Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Bodi ya Wadhamini wake waliosajiliwa, kimewasilisha maombi ya kumtaka Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi yake ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama, ajiondoe kwenye kesi hiyo.
Pia chama hicho kimefungua shauri la maombi kikiiomba Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, iondoe amri zake za zuio dhidi ya wadaiwa katika kesi hiyo, (Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu), kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama.
Juni 10, 2025, Mahakama hiyo ilitoa amri ya zuio dhidi ya wadaiwa kufanya shughuli za kisiasa na amri ya kuwazuia wao wadaiwa na watu wengine wanaofanya kazi kwa maelekezo au kwa niaba yao kutumia mali za chama hicho, mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo kufuatia shauri la maombi ya zuio hilo yaliyofunguliwa na wadai katika kesi hiyo, baada ya Mahakama kutupilia mbali mapingamizi ya wadaiwa dhidi ya kesi ya msingi na dhidi ya shauri la maombi ya zuio.
Uamuzi na amri hizo za Mahakama ndio uliowasukuma wadaiwa kuandika na kuwasilisha barua ya kumkataa jaji Mwanga kwa madai kuwa kwa mwenendo huo hawana imani naye kama atawatendea haki, pamoja na shauri hilo la maombi ya kuondoa amri hizo za mahakama.
Kutokana na kuwepo maombi hayo, kesi hiyo ya msingi ambayo ilikuwa imepangwa kusikilizwa leo madai ya msingi ya wadai imesimama kwa muda usiojulikana kusubiri mpaka maombi hayo yote yatakapotolewa uamuzi.
Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutokea Zanzibar.
Wakati kesi hiyo ilipoitwa leo Alhamisi Julai 10, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji, kiongozi wa jopo la mawakili wa wadaiwa, Mpale Mpoki ameieleza Mahakama kuwa wadaiwa hao (Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu) wameandika barua ya kumtaka Jaji huyo ajitoe katika kesi hiyo.
Wakili Mpoki amesema kuwa barua hiyo iliyoandikwa Juni 23, 2025 iliwasilishwa kwa Naibu Msajili Juni 24, 2025.
“Wanaomba na kumtaka Jaji Hamidu Mwanga ajitoe katika usikilizwaji wa shauri namba hilo, pia tulileta shauri la maombi ya kuondoa amri za Mahakama hii za Juni 10, 2025 katika shauri namba 8960/2025, ambalo limeshajiliwa,” amesema wakili Mpoki.
Wakili wa wadai, Shabani Marijani ameieleza Mahakama wamepata taarifa za kuwepo kwa barua hiyo ya wadaiwa kumkataa jaji leo Alhamisi asubuhi.
Hivyo amesema kwa kuwa suala la kumkataa jaji ni la kisheria, wanaomba ahirisho la muda wa kuipitia ili kuona kama kuna hoja huku akiiomba Mahakama iwape muda mfupi kwa kuwa shauri hilo linagusa masilahi ya umma.
Jaji Mwanga amekubaliana na hoja na maombi hayo na amepanga kusikiliza maombi ya wadaiwa kumtaka ajitoe katika kesi hiyo, Jumatatu Julai 14, 2025 saa 4:00 asubuhi, tarehe ambayo kesi ya msingi pia itatajwa.
Shauri la maombi ya kuondoa amri za Mahakama za zuio la wadaiwa kufanya shughuli za kisiasa na matumizi ya mali za umma nalo limetajwa leo.
Kuhusu shauri hilo, Wakili Mpoki amesema kwa kuwa kuna maombi yaliyowasilishwa na wateja wao (kumkataa jaji) ambayo yana athari za moja kwa moja kwa shauri hilo, ameiomba Mahakama usikilizwaji wake pia usubiri uamuzi wa maombi ya wadaiwa ya kumkataa jaji.
Hoja hiyo imeungwa mkono na mawakili wa upande wa wadai na Jaji Mwanga pia amekubaliana nayo.
“Kwa haya maombi kila kitu kitasimama kusubiri uamuzi wa maombi ya wadaiwa” amesema Jaji Mwanga na akaamuru kuwa maombi hayo pia yatatajwa Jumatatu, Julai 14, 2025.
Katika kesi hiyo ya madai ya mwaka 2025, wadai wanaiomba Mahakama hiyo itamke na kuamuru amri kuwa wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.
Wamechukua hatua hiyo na kuomba Mahakama iamuru na kutamka hivyo wakidai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.
Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa msingi huo, walalamikaji hao wanaomba Mahakama hiyo itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kwamba wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Vilevile wanaiomba Mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Amri nyingine wanazoomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.
Mbali na amri hizo vilevile wanaiomba Mahakama iamuru, wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona inafaa kuzitoa.