ULE uhondo wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) unatarajiwa kurejea upya kesho Ijumaa na Uwanja wa Donbosco Upanga kutakuwa na vita nzito kati ya Dar City dhidi ya KIUT.
Mchezo huo unasuburiwa kwa hamu na mashabiki wengi kuona kama KIUT yenye historia ya kufunga vigogo wa ligi, baada ya kuzifunga JKT kwa pointi 84-74 na UDSM Outsiders 68-58 kama itaweza kuizuia Dar City.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Denis Funganoti alisema wanaiheshimu Dar City kama timu kubwa isipokuwa hawaiogopi.
“Tumejipanga kucheza kwa nguvu na kasi kama tulivyocheza na JKT na UDSM, naamini tukifanya hivyo tutaivuruga,” alisema Funganoti.
Akizungumzia makosa waliyoyafanya katika michezo waliyopoteza, alisema ilitokana na dharau na kujiamini kwa wachezaji wake.
Alitaja baadhi ya michezo iliyopoteza ni pamoja na dhidi ya Kurasini Heat na Mchenga Star.
Ilifungwa na Kurasini Heat kwa pointi 68-58 na Mchenga Star kwa pointi 64-59, alisema katika michezo yote hawakustahili kufungwa kutokana na uwezo mkubwa walionao.
Katika mchezo wa leo Dar City inajivunia nyota wao, Ally Abdallah, Sharom Ikedigwe, Amin Mkosa, Jamel Marbuary na Haji Mbegu huku timu ya KIUT ikiwa na Rahim Ramadhani na Englibert Machumu.
Michezo mingine itakayochezwa leo, ni Kigamboni Queens na Polisi Stars, Tausi Royals na Ukonga Queens na wanaume itakuwa kati ya timu ya Pazi na Mchenga Star.
Timu ya Dar City inaongoza katika ligi hiyo kwa pointi 16, Pazi (15), ABC (14), Stein Warriors (14), JKT (13) na Savio (12).