Kambi yanga iko huku | Mwanaspoti

YANGA imebakiza hatua chache kumtangaza kocha mpya wa timu hiyo, lakini mezani kwa mabosi wao kuna nchi tatu zinataka kuona ufundi wa kwanza wa mtaalamu huyo wa ufundi.

Yanga inaelezwa imeshamalizana na kocha mpya wa kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyetimkia Ismailia ya Misri, huku jina la Julien Chevalier aliyekuwa Asec Mimosas ya Ivory Coast akitajwa, japo kumekuwa na usiri mkubwa kwa vile mabosi wanataka kufanya sapraizi kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Hata hivyo, hali ikiwa hivyo inaelezwa tayari mipango ya kambi mpya ya maandalizi ya msimu mpya imeshaanza na kuna nchi tatu zinaitaka Yanga, na hata mabosi wa klabu hiyo wamepanga kuchagua moja kwenda kuweka mambo sawa kabla ya msimu wa 2025-2026 kuanza baadaye.

Inadaiwa kuwa, mataifa hayo matatu yametuma mwaliko maalumu kwa Yanga yakitaka mabingwa hao wa Tanzania kwenda kuweka kambi maalumu ya kujiandaa na msimu mpya (pre season).

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga ambazo Mwanaspoti limejiridhisha ni kwamba mwaliko wa kwanza ni pale Kigali – Rwanda ambako imealikwa na Wananchi wenzao wa Rayon Sport.

Rayon Sport kitambo tu ilikuwa inapambana kuivuta Yanga Rwanda kwenda kucheza nayo mechi ya kirafiki.

Katika mwaliko huo Rayon imeihakikishia Yanga itaipatia nafasi ya kupata mazingira sahihi ya maandalizi ya msimu mpya pamoja na mechi za kirafiki huku mchezo mkubwa ukiwa dhidi yao utakaopigwa Agosti kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali.

Ukiondoa mwaliko huo wa Rwanda, pia klabu hiyo imeitwa kwenye ziara kama hiyo huko Namibia.

Mbali na maandalizi hayo Yanga itakuwa moja kati ya timu mwalikwa kwenye mashindano maalumu ambayo yatazishirikisha klabu za African Stars ambao ndio wenyeji huku Petro De Luanda(Angola) na Liolli FC (Lesotho) zikithibitisha kushiriki michuano hiyo.

Hesabu zingine kwa Yanga zilikuwa ni kwenda Afrika Kusini ambako msimu uliopita pia ilipata mwaliko na kutwaa Kombe la Toyota, lakini safari hii ikitaka kwenda yenyewe kwa hesabu zake.

Hata hivyo, kambi hiyo ya Afrika Kusini, inaweza kuota mbawa endapo mialiko ya Rwanda na Namibia ikiwavutia mabosi wa timu hiyo.

Bosi mmoja wa Yanga ameliambia Mwanaspoti,  kwamba bado haujafanyika uamuzi wa mwisho wa wapi wanakwenda ambapo sasa wanasubiri mchakato wa kocha mpya kuja kufanya uamuzi wa mwisho juu ya kambi ya maandalizi ya msimu ujao.

“Hayo maeneo yote ni sehemu sahihi lakini hatuwezi kufanya maamuzi sisi wenyewe tunasubiri kukamilika kwa mchakato wa kocha na baada ya hapo tutatangaza wapi tunakwenda,” alisema bosi huyo.

Kambi hiyo itakuwa ni eneo la kwanza kwa kocha huyo mpya kuonyesha ufundi wake mara baada ya kumalizana na klabu hiyo bingwa wa kihistoria nchini ikiwa ni siku chache tangu Hamdi kuondoka mara baada ya kuipa timu hiyo mataji mawili kwa mpigo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

Katika siku 148 alizokuwa Yanga kocha huyo aliiongoza timu hiyo kucheza mechi 21 na kushinda 19 na kutoka sare mbili, huku akitwaa nayo pia Kombe la Muungano.

Related Posts