Hati miliki za kimila 1,200 zatolewa Kishapu

Kishapu. Hati miliki za kimila 1,200 zimetolewa kwa wananchi wa vijiji vya Idukilo na Mwaduo Lohumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ikiwa ni juhudi za Serikali kutatua changamoto za migogoro ya mipaka ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji, pamoja na kuimarisha usalama wa miliki za ardhi.

Akizungumza leo Julai 10, 2025 wakati wa utoaji hati hizo,  Ofisa Mifumo kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, Jofrey Kakuru amesema lengo kuu la Tume hiyo ni kuhakikisha kila mwananchi anamilikishwa ardhi yake kwa mujibu wa sheria, ili kumuwezesha kuendesha maisha ya kiuchumi kwa utulivu na bila migogoro.

“Tunataka kuona wananchi wanakuwa na usalama wa miliki na kuondokana na migogoro ya mipaka ya ardhi, pia kupanga matumizi bora ya ardhi na hatimaye wanainuka kiuchumi kwa kutumia ardhi hiyo kama mtaji,” amesema Kakuru.

Mratibu wa timu ya matumizi bora ya ardhi ambaye pia ni ofisa ardhi mteule wa Wilaya ya Kishapu, Grace Pius ameeleza kuwa mpango huo umefanikiwa kutatua migogoro hasa kwa wananchi waliokuwa wakiishi karibu na maeneo ya mgodi, waliokuwa kwenye mgogoro wa mipaka na matumizi ya ardhi.

“Kupitia mipango hii ya matumizi bora ya ardhi, wananchi sasa wanaelewa ni maeneo gani ya makazi, kilimo, malisho au biashara na hivyo migogoro imepungua kwa kiwango kikubwa,” amesema Grace.

Msimamizi wa uandaaji wa hati za kimila, Edward Mpanda amewahamasisha wananchi wa vijiji vya Idukilo na Mwaduo Lohumbo kujitokeza kwa wingi wakiwa na nyaraka zao muhimu ili wapate hati miliki hizo bila kutozwa gharama yoyote.


“Shughuli hii ni bure, tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili wanufaike na mpango huu wa Serikali wa kuwapatia hati miliki za kimila ambazo zitawasaidia hata kupata mikopo kwa ajili ya kujiinua kiuchumi,” amesisitiza Mpanda.

Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa kijiji cha Ibukilo, Patrick Kapela ameeleza kuwa na matumaini ya kupungua na kuisha kabisa kwa migogoro ya ardhi iliyokuwa imekithiri kijijini hapo, pamoja na kutoa shukurani zake kwa Serikali.