Airtel Tanzania Yawapa Walimu Mafunzo ya Ujuzi wa Kidijitali Kupitia Mpango wa SmartWASOMI

Airtel Tanzania kupitia Airtel Africa Foundation, kwa kushirikiana na UNICEF na Wizara ya Elimu, imeandaa warsha ya mafunzo kwa walimu wa IT chini ya mpango wa Airtel SmartWASOMI, mradi wa kisasa wa ujifunzaji wa kidijitali unaolenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora kupitia teknolojia.

Warsha hiyo imewakutanisha walimu 60 kutoka shule za msingi na sekondari ambazo tayari zimeunganishwa na mpango wa Airtel SmartWASOMI. Mpango huu ulizinduliwa mwezi Mei 2024 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ikiwa ni ushirikiano kati ya Airtel Tanzania kupitia Airtel Africa Foundation, UNICEF na Serikali ya Tanzania. Zaidi ya shule 400 kote nchini zimeunganishwa na jukwaa hili, likiwa na huduma ya bure ya mtandao (zero-rated) kwa majukwaa ya mitaala ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Shule Direct, hivyo kuwapa maelfu ya wanafunzi na walimu fursa ya kupata rasilimali za ujifunzaji wa kidijitali bila gharama za data.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni wa Airtel Tanzania, Bi. Beatrice Singano, alisisitiza umuhimu wa walimu katika mafanikio ya mpango huo.

“Walimu ndio msingi wa mfumo wetu wa elimu, lengo la warsha hii ya mafunzo ni kuongeza uwezo wa walimu katika kufundisha kwa njia ya kidijitali na kuboresha matokeo ya elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari. Tunawekeza kikamilifu katika kuboresha elimu kupitia kuwaandaa walimu kutoa elimu bora inayojumuisha matumizi ya teknolojia,” alifafanua.

Bi. Singano aliongeza kuwa Airtel SmartWASOMI imeondoa kikwazo kikubwa cha ujifunzaji wa kidijitali kwa kutoa huduma ya kuingia kwenye maudhui ya elimu bila gharama ya data kupitia mtandao wa Airtel, hivyo kuwapa wanafunzi na walimu njia rahisi na ya uhakika ya kufikia vifaa vya kujifunzia vilivyokubaliwa na serikali.

“Katika mafunzo ya leo, walimu walipata uzoefu wa moja kwa moja wa kutumia zana za ujifunzaji wa kidijitali kupitia jukwaa la Airtel SmartWASOMI, ikiwa ni pamoja na kufikia maudhui ya mitaala, rasilimali shirikishi, na mbinu za kuingiza zana hizi kwenye ufundishaji wa kila siku darasani. Hii itasaidia walimu kurahisisha upangaji wa masomo, kuboresha ufundishaji kwa kutumia maudhui ya kidijitali, kutoa kazi shirikishi, na kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa ufanisi zaidi, hivyo kuongeza ushirikiano na ubora wa ufundishaji darasani,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Machapisho na Utafiti kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Bw. Kwangu Zabron Masalu, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dk. Aneth Komba, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amesisitiza sana matumizi ya teknolojia ya mawasiliano. Matokeo yake, masomo ya teknolojia sasa yanafundishwa kuanzia elimu ya awali hadi ngazi ya chuo kikuu.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa fursa hii inaleta mapinduzi katika mfumo wa elimu wa Tanzania, tukizingatia kuwa elimu yetu kwa sasa inalenga zaidi kuzalisha wahitimu wenye ujuzi na umahiri katika kila ngazi,” alisema Bw. Masalu.

Walimu walioshiriki warsha hiyo waliupokea mpango huo kwa furaha kubwa, kwa wengi, ilikuwa mara yao ya kwanza kushiriki kwenye jukwaa kubwa la kidijitali linalolenga shule za sekondari nchini Tanzania.

Bi. Neema Avumba, mwalimu kutoka Shule ya Msingi TEGETA A, jijini Dar es Salaam alisema: “Ningependa kutoa shukrani zangu kwa Airtel Tanzania, UNICEF na serikali kwa kuandaa mafunzo haya leo, kabla ya warsha hii, wengi wetu hatukujua uwezo wa zana za kidijitali, sasa najihisi nimewezeshwa kuleta mbinu mpya darasani, tayari naona jinsi zitakavyowavutia na kuwashirikisha wanafunzi kwa njia ambayo hatukuweza hapo awali.”

Kwa upande wake, Bw. Nassoro Shamsi, mwalimu kutoka Shule ya Msingi Mji Mwema, Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, aliongeza kwa kusema: “SmartWASOMI imefungua fursa mpya. Sasa tunapata maudhui ya mtaala yaliyowezeshwa na nyenzo za kufundishia bila gharama za data kwa kutumia mtandao wa Airtel. Nimefurahi sana kuanza kutumia ipasavyo jukwaa hili baada ya mafunzo haya.”

Mbali na mafunzo ya kiteknolojia, warsha hiyo pia iliwawezesha walimu kushirikiana, kuuliza maswali na kubadilishana uzoefu. Lengo si kuongeza ujuzi tu, bali pia kuunda mtandao wa mabalozi wa ujifunzaji wa kidijitali kote nchini.

Mpango wa Airtel Tanzania ni kufikia zaidi ya shule 1,000 ifikapo mwisho wa mwaka 2025, kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, ushirikiano madhubuti na jamii pamoja na msaada kutoka kwa wadau muhimu. Juhudi hizi zinaendana na ajenda ya kitaifa ya kukuza upatikanaji jumuishi wa elimu bora ya kidijitali na kuchangia malengo mapana ya kukabiliana na upungufu wa walimu wenye sifa, kuongeza uelewa wa kidijitali kwa wanafunzi, na kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa rasilimali za elimu katika mikoa yote.

Mkurugenzi wa Machapisho na Utafiti kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Bw. Kwangu Zabron Masalu (Katikati), akizungumza jijini Dar es Salaam jana, wakati wa warsha iliyoandaliwa kwa walimu wa IT, iliyoandaliwa na Airtel Tanzania kupitia Airtel Africa Foundation, kwa kushirikiana na UNICEF na Wizara ya Elimu, chini ya mpango wa Airtel SmartWASOMI, unaolenga kuboresha elimu ya kidigitali kwa kuwawezesha walimu na wanafunzi kupata maudhui ya kielimu kupitia maktaba mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania na Shule Direct bila gharama ya vifurushi vya data. Kushoto ni Bw. Audax Tibuhinda kutoka Unicef na kulia Bw. Jackson Mmbando, Meneja Mahusiano wa Airtel Tanzania. 

Ofisa Vifaa vya Intaneti wa Mradi wa SmartWASOMI, Bw. Harrison Isdory (kulia), akitoa mafunzo kuhusu matumizi ya baadhi ya vifaa hivyo katika wakati wa warsha iliyoandaliwa kwa walimu wa IT, iliyoandaliwa na Airtel Tanzania kupitia Airtel Africa Foundation, kwa kushirikiana na UNICEF na Wizara ya Elimu, chini ya mpango wa Airtel SmartWASOMI, unaolenga kuboresha elimu ya kidigitali kwa kuwawezesha walimu na wanafunzi kupata maudhui ya kielimu kupitia maktaba mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania na Shule Direct bila gharama ya vifurushi vya data. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana. 

Related Posts