kwamba msamaha huo utapitia vitengo vya ustawi wa jamii kwenye mikoa husika.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, awali mradi ulijikita katika eneo dogo la Tanzania Bara pekee, lakini kwa sasa wanakwenda maeneo mengi ambako wanaamini idadi ya watu watakaofikiwa itaongezeka, ikiwemo watoa huduma katika hospitali na vituo vya afya.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Yahaya Hussein amesema Taasisi ya Aga Khan imesimama katika eneo ambalo linahitajika wakati wote ili jamii ya Kitanzania iwe salama.

Dk Yahaya, ambaye ni mtumishi kutoka Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), amesisitiza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kwa magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo saratani, ili kuwezesha kuanza huduma za matibabu mapema na hivyo kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi, mashirika na watu binafsi ambao wataonekana kufanya kazi zao kwa maslahi ya wananchi na Taifa, hususani katika eneo la afya.

“Hawa wenzetu Aga Khan siyo mara yao ya kwanza, tumekuwa tukifanya nao kazi kupitia miradi mbalimbali, hasa chuo kikuu chao. Leo niwaombe Watanzania kutoa ushirikiano kwa kila hali ili tuweze kufanikisha jambo hili,” amesema Dk Yahaya.

Naye Mratibu wa saratani katika via vya uzazi kutoka Wizara ya Afya, Dk Safina Yuma amesema tatizo la ugonjwa huo ni kubwa, lakini linatokana na elimu ndogo walionayo watu wengi kuhusu dalili, madhara, na gharama kubwa za matibabu ya ugonjwa huo hasa unapokuwa katika viwango vya juu.

Dk Yuma amesema matibabu ya saratani ni gharama kubwa zaidi, hivyo wananchi watafute namna ya kujua afya zao kwani itasaidia kuokoa gharama hizo pindi wanapogundulika katika dalili za awali.

Related Posts