Aina nyingi za samaki wa maji baridi Afrika hatarini kutoweka

Dar es Salaam. Takriban asilimia 26 ya aina za samaki wa maji baridi waliofanyiwa utafiti barani Afrika wako hatarini kutoweka, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF).

Ripoti hiyo, iliyobeba jina la Samaki Waliopuuzwa Afrika, imetolewa kuelekea Mkutano wa Kimataifa wa Ramsar (COP15) kuhusu uhifadhi wa maeneo oevu, unaotarajiwa kufanyika nchini Zimbabwe kuanzia Julai 23 hadi 31, 2025.

Kwa mujibu wa WWF, Afrika ina zaidi ya aina 3,200 za samaki wa maji baridi, huku 28 zikiwa zimegunduliwa mwaka huu pekee.

Hata hivyo, mazingira ya asili ya viumbe hao yanazidi kuharibiwa kwa kasi, hali inayotishia maisha yao na maisha ya binadamu wanaowategemea.

Tanzania na Uganda zimetajwa kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa samaki wa maji baridi duniani, kutokana na mchango mkubwa wa Ziwa Victoria, jambo linalozifanya nchi hizo kuwa na wajibu mkubwa wa kuchukua hatua za uhifadhi.

“Afrika ni kitovu cha aina nyingi za samaki wa maji baridi duniani, lakini pia ni eneo ambalo viumbe hao wako hatarini zaidi,” amesema Eric Oyare, Kiongozi wa WWF Afrika anayeshughulikia sekta ya maji baridi.

Ameongeza: “Kupotea kwa samaki hawa kunamaanisha kupotea kwa usalama wa chakula, ajira, urithi wa kitamaduni, na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

Ripoti hiyo imetoa mifano ya kuporomoka kwa idadi ya samaki katika maeneo mbalimbali, ikiwemo upungufu wa hadi asilimia 90 wa baadhi ya samaki katika bonde la Zambezi.

Aidha, aina ya  chambo walioko Ziwa Malawi, ambao ni miongoni mwa vyakula vya msingi nchini humo, wamepungua kwa asilimia 94.

WWF kwa kushirikiana na mashirika mengine kama The Nature Conservancy, imetayarisha mpango wa dharura wa kuokoa bioanuwai ya maji baridi, unaojumuisha hatua sita muhimu, ikiwamo kuruhusu mito kutiririka kwenye  njia zake za asili,  kuboresha ubora wa maji.

Hatua nyingine ni kulinda na kurejesha makazi ya samaki, kukomesha uvuvi na matumizi yasiyo endelevu, kudhibiti spishi vamizi na kurejesha mito kwa kuondoa vizuizi visivyohitajika.

Machaya Chomba, Meneja wa Uhifadhi wa Maji Baridi Afrika kutoka  shirika la The Nature Conservancy, amesema kutoweka kwa samaki wa maji baridi si suala la mazingira pekee, bali ni tishio kwa usalama wa chakula na uchumi wa jamii nyingi za Kiafrika.

WWF pia imepongeza juhudi za uhifadhi zinazoongozwa na jamii katika nchi kama Tanzania, Zambia na Namibia, ambako maeneo ya kuzaliana samaki yanalindwa na rasilimali kusimamiwa kwa pamoja.

Katika kuelekea mkutano wa Ramsar, WWF inazitaka nchi za Afrika, zikiwemo Tanzania, kuchukua hatua madhubuti kwa kutekeleza mpango wa dharura, pamoja na kushiriki katika mpango wa kimataifa wa Freshwater Challenge na kutekeleza lengo la 30×30 la kulinda maji baridi, chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Bioanuwai.

“Itakuwa ni makosa makubwa kwa samaki wa maji baridi kuachwa nyuma katika mijadala ya uhifadhi,” amesema Nancy Rapando, Mkuu wa Mpango wa Chakula Afrika kutoka WWF, akiongeza: “Samaki hawa ni sehemu ya maisha, utamaduni, na maendeleo ya bara hili. Tunapaswa kuchukua hatua sasa.”

Related Posts