Aishi Manula kachagua klabu sahihi

HAKUNA mahali bora kama nyumbani na ndiyo maana wahenga wakasema nyumbani ni nyumbani hata kama kichakani.

Inapendeza zaidi kuona mtoto anapoamua kurejea nyumbani baada ya kukaa nje kwa miaka kadhaa katika harakati za utafutaji wa riziki na changamoto mpya.

Kijiweni hapa tunaona imekuwa ni jambo bora kwa kipa Aishi Manula kurejea katika klabu ya Azam baada ya kukaa nje ya timu hiyo kwa miaka saba akiitumikia Simba ambayo alijiunga nayo mwaka 2018.

Haiitajiki kutumia nguvu kubwa kuaminisha watu Azam FC ni nyumbani kwa Manula na ndiyo maana kijiwe kimefurahi kuona akijiunga na hiyo timu baada kumaliza mkataba wake na Simba siku ambayo msimu wa ligi 2024/2025 ulifikia tamati.

Azam na Manula kila upande hauna baya kwa mwingine. Azam ndiyo ilimuibua Manula akiwa mtoto mdogo na kumpa nafasi ya kutosha ya kucheza hadi akafikia daraja alilonalo sasa la kuwa kipa bora mzawa katika miaka ya hivi karibuni.

Manula mwenyewe aliichezea kwa juhudi na bidii kubwa Azam kiasi ambacho akaweza kushinda mataji kadhaa akiwa na timu hiyo kama Ligi Kuu na Kombe la Kagame.

Iko wazi Manula amepitia kipindi kigumu akiwa na Simba katika misimu miwili ikiyopita ambapo alikuwa akikabiliwa na majeraha, pia alipoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha timu hiyo.

Uamuzi wake wa kwenda Azam utakuwa na manufaa makubwa kwake kwa vile ni timu ambayo itampa uhuru mkubwa na atacheza kwa utulivu kuliko angebaki Simba au angeenda katika timu nyingine.

Uhamisho huu ni furaha kubwa bila shaka kwa benchi la ufundi la Taifa Stars kwa vile sasa kipa huyo mzoefu atapata fursa ya kucheza idadi kubwa ya mechi na zitalinda kipaji chake.

Related Posts